Usitishwaji mapigano washuhudiwa Idlib
6 Machi 2020Wakazi na vikosi vya upinzani wamesema kuna hali ya utulivu angani iliyoshuhudiwa kwa mara ya kwanza baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi kwenye ngome hiyo ya mwisho ya waasi nchini Syria, ingawa bado kuna hali ya wasiwasi.
"Tunatumai kwamba makubaliano haya yatakuwa msingi mzuri wa kusitisha mapigano mkoani Idlib, na kuhitimisha mateso ya raia na kusambaa kwa mzozo wa kiutu. Utatengeneza mazingira ya muendelezo wa mchakato wa amani katika taifa hilo, kati ya pande zote zinazozozana." Ni Putin huyo akizungumza baada ya kuingia makubaliano hayo ya kusitishwa mapigano.
Ni rais wa Urusi, Vladimir Putin baada ya kufikiwa kwa makubaliano na Uturuki ya kusitisha mapigano jana jioni kufuatia masaa sita ya majadiliano mjini Moscow ya kuudhibiti mzozo huo wa Idlib uliosababisha maelfu ya raia kuyakimbia makazi yao, katika eneo hilo la kaskazinimagharibi mwa Syria.
Urusi na Uturuki ambayo ni mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO wanaunga mkono pande tofauti kwenye vita hivyo vya Syria vilivyodumu kwa miaka tisa sasa. Urusi inamuunga mkono rais Bashar al-Assad na Uturuki ikiwasaidia waasi na wawili hao wakijikuta wakikaribiana zaidi kwenye mzozo huo katika wiki za karibuni.
Makubaliano kadhaa yaliyofikiwa ya kumaliza mapigano Idlib yalivunjwa. Wachambuzi na raia wanasema wanahofu hata makubaliano haya ya mwisho pia yatavunjwa kwa kuwa kwa namna yoyote ile hayakuzungumzia mzozo wa kiutu wala ulinzi wa anga.
Wito watolewa wa marufuku ya kuruka ndege anga ya Idlib.
Waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi alipokuwa akiwasili kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, mjini Zagreb nchini Croatia amesema makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yanatakiwa kuongezwa nguvu kwa marufuku ya kuruka ndege katika eneo hilo la Idlib ili kuzuia mashambulizi zaidi ya hospitali.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kufuatia makubalino hayo kwamba wataendeleza kazi waliyoianza kwa kuzingatia makubaliano ya Sochi na hali ya kisiasa nchini Syria.
Chini ya makubaliano hayo kutaundwa eneo la kiusalama katika barabara kuu ya M4, kaskazini mwa Syria , ambako vikosi vya Urusi na Uturuki vitaanzisha doria ya pamoja ifikapo Machi 15. Vikosi hivyo vya doria vitalinda maeneo kati ya mji wa Tronba na Idlib na kijiji kilichopo mkoa wa Latakia, ambako ni ngome ya serikali. Huu ni ushirikiano wa mwanzo kabisa kati ya wanajeshi wa Urusi na Uturuki huko Idlib.
Soma zaidi:Guterres atoa wito mapigano yasitishwe Idlib
Huku hayo yakiendelea, maafisa wa usalama nchini Ugiriki wamelazimika kutumia gesi ya kutoa machozi na mabomba ya maji kuzuwia jaribio la wahamiaji kushinikiza kuvuka mpaka wakitokea Uturuki mapema hii leo, huku maafisa wa Uturuki pia wakifyatua mabomu ya machozi kuelekea upande wa mpaka wa Ugiriki.
Maelfu ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Uturuki wamekuwa wakijaribu kuingia Ugiriki kupitia mipaka ya ardhini na baharini mashariki mwa nchi hiyo, baada ya Uturuki kutangaza kuifungua mipaka yake na Ulaya.
Mashirika: AFPE/APE/RTRE