Uchina yaikosoa Marekani kuhusu Venezuela
22 Mei 2018Swali linaloulizwa ni kitakachofuatia baada ya Marekani kuimarisha vikwazo na kuzitaka nchi nyengine za Amerika Kusini kuususia utawala huo wa Maduro.
Maduro, aliye na umri wa miaka 55-aliyemrithi mwanasiasa wa mrengo wa kushoto Hugo Chavez, alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 68 ya kura zilizopigwa, huku kiongozi huyo akiuita ni ushindi dhidi ya "ukoloni mambo leo."
Marekani yaiweikea Venezuela vikwazo
Lakini upinzani ulishikilia kuwa mazingira ya uchaguzi huo hayakuwa huru na haki na kuwataka wafuasi wake kuususia. Takwimu rasmi zinaonesha kuwa idadi ya watu waliojitokeza ilikuwa asilimia 46 na wakosoaji wanasema kuwa idadi hiyo ilikuwa ndogo ikilinganishwa na asilimia 80 mwaka 2013.
Upinzani ulituma picha kwenye mtandao wa Twitter ukionesha vituo vya kupigia kura visivyo na watu na kufurahia hatua ya Marekani na washirika wake wa kulaanini uchaguzi huo. Hata hivyo Uchina imeikosoa Marekani kuhusu hatua za kuiwekea Venezuela vikwazo baada ya Maduro kuchaguliwa. Maduro anazitegemea Uchina na Urusi ambazo zimetoa mabilioni ya fedha kulifadhili taifa hilo katika miaka ya hivi karibuni.
Ukosefu wa kuzingatia sheria kama vile kuwashinikiza wafanyikazi wa umma kumuunga mkono Maduro na kuahidi zawadi kwa wale watakaompigia kura, kuliufanya upinzani kujiondoa kwenye uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa rais wa muungano wa upinazini Omar Barboza, "wapinzani sasa watashinikiza kufanyika kwa uchaguzi huru mwishoni mwa mwaka huu." Lakini hatua ya Tume ya Uchaguzi ya taifa hilo kumtangaza Maduro mshindi, inaweza kuufanya upinzani usifanikiwe katika azma yake hiyo.
Alipoulizwa nini kingine ambacho upinzani unapanga kufanya, alisema, "hatua nyingine atazitangaza baadaye" na kuelezea, "malengo yake ya kuleta mageuzi ya kisiasa kwa kuzingatia katiba."
Umoja wa Mataifa una wasiwasi
Umoja wa Mataifa umesema kuwa unawasiwasi kuhusu hali ilivyo katika taifa hilo. Kwenye taarifa yake Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres, iliyosomwa na msemaji wake Stephane Dujaric alisema, "Katibu mkuu anafahamu matokeo ya uchaguzi wa urais wa Venezuela. Bila shaka katibu mkuu ana wasiwasi kuhusu hali ilivyo pamoja na changamoto kuu zinazoendelea kuathiri maisha ya watu. Anatoa wito kwa wahusika wote kuangazia changamoto hizo kwa dharura wakizingatia sheria na haki za binadamu."
Kwa raia wa kawaida wa Venezuela, wanahisi kuwa wapinzani wa Maduro hawana njia nyingine ya kumkabili rais huyo.
Wafuasi wa upinzani walikuwa wamejawa na matarajio baada ya muungano huo kushinda kwenye uchaguzi wa bunge mwaka 2015. Ushindi huo ulifutwa baada ya mahakama ya Juu kuondoa mamlaka ya bunge hilo.
Wakati muungano huo ulipopanga kura ya maoni dhidi ya Maduro mwaka 2016,mamlaka hiyo akalizima jaribio hilo ukidai kuwa sahihi ambazo zilikusanywa zilikuwa bandia.
Marekani inaongoza kampeni ya nchi kadhaa za Amerika Kusini, kuususia utawala wa Maduro, hatua ambayo imeshambuliwa vikali na Kiongozi huyo. Miongoni mwa nchi zinazomuunga mkono maduro katika kanda hiyo ni El Salvador.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman