Umoja wa Ulaya wapania kuimarisha ulinzi wa nchi wanachama
19 Julai 2022Umoja wa Ulaya umependekeza kutumia kiasi cha Euro milioni 500 kwa ajjili ya kununua silaha ili kuziba pengo lililotokana na silaha zilizotolewa kwa ajili ya kuisaidia Ukraine. Kamishna wa masoko ya ndani ya Umoja huo, Thierry Breton amesema inapasa kuliziba pengo hilo haraka. Kamishna huyo ameeleza juu ya mpango huo wa pamoja utakaofadhiliwa kutokana na bajeti ya Umoja wa Ulaya kwamba utazipa nchi wanachama motisha wa kuchangia zaidi. Amesema lengo la mradi huo ni kuimarisha ulinzi wa nchi za Umoja wa Ulaya.
Wakati hayo yakiendelea habari kutoka Ukraine zinasema mtu mmoja ameuawa kutokana na shambulio la kombora lililofanywa na majeshi ya Urusi katika mji wa Kramatorski wa mashariki mwa nchi hiyo. Taarifa hiyo imetolewa na gavana wa jimbo hilo Pavlo KyryLenko. Amesema shambulio hilo lilisababisha milipuko mikubwa na moto kwenye jengo la makaazi ya raia. Urusi haijesema chochote juu ya hali ya mji wa Kramatorski, tangu ilipoanza uvamizi nchini Ukraine tarehe 24 mwezi Februari.
Maafisa wa serikali wa Ukraine wamesema wanahofia kwamba mji wa Kramatorski uliokuwa na wakaazi 150,000 kabla ya uvamizi wa Urusi, utakuwa ni lengo kuu la mashambulio ya Urusi mashariki mwa nchi hiyo. Ukraine imesema majeshi ya Urusi yameongeza, mashambulio kwa kiwango kikubwa kwa kutumia makombora ya masafa marefu.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa kusisitiza ushirikiano wa karibu miongoni mwa serikali za ulimwengu katika mfumo wa ugavi duniani kuwa ni muhimu kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Kwa mujibu wa taarifa ya maafisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Blinken pia atasisitiza umuhimu wa kupunguza kutegemea nishati za gesi na mafuta kutoka nchi zisizoaminika na badala yake kuweka mkazo juu ya biashara ya bidhaa za nishati safi.
Na gazeti la Financial Times limeripoti juu ya tahadhari iliyotolewa na shirika la fedha la kimataifa IMF kwamba vikwazo dhidi ya gesi ya Urusi vinaweza kusababisha mdororo mkubwa wa uchumi katika nchi za Ulaya mashariki na Italia kwa zaidi ya asilimia 5 ikiwa nchi nyingine duniani zitahodhi akiba zao za nishati.
Shirika la IMF limetabiri kwamba uchumi wa nchi za Ulaya mashariki pamoja na Italia unaweza kunywea ikiwa hatua hazitachukuliwa ili kususia gesi kutoka Urusi, bila ya nchi kugawana gesi kioevu na bila ya kupunguza bei kwa njia bandia. Nchi hizo za Ulaya mashariki ni pamoja na Jamhuri ya Czech, Hungary na Slovakia.
Vyanzo:AFP/RTRE