Upinzani Venezuela ulifanya mikutano ya siri na jeshi
31 Januari 2019Katika maoni yaliyochapishwa leo na gazeti la Marekani la New York Times, Guaido amesema hatua ya jeshi kuondoa uungaji mkono wao kwa Maduro ni muhimu katika kuwezesha mabadiliko ya serikali, na wengi wanaohudumu wanakubaliana kuwa matukio ya karibuni nchini humo hayakubaliki.
Guaido mwenye umri wa miaka 35, jana aliwaongoza maelfu ya waandamanaji wa upinzani mjini Caracas, akisema uamuzi wa mahakama ya juu nchini humo wa kumzuia kuondoka nchini humo haumpi wasiwasi wowote, akiongeza kuwa watu hawataki kuondoka nchini humo. Wanachotaka ni watu kurudi nchini humo.
Mamilioni ya Wavenezuela wamekimbia nchi hiyo tangu uongozi wa Hugo Chavez. Hali imezorota chini ya Maduro, ambaye ameshuhudia hali mbaya ya kiuchumi ambayo imesababisha mfumko wa bei kwa zaidi ya asilimia milioni moja.
Wakati huo huo, mamlaka nchini Venezuela zinawazuilia wanahabari watatu wa kigeni na dereva wanaofanya kazi na shirika la habari la Uhispania EFE, ikiwa ni katika tukio la karibuni la kukamatwa wanahabari wanaoripoti matukio yanayoendelea nchini humo.
Serikali ya Uhispania imelaani kukamtwa kwao na kuitaka Venezuela iwaachie huru maramoja. Kukamatwa kwao kunafuatia kutimuliwa nchini humo kwa maripota wawili wa Chile waliokamatwa wiki hii.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Venezuela Jorge Arreaza alisema kuwa wanahabari wanaingia nchini humo kinyume cha sheria. Katika ujumbe wake wa Twitter, waziri huyo alisema baadhi ya wanahabari walijaribu kuingia katika Ikulu bila kibali.
Mapema jana, Maduro alijaribu kuzungumza na wanajeshi, ambapo alikutana na karibu askari 2,500 katika mji mkuu akitoa wito wa umoja huku akiwakemea wale aliowaita mamluki jeshini.
Rais wa Marekani Donald Trump amemtambua Guaido kuwa kaimu rais, lakini Umoja wa Ulaya bado haujafanya hivyo. Ujerumani na mataifa kadhaa ya Ulaya yamempa Maduro muda wa mwisho, wakisema watamuidhinisha Guiado kuwa kiongozi kama hatoitisha uchaguzi wa huru na haki ifikapo Jumapili hii.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/Reuters/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga