Urusi yadai kutwaa maeneo zaidi ya Bakhmut
23 Aprili 2023Mapigano ya kuwania udhibiti wa mji huo yamegeuka kuwa mojawapo ya makali sana ndani ya kipindi cha miezi 14 cha uvamizi wa Urusi, ambapo mashahidi wanasema mji huo wa mashariki mwa Ukraine takribani umesalia magofu matupu kutokana na makombora na mizinga ya Urusi.
Urusi inasema kuutwaa mji huo kutaiwezesha kuimarisha mashambulizi makubwa zaidi ndani kabisa ya maeneo ya mashariki mwa Ukraine.
Endapo watafanikiwa, wanajeshi wa Moscow wana uwezekano mkubwa zaidi wa kukabiliwa na mapigano ya mitaani kuelekea miji ya karibu ya Kramatorsk na Sloviansk.
Soma zaidi: Marekani, Ufaransa zaapa kuiwajibisha Urusi kwa vita Ukraine
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema siku ya Jumapili (Aprili 23) kwamba vikosi vyake vya ardhini wilaya mbili zaidi za magharibi mwa Bakhmut na kwamba vikosi vya anga vinaongeza kampeni yake maeneo ya kaskazini na kusini mwa Ukraine.
Yevgeny Prigozhin, mkuu wa kikosi cha kampuni ya kijeshi ya Wagner ambacho kinaongoza mashambulizi hayo, amesai kwamba vikosi vyake vinadhibiti 80% ya Bakhmut, ingawa mara kadhaa Kyiv imekuwa ikikanusha madai kwamba vikosi vyake vinajipanga kujiondowa kwenye mji huo.
Urusi yakanusha kuwepo kwa wanajeshi wa Ukraine
Kwa upande mwengine, mkuu wa jimbo la Kherson anayeelemea upande wa Urusi, alikanusha siku ya Jumapili ripoti za taasisi moja ya wataalamu ya Marekani kwamba wanajeshi wa Ukraine wametwaa maeneo yanayopakana na kingo za Mto Dnipro ulioko mashariki mwa nchi hiyo.
"Hakuna hata unyayo wa adui uliosalia kwenye upande wa mashariki wa Mto Dnipro.... Jeshi letu linalidhibiti eneo hilo kikamilifu," aliandika Vladimir Saldo kupitia chaneli yake ya Telegram, akiongeza kwamba kunaweza kuwapo matukio ya makundi yanayofanya hujuma kujipiga picha za "selfie... kabla ya kuangamizwa ama kusukumwa mtoni na wapiganaji wetu."
Soma zaidi: Urusi yateka wilaya tatu Ukraine
Ikiwanukuu waandishi wa blogu za masuala ya kijeshi wa Urusi waliomo ndani ya vikosi vya Moscow, Taasisi ya Utafiti wa Vita ilisema Ukraine imeweza kuchukuwa maeneo kwenye ukingo wa mashariki wa mto huo, ingawa haikuwa wazi "kwa kiwango gani wala kwa dhamira gani."
Msemaji wa kamandi ya kijeshi ya kusini mwa Ukraine hakukanusha wala kuthibitisha ripoti hiyo na badala yake alitowa wito wa kile alichosema ni "ukimya wa taarifa" ili kuilinda operesheni ya usalama.
Vyanzo: Reuters, AFP