Urusi yatafuta muujiza, Messi na Ronaldo nje
1 Julai 2018Wakati wenyeji Urusi wakijitayarisha kuvaana na Uhisoania , Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wameyaaga mashindano.
Michezo mingine ya kundi la timu 16 zilizobakia katika fainali hizi zinawakutanisha timu ya Croatia yenye wachezaji wenye vipaji wakiongozwa na Luka Modric, timu ambayo ina rekodi safi katika awamu ya makundi ikicheza dhidi ya Denmark, lakini watahitaji kupata uchawi uliofanyika katika kasheshe iliyotokea katika michezo ya kwanza ya awamu hii ya mtoano jana Jumamosi.
Ufaransa iliipiga mweleka Argentina kwa mabao 4-3 katika pambano kali la kombe la dunia, wakati kijana wa miaka 19 Kylian Mbappe alijitangaza katika medani hii kubwa ya dunia kwa kupachika ambao mawili na Le Bleus waliwarejesa nyumbani makamu bingwa wa dunia wa mwaka 2014.
Mbappe alikuwa kijana wa kwanza kufunga mabao mawili katika fainali za kombe la dunia tangu pale Pele akiwa na umri wa miaka 17 alipofunga katika fainali za mwaka 1958.
Mchezaji huyo mkongwe wa Brazil aliandika katika ukurasa wa Twitter akimzungumzia Mfaransa huyo: "Hongera kwa Mbappe, mabao 2 katika kombe la dunia kwa kijana mdogo namna hiyo yanakuweka katika kundi la wakubwa."
Messi na Ronaldo washindwa kufunga katika awamu ya mtoano
Messi hata hivyo alishindwa kufumania nyavu, akiondoka nchini Urusi akiwa na bao 1, na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 anayechezea klabu ya Barcelona huenda amekwisha tanabahi kuwa hakuna tena nafasi ya kushinda kombe la dunia.
Baadaye mjini Sochi, Ronaldo, ambaye alianza kombe la dunia kwa kufunga mabao 3 dhidi ya Uhispania, hakuna na uwezo tena kuizuwia Ureno kuteleza nje ya mashindano hayo wakati Edinson Cavani alipotundika mpira mara mbili wavuni katika ushindi wa mabao 2-1 na kuwarejesha mabingwa hao wa bara la Ulaya nyumbani.
Cavani , ambaye huchezea timu moja na Mbappe katika klabu ya Paris Saint-Germain, alifungua kitabu cha mabao akiruka juu na kuuweka mpira wavuni kabla ya kufunga kwa ustadi mkubwa akimwacha mlinda mlango Rui Patricio akishindwa kufanya lolote kuzuwia mkwaju huo na kuwa bao la ushindi katika mchezo huo baada ya Pepe kusawazisha hapo kabla.
Licha ya kwamba mchezaji huyo wa Uruguay alichechea wakati akitoka uwanjani kwa maumivu , baadaye alisema aligongwa tu na anatarajia kurejea uwanjani kupambana na ufaransa katika robo fainali.
Ronaldo atakuwa na umri wa miaka 37 wakati fainali nyingine za kombe la dunia zitakapofanyika nchini Qatar, lakini hakutaka kuingizwa katika mjadala iwapo anapanga kuachia ngazi katika timu ya taifa.
"Huu si wakati wa kuzungumzia juu ya hatima yangu na makocha," alisema Ronaldo, ambae, kama Messi , anaondoka katika fainali za kombe la dunia akiwa hajafunga bao katika awamu ya mtoano.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Zainab Aziz