Urusi, China zamkingia kifua Maduro
22 Februari 2019China imetamka hadharani hivi leo (Ijumaa, 22 Februari) ikipinga hatua yoyote inayoweza kuzusha ghasia na machafuko nchini Venezuela. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Beijing asubuhi ya leo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Geng Shuang, amesema nchi yake inafahamu kuwa pamekuwepo na hatua za makusudi za uchokozi dhidi ya serikali ya Venezuela, licha ya serikali hiyo kujizuwia kujibu uchokozi huo.
"Tumeona kwamba kipindi sasa serikali ya Venezuela imejizuwia na imejitolea kudumisha amani na utulivu wa ndani ya nchi, hali ambayo imewezesha kuzuwia umwagikaji damu mkubwa. Lakini kama kile kinachoitwa misaada ya kibinaadamu kitalazimishwa kuingia ndani ya Venezuela, ni wazi kuwa kutazuka machafuko yatakayokuwa na matokeo mabaya kabisa," alisema Shuang, akiongeza kuwa nchi yake inapingana na uingiliaji kati kijeshi dhidi ya Venezuela na pia inakataa vitendo vyovyote ambavyo vitachochea machafuko.
Kauli kama hii imetolewa pia na Urusi, ambayo nayo kupitia msemaji wake wa mambo ya kigeni, Maria Zakharova, imesema inafahamu kuwa Marekani inaandaa uchokozi ikitumia kanuni za hali ya juu za sayansi ya kijeshi.
"Vikosi maalum vya jeshi la Marekani na vifaa vinatumwa karibu sana na mpaka wa Venezueal. Kuna taarifa kwamba kampuni za Kimarekani na washirika wao wa Jumuiya ya NATO wananunuwa kiwango kikubwa cha silaha kutoka moja ya nchi za Ulaya Mashariki kwa ajili ya kuwafikishia wapinzani ndani ya ardhi ya Venezuela," alisema Zakharova, akiongeza kuwa kile kinachoitwa misaada ya kibinaadamu inayopangwa kuingizwa nchini Venezuela mwanzoni mwa mwezi ujao wa Machi, kitakuwa ni sehemu ndogo tu ya matumizi ya kibinaadamu, huku sehemu kubwa zikiwa zana za kijeshi.
Haya yanakuja huku Marekani ikiimarisha shinikizo lake dhidi ya serikali ya Venezuela, nayo serikali ya Rais Maduro ikiamuru kufungwa mpaka kati ya nchi hiyo na Brazil.
Kwenye hotuba yake ya mwanzoni mwa wiki kwa jamii ya Wavenezuela wanaoishi nchini Marekani, Rais Donald Trump alisema Marekani inataka pawepo na ukabidhianaji wa amani wa madaraka nchini Venezuela lakini hakuondosha uwezekano wa hatua za kijeshi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga