Urusi: Kombora dhidi ya Ukraine onyo kwa nchi za Magharibi
22 Novemba 2024Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov ameyasema hayo Ijumaa siku moja baada ya Rais Putin kusema kuwa jeshi lake liliishambulia ngome ya kijeshi ndani ya Ukraine kwa kutumia kombora jipya la masafa marefu aina ya Oreshnik.
Akizungumza na wanahabari, Peskov amesema kuwa ujumbe mkuu wa shambulio hilo ni kuwa maamuzi ya kizembe na hatua za mataifa ya magharibi yanayozalisha makombora na kuyapeleka Ukraine na kutumiwa dhidi ya Urusi, haziwezi kukaliwa kimya.
Soma zaidi: Putin aonya kuwa vita vya Ukraine vinachukua mkondo wa kidunia
Amefafanua kuwa Urusi haina wajibu wa kuitahadharisha Marekani kuhusu shambulio hilo lakini iliamua kuitaarifu dakika 30 kabla ya kushambulia. Peskov amesema Rais Putin bado yuko tayari kwa mazungumzo ya usuluhishi ingawa alibainisha kwamba utawala wa Rais wa Marekani anayemaliza muda wake unapendela kuendelea na hatua ya kuuchochea mvutano huo.
Putin alisema Alhamisi kuwa Urusi ilirusha kombora lake jipya baada ya Ukraine kuishambulia Urusi kwa kutumia kombora la masafa marefu la Marekani aina ya ATAMCMS baada ya utawala wa Biden kuidhinisha hatua hiyo. Alidai pia kwamba makombora ya Uingereza aina ya Storm Shadow yalitumika kuishambulia nchi yake.
Kwa upande wake Rais wa Ukrainie Volodymyr Zelenskiy amesema kitendo cha Urusi kutumia kombora la kisasa kuishambulia nchi yake yanazidi kuchochea vita na kuwa kinapaswa kulaaniwa na dunia nzima.