Jeshi lamzuia Mwanadiplomasia wa Marekani kumuona Bazoum
9 Agosti 2023Mazungumzo hayo yamefanyika huku mshauri wa Bazoum akieleza kuwa kiongozi huyo wa zamani na familia yake imewekwa katika mazingira magumu kizuizini.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema Antony Blinken na Rais Mohamed Bazoum wamejadili juu ya ziara ya hivi karibuni ya mwanadiplomasia huyo wa Marekani mjini Niamey na kwamba bi Victoria Nuland ameelezea msimamo wa Washington wa kuunga mkono suluhu ambayo itairudisha Niger katika utawala wa kidemokrasia.
Katika ziara hiyo, mwanadiplomasia huyo wa Marekani pia amesisitiza umuhimu wa usalama wa Rais Bazoum na familia yake akiwemo mkewe na mwanawe wa kiume.
Soma pia: ECOWAS kuwawekea vikwazo watawala wa kijeshi Niger
Mnamo siku ya Jumatatu, Nuland alisafiri hadi mji mkuu wa Niger, Niamey na kufanya mazungumzo ya "wazi na magumu" na viongozi wakuu wa kijeshi.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Nuland amesema viongozi wa kijeshi hawakutilia maanani mapendekezo ya Marekani ya kujaribu kurejesha utaratibu wa sheria na kwamba ombi lake la kutaka kukutana na Rais Bazoum lilikataliwa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matt Miller amesema, "Bado tuna matumaini na tunajaribu kupata matokeo ambayo ni kurejea kwa utaratibu wa kikatiba. Tunatumai hatufikia hatua ambapo tunahitaji kufanya maamuzi magumu kwa sababu matarajio yetu ni kuona utaratibu wa kikatiba umerejeshwa. Hatuamini kwamba milango imefungwa kwa wakati huu, lakini ni hali inayobadilika sana."
Bazoum amewekwa kizuizini katika makaazi yake tangu Julai 26, siku yaliyofanyika mapinduzi ya kijeshi. Juhudi za kidiplomasia za kuwashawishi viongozi hao wa kijeshi kumrejesha madarakani Rais Bazoum zimegonga mwamba.
Bazoum azuiliwa katika mazingira magumu
Wakati hayo yanaripotiwa, mshauri wa Rais Bazoum ameliambia shirika la habari la AP kuwa kiongozi huyo wa zamani anaishiwa na chakula na kwamba anapitia hali zinazozidi kuwa mbaya wiki mbili tu baada ya kung'olewa madarakani.
Mshauri huyo amedai kuwa familia ya Bazoum inaishi bila ya umeme na kwamba analishwa wali na vyakula vya mikebe pekee.
Kwa mujibu wa mshauri huyo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwani hajaidhinishwa kuzungumza na vyombo vya habari juu ya suala hilo, ameongeza kuwa Bazoum yu bukheri wa afya kwa sasa na kusisitiza kuwa, kamwe hatojiuzulu.
Chama cha kisiasa cha Bazoum pia kimetoa taarifa kuelezea mazingira magumu anayopitia kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 63 na kwamba familia yake imekosa maji.
Ama kwa upande mwengine, Kiongozi wa zamani wa waasi na mwanasiasa nchini Niger ameanzisha vuguvugu linalopinga utawala wa kijeshi, ishara ya kwanza ya upinzani wa ndani dhidi ya utawala huo.
Rhissa Ag Boula amesema katika taarifa iliyoonekana leo kuwa, baraza lake jipya la upinzani la CCR linalenga kumrejesha madarakani Rais Mohamed Bazoum.
Upinzani wa Ag Boula unaibua wasiwasi wa kutokea mzozo wa ndani nchini Niger, ambayo ni mzalishaji mkuu wa madini ya urani na pia yenye mamia ya wanajeshi wa kulinda amani kutoka Marekani na Mataifa ya Magharibi kama sehemu ya juhudi za kimataifa kupambana na waasi katika ukanda wa Sahel.