Ulimwengu waomboleza kifo cha Pele
30 Desemba 2022Salamu za rambirambi zinaendelea kumiminika kutoka kila pembe ya dunia tangu ilipofahamika Alhamisi jioni kuwa Pele, mkongwe wa mchezo wa soka na moja ya wasakata kambumbu maarufu zaidi ulimwenguni amefariki dunia.
Salamu za pole na rambi rambi zimetoka kwa wanasiasa, wanamichezo, wanamuziki na watu wengine mashuhuri wote wakimtaja Pele, aliyekuwa mchezaji wa soka wa Brazil kuwa nyota isiyozimika.
Picha zake zimetandaa mbele ya kurasa za magazeti tangu mjini Rio de Janeiro kwenye ardhi ya taifa lake hadi mjini Berlin hapa Ujerumani.
Nyota wa kandanda wa Brazil Neymar amesema Pele "aliubadili mchezo wa soka kuwa Sanaa” huku kiungo mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe amesema urathi unaoachwa na Pele kwenye kabumbu "kamwe hautasahaulika”.
Kwa upande wake Cristiano Ronaldo wa Ureno amesema Pele "alikuwa mfano wa kuigwa kwa mamilioni ya watu”. Nahodha wa timu ya sokaya Argentina ambaye wiki mbili zilizopita ilinyakua kombe la dunia, Lionel Messi aliandika maneno mafupi tu ya kumwombea Pele "apumzike kwa amani”
Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino amesema "rikodi ya Pele haiwezi kuelezwa kwa ufupi kwa kutumia maneno” ujumbe ulioranda na ule wa rais wa shirikisho la soka barani Ulaya, UEFA, Aleksander Ceferin aliyemsifu Pele kwa umahiri uwanjani na hata kuendelea kuwa mtu maarufu sana baada ya kustaafu kucheza mpira wa miguu. Shirikisho la Soka nchini Ujerumani DFB limesema Pele ni "alama kwa vizazi vijavyo”.
Nahodha wa timu ya soka ya Brazil na mchezaji wa klabu ya Chelsea Thiago Silva amemwombea Pele apumzike kwa amani.
Wanasiasa nao wamwelezea Pele kama mfano wa kuigwa
Wanasiasa pia wameomboleza kifo hicho ambapo rais anayeondoka madarakani nchini Brazil Jair Bolsonaro amesema Pele "alifanya mchezo wa kandanda kuwa burudani ya kusisimua”. Mbali ya salamu hizo kiongozi huyo pia ametangaza siku tatu za maombolezo kufutia kifo cha mkongwe huyo wa soka.
Mwanasiasa wa mrengo wa shoto atakayeapishwa siku ya Jumapili kuwa rais mpya wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amesema "hapatotokea mchezaji mwingine yeyote wa soka mwenye kuvaa jezi namba 10 mgongoni” atakayekuwa Hodari uwanjani kumzidi Pele.
Rais wa Marekani Joe Biden naye pia ametuma salamu za pole akisema familia yake ilivutiwa sana na umahiri wa mchezaji huyo wa kandanda.
Ujumbe sawa na huo umetolewa vilevile na viongozi wengine wa dunia ikiwemo Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni, rais wa Ireland Michael D. Higgins na viongozi wa Argentina, Bolivia na rais wa zamani wa Marekani Barack Obama.
Wanamuziki mashuhuri wa Brazil Caetano Veloso na Gilberto Gil nao wametuma salamu za pole sambamba na mkuu wa kamati ya Olimiki duniani Thomas Bach.
Mwili wa Pele kuzikwa Jumanne ijayo huko Santos
Pele aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 82 ndiye mchezaji pekee wa soka kuwahi kunyakua makomba matatu ya dunia akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Brazil mnamo mwaka 1958, 1962 na 1970.
Kwa heshima ya mchezaji huyo anayefahamika nchini Brazil kama "Mfalme”, taifa hilo la Amerika Kusini linaanza hii leo siku tatu za maombolezo ya taifa kuenzi mchango wa Pele anayezingatiwa na wengi kuwa mchezaji bora zaidi katika historia ya mchezo wa soka duniani.
Ratiba ya mazishi yake nayo pia imetolewa. Pele atazikwa siku ya Jumanne katika mji alikozaliwa wa Santos katika tukio litakalohudhuriwa na familia yake na jamaa wengine wa karibu.
Klabu ya zamani FC Santos imesema mapema siku ya Jumatatu jeneza lenye mwili wa Pele linaondolewa kutokahospitali alikoaga dunia mjini Sao Paulo na kupelekwa kwenye mji huo wa mwambao kiasi umbali wa kilometa 80.
Kisha litawekwa kwenye uwanja wa klabu ya FC Santos ambapo waombolezaji watapata nafasi ya kutoa heshima za mwisho.