Msumbiji: Upinzani watoa wito kuomboleza vifo vya watu 50
20 Novemba 2024Katika chapisho kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook, Mondlane ametaka pia kuhesabiwa upya kwa kura baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Daniel Chapo wa chama cha Frelimo kilichopo madarakani kwa karibu nusu karne kuwa mshindi.
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi anayetakiwa kuondoka madarakani mwezi Januari amelihutubia taifa siku ya Jumanne na kulaani "jaribio la kuanzisha machafuko katika nchi hiyo" huku akihimiza kufanyike mazungumzo ili kumaliza machafuko yaliyodumu kwa wiki kadhaa.
Viongozi wa SADC kujadili ghasia za Msumbiji
Hayo yanajiri wakati viongozi wa nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) watakutana siku ya Jumatano (20.11.2024) mjini Harare kwa mkutano unaotarajiwa kujadili machafuko nchini Msumbiji, miongoni mwa masuala mengine ya kikanda.
Mzozo wa kisiasa na kijamii unaozidi kuongezeka Msumbiji utakuwa ndio ajenda kuu ya mkutano wa kilele wa SADC ulioitishwa baada ya matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 9 kusababisha maandamano ya wiki kadhaa na kumfanya mgombea wa upinzani aliyeshindwa kupinga matokeo.
Soma pia: Mzozo wa kisiasa wa Msumbiji kutawala mkutano wa kilele wa SADC
Watu wasiopungua 30 wanaripotiwa kuuawa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi kufuatia ushindi wa mgombea wa chama tawala cha FRELIMO Daniel Chapo.
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane anayapinga matokeo hayo ambayo anadai kuwa yamechakachuliwa na kuitisha maandamano ya nchi nzima. Miito imekuwa ikitolewa ili kurejeshwa hali ya utulivu na utawala wa sheria nchini Msumbiji.