Ghasia za magenge ya wahalifu zaongezeka nchini Haiti
28 Septemba 2023Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyasema hayo katika ripoti yake mpya kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Amesema watu wapatao 2,728 wameorodheshwa kuuawa kimakusudi kati ya Oktoba mwaka jana wa 2022 na Juni mwaka huu miongoni mwao wakiwemo wanawake 247, wavulana 58 na wasichana 20.
Magenge hayo ya wahalifu pia yanaendelea kutumia unyanyasaji wa kijinsia ikiwa ni pamoja na ubakaji wa kundi la wahalifu dhidi ya mhanga mmoja kwa lengo la kuwatishia watu walio chini ya udhibiti wa magenge pinzani amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Ameelezea matukio 452 za ubakaji yaliorodheshwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba 2022 hadi mwezi Juni 2023. Guterres amesema karibu watu 130,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na ghasia za magenge hayo na hakuna hatua thabiti zilizofikiwa tangu lilipopitishwa azimio la Oktoba mwaka jana.
Amesema Haiti haina mfumo madhubuti wa mahakama unaoweza kushughulikia kesi zinazowakabili wahusika wa magenge hayo ya uhalifu na kwamba nguvu ya magenge hayo ni kubwa kuliko taasisi za kitaifa zilizo dhaifu.
Polisi wa Haiti wameshindwa kukabiliana na magenge yenye nguvu licha ya kuongezewa bajeti. Guterres amesema polisi ya Hiti pia inakabiliwa na upungufu wa wafanyakazi kutokana na baadhi yao kujiuzulu wengine wanastaafu na wengine wanauawa wakati wakiwa wanatimiza majukumu yao ya kazi.
Soma pia:Magenge yenye silaha nchini Haiti yataka serikali ipinduliwe
Katibu Mkuu Guterres pia amewasilisha ripoti kuhusu maendeleo katika kulitimiza azimio la Baraza la Usalama lililopitishwa Oktoba mwaka jana juu ya vikwazo dhidi ya kiongozi wa genge moja la wahalifu nchini Haiti.
Wakati huo huo wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wanalijadili azimio jipya la umoja huo juu ya kuidhinisha kikosi cha kimataifa ambacho hakitakuwa chini ya Umoja wa Mataifa.
Badala yake kitaongozwa na Kenya kwa ajili ya kulinda usalama na kupambana na magenge ya nchini Haiti. Wanadiplomasia wamesema azimio hilo litapigiwa kura baadaye wiki hii au wiki ijayo.
Chanzo: AP